Jumapili, 27 Mei 2018

ZAIDI YA BILIONI NNE KUTUMIKA KWENYE MIRADI YA UTAFITI.


·         WAZIRI NDALICHAKO ASISITIZA KUWA ZISITUMIKE VINGINEVYO

Serikali imetoa zaidi ya bilioni nne kwa ajili ya Taasisi na Watafiti walioshinda maandiko ya miradi 8 ya utafiti ambayo itaanza kufadhiliwa mwaka huu wa fedha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam kabla ya kukabidhi hundi kwa Taasisi zilizoshinda fedha hizo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa. Joyce Ndalichako amesema miradi yote iliyopata fedha ni ile ambayo ina malengo madhubuti ya kuimarisha uchumi wa viwanda hadi ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako amesema kufadhiliwa kwa miradi hiyo nane kutaleta mchango mkubwa wa uzalishaji wa dawa nchini na kupunguza uagizwaji wa dawa kutoka nje, uboreshaji wa maabara za uhandishi jeni, kuongeza ushindani wa bidhaa, kuongeza uzalishaji wa mazao, uzalishaji wa mimea, pamoja na kuchangia katika uanzishwaji wa viwanda.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi hundi kwa Taasisi na Watafiti walioshinda maandiko ya Miradi ya utafiti unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)

Waziri Ndalichako amezitaka taasisi zilizopata fedha hizo kuzitumia kwa uadilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa na siyo vinginevyo.

Miradi hiyo nane ni pamoja na ule wa umaliziaji wa kiwanda cha uzalishaji wa dawa na maabara ya utafiti ya mabibo, uimarishaji wa miundombinu ya utafiti na ugunduzi wa dawa katika chuo kikuu cha tiba (MUHAS), Muhimbili, ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa maabara ya uhandisi jeni ya Taasisi ya Mifugo TALIRI kwa ajili ya kuongeza kasi ya uzalishaji wa mifugo, Uboreshaji wa maabara ya Chanjo ya Taasisi ya Taifa Kibaha.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokelewa na baadhi ya watumishi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) mara baada ya kuwasili katika Taasisi hiyo jijini Dar Es Salaam. 

Miradi mingine ni Uboreshaji wa maabara ya udongo, ili kuimarisha Afya ya Udongo kwa ajili ya kilimo endelevu kwa lengo la kuimarisha uchumi wa viwanda, Uboreshaji wa maabara ya kisasa ya utafiti wa mbogamboga na matunda kaskazini mwa Tanzania (HORTI Tengeru), Ukarabati wa mtambo wa utafiti wa kutengeneza mvinyo  katika taasisi ya utafiti wa kilimo, Makutopora na uboreshaji wa usimamizi wa maabara za uchakataji wa mazao ya taasisi ya utafiti wa viwanda TIRDO. 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk. Amosi Nungu akizungumza na washiriki wa Mkutano wa utoaji wa hundi kwa washindi wa maandiko ya miradi

Jumatatu, 21 Mei 2018

EP4R IMEIFANYA SHULE YA SEKONDARI WASICHANA SONGEA KUWA MPYA


Mkuu wa shule ya Sekondari wasichana Songea Tupoke Ndwala amesema shule yake ilipokea zaidi ya milioni Mia mbili kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia kwa ajili ya ukarabati wa mabweni na tayari wamekwisha karabati bweni moja ambalo Lina uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike 115.

Akizungumza na waandishi wa habari Ndwala amesema kabla ya kupokea Fedha hizo kwa ajili ya ukarabati hali ilikuwa mbaya, ikizingatiwa kuwa shule hiyo ni miongoni mwa shule kongwe hapa nchini na hivyo ilikuwa haijafanyiwa ukarabati.

“Kwa kweli naipongeza sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ukarabati huu ambao kwa kweli sasa hivi muonekano wa shule na mabweni umeifanya shule iwe mpya, mandhari ya shule ni nzuri, walimu na wanafunzi ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa miundombinu hii kwa kweli wanafurahia pia wanajifunza na kufundisha kwa Amani”, anasema Ndwala ambaye ni Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari wasichana Songea.
BWENI la MPUTA ni moja ya BWENI lililokarabatiwa katika shule ya sekondari wasichana Songea, (Songea Girls Secondary School) iliyopo manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameelezea kufurahishwa na ukarabati huo na kusema kuwa hivi sasa mabweni yanapendeza hata ukitaka kupiga kumbukumbu ya picha kuonyesha kuwa nilisoma hapa inavutia tofauti na ilivyokuwa awali mabweni yalikuwa  hayavutii. 

Mary Komba anasema awali mabweni kwa maana ya Dari, Sakafu, Vitanda, makabati  na hata rangi iliyokuwa imepigwa ukutani ilikuwa mbaya lakini sasa hivi tumerejea kwenye hali ya nzuri na tunafurahia mno.

“Kwa kweli tunaipongeza sana Serikali ya awamu ya Tano kwa kutuboreshea miundombinu hii ya shule, sasa hivi mabweni yetu ni mazuri na yanapendeza sana hivyo tunaahidi na sisi tutasoma kwa bidii na kufaulu kwa kuwa miundombinu ni mizuri ya kujifunzia”, anasema Mary Komba mmoja wa wanafunzi wa kidato Cha Tano katika shule hiyo.
Muonekano wa sasa wa BWENI la MPUTA baada ya Kufanyiwa ukarabati na fedha zilizotolewa na Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kupitia programu yake ya lipa kulingana na Matokeo, EP4R.

Katika hatua nyingine timu  ya Maafisa kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na na wanahabari walifika katika shule ya Msingi Tembo Mashujaa na kufurahishwa na namna mwalimu wa darasa la pili alivyokuwa akitumia mbinu za kufundishia za kuimbaa , kucheza na wanafunzi wake kwa lengo la kuwafundisha wanafunzi hao.

Mwalimu Assumpta Banda ambaye anafundisha wanafunzi wa darasa la pili  anasema ualimu ni Wito, nidhamu, uadilifu na upendo kwa wale unaowafundisha na kuwa hayo ndiyo yamekuwa maisha yake na anaipenda sana kazi yake.

“ Mwezi ujao ninastaafu, kazi ya Ualimu ni wito. Madarasa haya ya chini ndiyo Msingi wa Elimu hivyo naishukuru sana Serikali kwa kutupatia mafunzo ya KKK ambapo hivi sasa tunatumia zana na mbinu za kufundishia hali ambayo inarahisisha mwanafunzi kuelewa kwa wepesi na pia watoto wanaoenda shule”, anasema Ndwala.
Ukarabati ukiwa unaendelea katika mabweni mengine katika shule ya sekondari wasichana Songea. Shule hiyo ipo kwenye manispaa ya Songea mkoani Ruvuma

Jumamosi, 19 Mei 2018

WANAFUNZI WA CHIDYA WAIPONGEZA SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAJI.


Wanafunzi wa shule ya Sekondari Chidya iliyopo Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wameipongeza serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule hiyo pamoja na kuchimba kisima ambacho kimewapungizia adha ya upatikanaji wa Maji kwa urahisi.

Wanafunzi hao wametoa kauli hiyo wakati walipofanya mahojiano na waandishi wa habari kufuatia ziara ya ufuatiliaji wa uboreshaji wa miundombinu ya shule na ujifunzaji na ufundishaji wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu - KKK.

 Wanafunzi hao wamesema mwanzoni miundombinu ilikuwa imechakaa pia walikuwa wanafuata Maji umbali takribani kilometa moja na pia iliwalazimu kila siku kuamka alfajiri ili kufuatilia Maji hivyo iliwafanya wachoke na hata kupunguza morali ya kusoma.

 Jengo la Utawala lililokarabatiwa katika Shule ya Sekondari Chidya Wilayani Masasi Mkoani Mtwara.

“Kwa kweli hili la Maji wanafunzi lilikuwa linakera sana maana inatulazimu kuamka kila siku alfajiri kufuatilia maji na kisha kujindaa kuelekea shuleni kwa ajili ya masomo, kwa kweli hii ilikuwa inatuchosha na pia ilikuwa ni hatari kwa sababu tulikuwa tunakutana na wadudu wabaya kama vile nyoka,” anasema mmoja wa wanafunzi hao Saidi Mnguvu.

 “Nakumbuka tulikuwa tunatolewa darasani kwa ajili ya kuafuatilia maji, hata vipindi wakati mwingine vilikuwa vinakatishwa ili tuweze kwenda kufuata Maji sasa adha hii ya Maji kwa kweli imeisha na sasa tunaishi kwa raha na tunapata Maji muda wote,” anasema Mnguvu.
Muonekano wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika Shule ya Sekondari Chidya iliyopo Wilayani Masasi Mkoani Mtwara. 


 Mkuu wa shule hiyo ya Sekondari ya Chidya Zawadi Mdimbe ali
sema shule hiyo ilipokea zaidi ya milioni Mia mbili kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa kulingana na matokeo yaani (EP4R) ambazo zimetumika kukarabati Miundombinu ya vyumba vya madarasa, ujenzi wa Nyumba za walimu, kuboresha miundombinu ya Maji, bwalo, Jiko pamoja na kukarabati ofisi za walimu za shule hiyo.
Muonekano wa majengo mawili yenye vyumba vya madarasa vilivyokarabatiwa katika Shule ya Sekondari Chidya Wilayani Masasi Mkoani Mtwara.

Alhamisi, 17 Mei 2018

KKK IMEONDOA WASIOJUA KUSOMA NA KUANDIKA


·   EP4R IMEONDOA ADHA YA VYOO ILIYOKUWA INAIKABILI SHULE YAMBAWALA 

Mkuu wa shule ya Ufundi Mtwara Paul Kaji amepongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuboresha miundombinu ya shule hiyo na hivyo kuondoa kabisa changamoto mbalimbali zilizoKuwa kikwazo kwa wanafunzi na walimu shuleni hapo.

Kaji ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na timu ya wanahabari waliofika shuleni hapo kwa lengo la kuangalia ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo ambapo zaidi ya bilioni moja imetumika kukarabati vyumba vya madarsa, ofisi za walimu, mabweni, Bwalo la chakula, sehemu za kuandalia chakula (majiko), kukarabati njia Maalumu za wanafunzi wenye ulemavu, kurejesha miundombinu ya umeme na Maji katika hali ya kawaida.

Pia baadhi ya wanafunzi waliohojiwa wameelezea kufurahishwa na ukarabati huo na hivyo kuwafanya kuwa katika mazingira mazuri ya kusomea.
“Tunaishukuru Serikali kwa kutuboreshea miundombinu ya shule siyo tu shule yetu imependeza bali hata sisi tuna uwezo wa kusoma muda wowote kwa kuwa umeme upo, tunawasilisha shukrani na hivyo tunaahidi tutasoma kwa bidii ili tufaulu vizuri” anasema David Andrew mmoja wa wanafunzi wa kidato cha pili katika shule hiyo ambaye anasomea fani ya ujenzi.

Muonekano wa darasa linaloongea KKK katika Shule ya Msingi Msijute iliyopo Mkoani Mtwara


Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Mbawala Ali Haroun amesema licha ya kujenga madarasa mapya lakini jambo ambalo limeleta heshima kwao ni ujenzi wa matundu ya vyoo.

Alisema katika fedha hizo wamejenga matundu ya vyoo 10 na kufanya jumla ya matundu ya vyoo kuwa 16 na madarasa 8 jambo ambalo limesaidia kuongeza wanafunzi na kila darasa kukaa wanafunzi kulingana na ukubwa wa darasa.
Hata hivyo aliongeza kuwa matundu ya vyoo yamewasaidia katika kuhakikisha walimu wanakaa shuleni muda wote kuliko hapo zamani ambapo ilikuwa ni lazima kwenda kujisaidia majumbani kwao.

‘’Hapo awali kulikuwa na shida kabisa kwani walimu walikuwa wanafika shuleni wakijisikia kubanwa na haja wanakimbilia nyumbani na kuwafanya kuchukua muda mwingi hadi wa vipindi ndipo wanarejea shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo,’’

‘’ Programu hii ni mkombozi kwetu kwani hata wanafunzi waliokuwa wakikaa katika madarasa kwa kubebana sasa wanakaa kwa nafasi na mpaka chumba kimoja kimebaki kwa kukosa wanafunzi,’’aliongeza mwalimu Ally.
Mwalimu wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Msijute Mariamu Milanzi akifundisha kwa kutumia zana zilizowekwa katika darasa darasa la awali. Matumizi ya Zana za kufundishia unasaidia watoto kuelewa kwa urahisi kupenda shule na kupunguza utoro.

Naye mwalimu, Isabela Mwambona alisema mradi huo umewarahisishia kazi kutokana na kufundisha kwa nafasi na hata kuwafikia wanafunzi  mmoja baada ya mwingine kwa ufundishaji.

Katika hatua nyingine programu ya Kusoma, Kuandika na  Kuhesabu (KKK) imezaa matunda katika shule mbalimbali za Mkoa wa Lindi na Mtwara.
Isabela alisema tangu wapeate mafunzo ya ufundishaji wa KKK kwa kutumia vitendo na michoro kwa sasa wamefanikiwa kupunguza idadi ya wasiojua Kusoma na Kuandika shuleni hapo.
Wanafunzi wa Darasa la Awali katika shule ya Msingi Msijute wakiwa darasani tayari kwa kuanza masomo. 

Jumatano, 16 Mei 2018

EP4R ILIVYOSAIDIA KUONDOA CHANGAMOTO YA MIMBA KWA WANAFUNZI WA KIKE MKOANI LINDI.


Wakuu wa shule za Sekondari mkoani Lindi wamesema kuwa ujenzi wa mabweni unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Lipa Kulingana na matokeo, yaani EP4R katika mkoa huo utasaidia sana kuondoa changamoto ya wananfunzi wa kike kupata mimba wakiwa katika umri mdogo.

Wakizungumza na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali Mkuu wa shule ya sekondari ya Ruangwa Mwalimu Herber Ngonyani amesema kupitia mradi wa EP4R shule hiyo imeweza kujenga mabweni Mawili ambayo yanauwezo wa kuchukua wanafunzi Laki moja na sitini kwa wakati mmoja, huku Mkuu wa shule ya Sekondari Nkowe Ahmed Maliki akikiri kuwa shule yake  imejenga mabweni mawili yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi mia moja na ishirini na nane kwa mara moja.
Muonekano wa bweni katika Shule ya Sekondari Ruangwa Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi. Bweni hilo limejengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).


Wakuu hao wa shule wameeleza kwa muda mrefu watoto wa kike katika wilaya hiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu na hivyo kukumbana na vishawishi ambavyo hupoteza ndoto za wanafunzi hao.

“ Nikiri kuwa mwamako wa Elimu katika Wilaya yetu bado uko chini hivyo hata hamasa ya wazazi na watoto nayo iko chini katika suala zima la Elimu, sasa hiki ambacho Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia inachokitekeleza kupitia mradi wa Lipa kulingana na matokeo kwa kweli ni mkombozi kwa watoto wa kike kwa kuwa sasa watasoma kwa utulivu tena wakiwa katika mazingira ya shule kutokana na ujenzi huu wa mabweni,”anasema Mwalimu Herbert Ngonyani.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya Nkowe Ahmed Maliki amessitiza kuwa uwepo wa mabweni utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya utoro miongoni mwa wanafunzi pamoja na kuwasidia wanafunzi wa kike kupuka mazingira hatarishi ya kutembea umbali mrefu takribani kilometa 4 hadi tano kwa siku kwa ajili ya kufika shuleni. 
Muonekano wa bweni katika Shule ya Sekondari Nkowe Wilayani Ruangwa Mkoani Lindi. Bweni hilo limejengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). Bweni hilo litasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi wa kike kupata mimba katika umri mdogo.

Mwalimu Malik amesema kuwa mabweni hayo yatasaidia siyo tu kuhuduia wanafunzi wa wanaotoka kwenye mkoa wa Lindi pekee bali wananfunzi kutoka mikoa mbalimbali watanufaika na mabweni hayo.


Katika kutekeleza uboreshaji wa Miundombinu ya shule za msingi, moja ya shule ambazo zilipatiwa fedha za kujenga miundombinu hiyo ni pamoja na shule ya msingi Nangumbu ambayo ilipatiwa kiais cha shilingi Milioni sitini na sita kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa vitatu na matundu ya vyoo sita lakini shule hiyo imeweza kujenga vyumba vya madarasa vinne, ofisi moja na matundu kumi ya vyoo.

Timu ya wananhabari ambayo imeambatana na maafisa wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kesho itaendelea na ziara yake Mkoani Mtwara ikiwa na lengo la kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari inayotekelezwa kupitia program ya lipa kulingana na matokeo.
Muonekano wa moja ya darasa liliojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika Shule ya Sekondari Nkowe iliyopo katika Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.





Jumatatu, 14 Mei 2018

ZAMBI: AELEZEA EP4R ILIVYOBORESHA MIUNDOMBINU YA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI


  •          AKIRI KUWA SASA SHULE ZIMEKUWA MPYA

Zaidi ya shilingi bilioni 2 zimetumika kujenga na kukarabati miundombinu ya shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa wa Lindi na hivyo kuchochea kuongeza kwa kiwango cha ufaulu miongoni mwa wanafunzi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi wakati akizungumza na timu ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari ameeleza kuwa Mpango huo Maalumu wa  Lipa Kulingana na Matokeo yaani EP4R umebadilisha muonekano wa mazingira na kuzifanya shule nyingi za Mkoa huo kuwa mpya.

Muonekano wa moja ya Jengo la darasa la Shule ya Msingi Kitomanga lililopo katika Halmashauri ya Lindi Vijijini Mkoani Lindi liliojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). 

Zambi amesema kupitia EP4R Mkoa huo umejenga vyumba vya madarasa 30 kwa shule za Msingi, vyumba 22 kwa shule za sekondari, maabara 6 zimekarabatiwa, na ujenzi wa matundu ya vyoo 84 na kuwa ujenzi na michiro ya miundombinu hiyo imekuwa ikizigatia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.


Hata hivyo ameeleza kuwa bado ujenzi wa miundombinu mingine unaendelea katika shule za Msingi na Sekondari ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule mbalimbali.

“Kabla ya ukarabati nikiri kuwa hali ilikuwa siyo nzuri katika miundombinu ya shule lakini kupitia EP4R Mkoa wa Lindi miundombinu yake imebadilika sana ambapo pia imeongeza hamasa ya wanafunzi kusoma na hivyo kuongeza ufaulu, pia utoro umepungua sana maana kuboreka kwa miundombinu kumehamasisha wanafunzi kupenda shule,” anasema Zambi.
1.       Muonekano wa moja ya Jengo la darasa la Shule ya Sekondari Kilwa lililopo katika Halmashauri ya Lindi Mkoani Lindi liliojengwa na Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). 

Mkuu huyo wa mMkoa amesema kuwa ukarabati wa maabara kwa Mkoa huo pia umesaidia sana mwitikio wa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kwa kuwa hivi sasa wanafanya mazoezi kwa vitendo na hivyo kuwafanya waelewe kwa urahisi.

Mkuu huyo wa mkoa amekiri kuwa bado mwitikio wa Elimu katika Mkoa  huo uko chini na hivyo kuwafanya watoto walio wengi kutothamini Elimu.

“Mwitikio wa wananchi kuhusu Elimu bado uko chini, na wazazi ndiyo wanaochangia kwa kuwa ndiyo wanaowapeleka watoto wao kwenda kufanya shughuli za shambani ikiwemo kutuma korosho pamoja na kushiriki katika masuala ya mila na tamaduni za kuwapeleka watoto kwenye unyago,” anasema Zambi.
 Muonekano wa moja ya Jengo la darasa la Shule ya Msingi Masoko lililopo katika  Halmashauri ya Kilwa Mkoani Lindi liliojengwa na Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). 


Mkuu huyo amesisitiza kuwa ni vyema wazazi wakatambua umuhimu wa Elimu ili kuwasaidia watoto kupenda shule kwa lengo la kuliletea taifa Maendeleo.

Timu ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali pamoja na Maafisa kutoka Kitengo Cha Mawasiliano Cha Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wako Mkoani Lindi kwa ajili ya kufuatilia uboreshaji wa miundombinu inayojengwa na kukarabatiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo, EP4R.

Mikoa mingine ambayo timu hiyo itafanya ufuatiliaji ni pamoja na Mkoa wa Mtwara na Songea.
1.       Muonekano wa jingo la Choo kilichojengwa katika Shule ya Msingi Kitomanga iliyopo Wilayani Lindi Vijijini Mkoani Lindi, Ujenzi choo hicho umetekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).

PROF. NDALICHAKO: TUMIENI FURSA YA FEDHA ZA UMOJA WA ULAYA KATIKA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa wito kwa Taasisi za Kitafiti, Vyuo Vikuu na watu mbalimbali ambao wanahusika na  kufanya tafiti katika masuala ya uchumi pamoja na usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma kuhakikisha wanatumia vizuri fedha zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kufanya tatiti zenye tija.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na  wageni waliofika kushuhudia uzinduzi rasmi wa wito kwa ajili ya maandiko ya kuomba fedha kiasi cha uro milioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania bilioni nne zilizotolewa na Umoja wa Ulaya.

Waziri Ndalichako ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa wito kwa ajili ya maandiko ya kuomba fedha kiasi cha uro milioni 1.5 ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania bilioni nne zilizotolewa na Umoja wa Ulaya kwa lengo la kuwezesha tafiti hizo ili kuiwezesha serikali kusimamia raslimali za nchi katika kuleta tija na kuisaidia serikali ya awamu ya tano  kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya Nchini na Afrika Mashariki Roeland Van de Geer amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kusaidia watafiti, Vyuo Vikuu na Mashirika ya Kitafiti yasiyokuwa ya kiserikali kwa kuwa ni wachangiaji wa mijadala ya kisera kupitia matokeo ya tafiti wanazofanya  katika kuleta mabadiliko ya uchumi wa viwanda na kuondoa umasikini.