Ijumaa, 6 Aprili 2018

DK. SEMAKAFU AZUNGUMZIA HAKI ZA MTOTO


Serikali ya awamu ya Tano  imesema katika kulinda haki za mtoto imedhamiria kujenga shule za Elimu Jumuishi na zile za  wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika kila mkoa.

Kauli hiyo imetolewa na  Naibu Katibu Mkuu wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave maria Semakafu jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa wadau unaojadili haki za mtoto.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave maria Semakafu akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau kuhusu haki za mtoto, mkutano ambao umefanyika jijini Dar es salaam.

Dk. Semakafu amesema lengo la ujenzi wa shule hizo ni kuhakikisha watoto wote wa kitanzania wapata Elimu bila vikwazo vya aina yoyote kwani Elimu ni msingi wa Maenedeleo.

Amesema katika kutekeleza hilo tayari Wizara hiyo inajenga shule ya mfano kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika chuo cha Ualimu Patandi kilichopo mkoani Arusha, ambapo shule hiyo itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi wa shule ya msingi mpaka Sekondari.
Wageni waalikwa katika meza kuu wakifuatilia majadiliano kupitia jukwaa la kutetea haki za mtoto.

Naibu Katibu Mkuu huyo amewataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wote wenye umri wa kwenda shule bila kuangalia changamoto za kimaumbele walizonazo watoto wao kwa kuwa tayari Serikali imewekeza katika eneo hilo.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano unaojadili haki za mtoto wakisikiliza kwa makani hotuba ya Naibu katibu Mkuu Dk. Semakafu (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano huo jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa UNICEF katika masuala ya Elimu nchini Tanzania Cecilia Baldeh amesema tayari Tanzania imekwisha piga hatua katika kulinda na kutetea haki za mtoto ikiwa ni pamoja na Serikali kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanakwenda kwa kuwa Elimu msingi hivi sasa inatolewa bure.
Wawakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimatifa la nchini Sweden, SIDA wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu kabla ya kufungua mkutano wa wadau wa ndani na nje ya nchi unaojadili haki za mtoto.





Jumatano, 4 Aprili 2018

Waziri Ndalichako: Kila jambo linautaratibu wake katika kulitekeza


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Profesa Joyce Ndalichako amelitaka shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa Shule nchini –TAMONGSCO kuwa na mtazamo chanya wanapotekekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuelewa kuwa kila Jambo linautaratibu wake katika kulitekeleza.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifungua mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo ambapo amesisitiza kuwa Elimu ni kitu muhimu na hakiwezi kuendeshwa bila kufuata utaratibu, kusisitiza kuwa hata uendeshaji wa shule una taratibu zake.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa  ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa shule (TAMONGSCO) uliofanyika Mjini Dodoma .
Profesa Ndalichako aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa Serikali haiwezi kuweka vikwazo na vizuizi kwa wadau wake wa Elimu, kwa kuwa lengo ni kuhakikisha Elimu bora inatolewa kwa manufaa ya Taifa.


“Hata siku moja Serikali haiwezi kuweka vikwazo na vizuizi kwa wadau ambao kwa namna moja ama nyingine wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono  juhudi zinazofanywa na serikali, Pia Serikali inatambua thamani na mchango unaotolewa na sekta binafsi katika Elimu,
 “Hivyo sioni kuwa  ni sahihi kwenu nyinyi TAMONGSCO kuja na kauli mbiu inayosema kuwa  “ Kwa nini vikwazo na vizuizi katika shule na Taasisi zisizo za Serikali,”alisema Waziri Ndalichako.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamilki wa Shule (TAMONGSCO) wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ambaye hayupo pichani wakati akifungua Mkutano huo.   

Waziri Ndalichako pia amewataka Mameneja na Wamiliki hao wa shule kuwa wazalendo kwa kutoa kipaumbele katika kuajiri walimu wa Kitanzania, kabla ya kufikiria wageni.

Amesema ili kuunga mkono kauli mbiu ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda ni vyema wawekezaji wakawekeza zaidi kwenye eneo la ufundi stadi, ikiwa ni pamoja na mafunzo yanayotolewa kuendana na soko la ajira.

Kwa upande wao TAMONGSCO wameeleza kuwa lengo la mkutano wao ni kujadiliana kwa pamoja mafanikio na changamoto mbalimbali zilizopo katika sekta ya Elimu ili kuzipatia ufumbuzi wa pamoja.

Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa Shule (TAMONGSCO) William Magero akikabidhi risala kwa Mgeni Rasmi katika mkutano Mkuu wa shirikisho hilo  uliofanyika Mjini Dodoma

Jumanne, 3 Aprili 2018

Dk. Semakafu afanya mazungumzo na Kampuni ya Kichina itakayosimamia ujenzi wa VETA, Mkoani Kagera


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) ambayo inatarajia kusimamia ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi, VETA cha Mkoa wa KAGERA.

Mazungumzo hayo yamefanyika leo katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo UDOM mkoani Dodoma ambapo kwa pamoja wamejadiliana hatua za awali za Ujenzi wa chuo hicho na kuwa tayari kampuni hiyo imekwisha andaa michoro ya namna chuo hicho kitakavyokuwa huku wakisisitiza kuwa ujenzi huo utafanyika kwa awamu mbili.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akifanya majadiliano kuhusu ujenzi wa VETA mkoani KAGERA
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu Msaidizi wa kamapuni hiyo Fang Kefang amemweleza Dk. Semakafu kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi huo itachukua miezi 18 na majengo yatakayojengwa yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi mia nne (400).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza na Meneja Mkuu Msaidizi wa Idara ya Usanifu Majengo wa Kampuni ya Ujenzi ya Kichina (CHINA QIYUAN ENGINEERING CORPORATION) Fang Kefeng, Kampuni inayotarajiwa kusimamia ujenzi wa Chuo Cha Ufundi Stadi, VETA cha Mkoa wa Kagera.



Jumanne, 27 Machi 2018

Wizara ya Elimu yawasilisha Taarifa ya Utekelezaji, Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2018/19 kwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha Taarifa ya Utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2017/18 na Makadirio ya Bajeti kwa mwaka 2018/19 kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Uwasilishaji wa taarifa hiyo umefanyika leo katika ofisi za Bunge zilizopo Mkoani Dodoma ambapo wajumbe wa Kamati hiyo wamepata fursa ya kupitia na kujadili Fungu 46. 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Pro.Joyce Ndalichako  akifafanua jambo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji  2017/18 na Makadirio ya Bajeti kwa Mwaka 2018/19 kwenye Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.


Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Juma Nkamia akisitiza jambo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ya utekelezaji na Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018/19 Mkoani Dodoma.

Wajumbe wa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa Taarifa ya utekelezaji na Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2018/19.

Alhamisi, 15 Machi 2018

Maafisa Habari wa Serikali watoa msaada kwa Shule ya Laibon


Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali Leo wamekabidhi msaada wa Vitabu, Madaftari, kalamu na Matanki mawili ya kuhifadhia maji katika Shule ya Msingi Laibon iliyopo mkoani ARUSHA.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Chama Cha Maafisa hao- TAGCO, Pascal Shelutete amesema lengo ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali za kutoa Elimu bure.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Rashid Njarita ameshukuru kupokea msaada huo ambapo amesema matanki ya maji yataondoa changamoto ya maji iliyokuwepo shuleni hapo.

Msaada uliotolewa unathamani ya shilingi milioni mbili na laki tano.

Mwenyekiti wa Chama Cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali - TAGCO, Pascal Shelutete akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Laibon Rashid Njarita Madaftari kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.
Maafisa hao wa Mawasiliano wanashiriki kikao kazi ambacho kinalenga kujengeana uwezo wa namna bora ya kutangaza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.


Kikao hicho kimeanza Machi 12 na kitamaliza Machi 16, 2018 huku kauli mbiu ya mkutano huo inasema Je? Mawasiliano ya kimkakati yanachagiza Vipi Tanzania ya Viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abass akimkabidhi daftari mmoja wa wanafunzi wa shule ya Msingi Laibon iliyopo mkoani Arusha.



Ijumaa, 9 Machi 2018

Naibu Waziri Ole Nasha asisitiza uadilifu na utunzaji wa siri za ofisi.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amewataka watumishi wapya wa Wizara hiyo kuwa waadilifu katika utendaji kazi pamoja na kutunza siri katika maeneo wanayofanyia kazi.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa rai hiyo mjini Dodoma wakati wa akifunga mafunzo kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo, mafunzo ambayo yamelenga kuwakumbusha taratibu, sheria na miongozo ya kazi inayotakiwa katika utumishi wa umma.

Naibu Waziri huyo amesema anaamini mafunzo yaliyotolewa yatawawezesha kuwa watumishi bora wa umma ambao wanafahamu vema mipaka ya kazi, taratibu za kiutumishi lakini pia haki na wajibu katika utendaji kazi.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Mhe.William Ole Nasha akifunga mafunzo ya watumishi wapya wa Wizara hiyo ambapo amewataka kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma,ikiwa ni pamoja na kutunza Siri za ofisi.

Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara hiyo Moshi Kabengwe kuandaa utaratibu wa mafunzo kwa watumishi wengine wa Wizara hiyo ili kuwakumbusha taratibu, kanuni na miongozo kwa lengo la kuepuka ukiukaji wa maadili na pia kuleta chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi miongoni mwa watumishi.


Nae mmoja wa watumishi aliyeshiriki mafunzo hayo Lazaro Julius kutoka Ofisi ya Kamishna wa Elimu wa Wizara hiyo amesema mafunzo hayo ni muongozo thabiti katika kutekeleza majukumu ya kazi za kila siku katika utumishi wa umma ambapo ameahidi kuzingatia na kutekeleza yote yaliyoelekezwa.

Mafunzo  kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo yamefanyika kwa siku Nne kuanzia Machi 6, na yameshirikisha waajiriwa wapya kutoka wizara ya Elimu Makao Makuu na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Watumishi wapya wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakifuatilia mafunzo Maalumu ya namna wanavyotakiwa kutekeleza majukumu yao katika Utumishi wa Umma ambayo yamefanyika mkoani Dodoma.