Jumanne, 17 Julai 2018

SERIKALI YAZINDUA MFUKO WA KUENDELEZA UJUZI


Serikali imezindua Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) utakaowezesha watoa huduma za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali kutoa mafunzo yenye tija yatakayoweza kukuza stadi za kazi.

Akizindua Mfuko huo Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema mfuko huo unalenga kuboresha stadi za kazi, uwezo wa kujiajiri na kuchangia ongezeko la wataalam  wenye stadi mbalimbali katika taaluma za Kilimo, Utalii, Nishati, Ujenzi, Uchukuzi na TEHAMA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa Elimu (hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) Jijini Dar es Salaam utakaowezesha watoa huduma za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali kutoa mafunzo yenye tija yatakayoweza kukuza stadi za kazi uliofanyika.

Prof. Ndalichako amesema katika kuleta ufanisi wa kukuza ujuzi Wizara yake itaanzisha kwa mara ya kwanza Baraza la Taifa la Ujuzi (National Skills Council – NSC) ambalo litasimamia mabaraza ya kisekta ya kukuza ujuzi (Sectoral Skills Council).

“Tayari Wizara ina makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) itakayosaidia uanzishwaji wa mabaraza hayo na  Baraza la Taifa la Ujuzi (NSC) litakuwa waangalizi wa mfuko huu wa SDF tunaouzindua leo, hivyo sekta binafsi itakuwa na fursa ya kutoa mchango wake katika ukuzaji ujuzi hapa nchini. “alisisitiza Prof. Ndalichako



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na washiriki wa uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wote watakaopata fedha za Mfuko huo kuzitumia kwa malengo yaliyowekwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dk. Erasmus Kipesha amesema Taasisi yake ina jukumu la kuusimamia Mfuko huo na imedhamiria kuhakikisha kuwa rasilimali zilizoelekezwa katika Mfuko huo zinatumika kwa weledi, taratibu, haki, ubora, na ufanisi wa hali ya juu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Dk. Erasmus Kipesha mfano wa hundi kwa ajili ya Taasisi za Elimu ya Ufundi zitakazoshiriki katika kukuza na kuendeleza ujuzi. Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Jumatano, 11 Julai 2018

WAZIRI NDALICHAKO AMTAKA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU KUWACHUKULIA HATUA WALIOHUSIKA NA SAKATA LA VIFAA VYA MAABARA CHUO CHA UALIMU KASULU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na uagizaji na upokeaji wa vifaa vya maabara katika Chuo cha Ualimu Wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo Wilayani Kasulu alipofanya ziara katika Chuo hicho na kukuta idadi kubwa ya kemikali za maabara zisizohitajika lakini pia vifaa vya maabara kutokuwa na ubora huku chuo kikiomba kununuliwa tena vifaa vya maabara na kemikali.

“Haiwezekani kwa sasa manasema mna upungufu wa vifaa pamoja na kemikali wakati mmevijaza hapa chuoni tena kwa utaratibu usiofaa, huku mkisema vitaharibika kwa kuwa havihitajiki, ni nani aliviagiza na ni kwanini mliviagiza bila ya kuwa na uhitaji, kwa hili sio la kufumbia macho ni lazima hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika katika suala hili”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Watumishi wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Mkoani Kigoma wakati alipowasili chuoni hapo. 
Waziri Ndalichako pia ameitaka Idara ya Elimu ya Ualimu katika Wizara hiyo pamoja na Chuo cha Ualimu Kasulu kutoa taarifa ya kina ya uagizaji na upokeaji wa vifaa hivyo kwa kuwa kumekuwepo na kutokuelewana baina yao ni nani alitoa mahitaji halisi ya vifaa hivyo hali iliyoisababishia Serikali hasara ya kununua vifaa visivyohitajika wakati zipo shule za Sekondari zingeweza kupata vifaa hivyo.

“Bahati mbaya bodi yenu haina taarifa ya manunuzi haya, wakuu wa vyuo muache tabia ya kuficha mambo yanayoendelea chuoni hapa nachukua hatua na bodi iangalie hatua za kuchukua hatuwezi kuruhusu mtu anayefanya uhalifu huu akabaki salama,” alisema Profesa Ndalichako.
Wzairi wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua kemikali za Maabara katika Chuo cha Ualimu Kasulu

Awali Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu Josephat Mwangamila katika hotuba yake alisema Chuo hicho kina deni la takribani shilingi milioni 64 kwa ajili ya ununuzi wa Kemikali na Vifaa kwa ajili ya matumizi ya ofisi (stationary) kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya mitihani.

Mkuu wa Chuo alisema walifikia uamuzi wa kununua kemikali hizo kwa kuwa hawakuwa nazo chuoni hapo lakini pia zilizokuwepo hazihitajiki kwa matumizi chuoni hapo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya majengo ya Chuo Cha Ualimu Kabanga Mkoani Kigoma. Akiwa Chuoni hapo Profesa Ndalichako amezungumza na wakufunzi pamoja na watumishi wa chuo na kuahidi kujenga upya Chuo hicho kwa kuwa miundombinu yake imechakaa. 

Serikali imenunua vifaa vya maabara  vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Moja ambavyo vimesambazwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini ikiwa ni juhudi za kuhakikisha walimu wanapata mafunzo kwa vitendo ili wakaweze kufundisha kwa umahiri pindi wanapomaliza masomo yao.

Waziri wa Elimu pia ametembelea Chuo cha Ualimu Kabanga ambapo ameahidi kujenga upya chuo hicho katika mwaka wa fedha ulioanza 2018/19 kwa kuwa majengo yake ni chakavu na kuvitaka vyuo ambavyo vimekarabatiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kutunza miundombinu ya vyuo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya ngazi za mabweni ambayo imechakaa katika Chuo Cha Ualimu Kasulu, Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma

Ijumaa, 6 Julai 2018

DK. SEMAKAFU ASEMA HAKUNA ATAKAESALIMIKA MATUMIZI YA FORCE AKAUNTI


Serikali imesema haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yeyote atakayekiuka utaratibu wa kutumia Force Akaunti katika kutekeleza shughuli za ujenzi na ukarabati kwenye Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDC’S).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Dk. Avemaria Semakafu  mjini Morogoro wakati wa akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wakuu wa vyuo, maboharia na wahasibu kuhusu utaratibu wa kutumia Force Akaunti katika shughuli za ujenzi na ukarabati katika vyuo vya FDCs.
kuwa upo kisheria na kwa yeyote atakaepindisha utaratibu huo atawajibika kwa hilo. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akizungumza na wajumbe (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo ya matumizi ya utaratibu wa Force Account Mjini Morogoro. Amewataka wajumbe kuhakikisha wanafuata utaratibu huo.
Alisema utaratibu huo uko kisheria na kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha kupata taaluma ya kutumia utaratibu huo  ambapo amewataka washiriki hao kwenda kutumia taaluma hiyo kama nyenzo kuleta mabadiliko wakati wa kutekeleza miradi katika maeneo yao.


 “Ni muhimu kwa Wakuu wa Vyuo na wote mtakaohusika katika shughuli za ujenzi na ukarabati kuhakikisha mnafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa kuwa hakuna atakaesalimika kwa kuvunja sheria hizi,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo  Dk Semakafu.


Wajumbe wa Kikao wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu wakati wa kufunga mafunzo ya matumizi ya Force Account kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maboharia na Wahasibu yaliyofanyika mjini Morogoro.
Amesema Vyuo vya maendeleo ya Wananchi vilianzishwa kwa malengo mahususi ikiwa ni pamoja na kutoa stadi na mafunzo kwa wananchi hivyo miradi hiyo ikikamilika kwa wakati vyuo vitaweza kutimiza malengo yake lakini pia thamani halisi ya matumizi ya fedha (Value for Money) za ujenzi na ukarabati zitaonekana.

Mafunzo hayo ya utaratibu wa kutumia Force Akaunti yameshirikisha wajumbe kutoka Vyuo vya maenedeleo ya wananchi 11 na yameendeshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya  mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Ajira (ESPJ).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya namna ya kutumia force Akaunti yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jumatano, 4 Julai 2018

WAZIRI NDALICHAKO AIELEKEZA COSTECH KUPELEKEA MIONGOZO YA KUSAIDIA WABUNIFU KWENYE HALMASHAURI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce NDALICHAKO ameitaka Tume ya Taifa ya Sayansi naTeknolojia, COSTECH -kuhakikisha miongozo yote ya namna yakuwasaidia wabunifu inapelekwa  katika ngazi ya Halmashauri ili kuwezesha kupatikana kwa bunifu zitakazosaidia nchi kufikia uchumi wa viwanda.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo katika kongamano la  sita la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na ubunifu linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wanasayansi na wavunifu katika kongamano la sita la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Ndalichako amesema miongozo ikipelekwa kwenye halmashauri itasaidia  kupatikana kwa wabunifu watakaoendeleza  Teknolojia  na kufanya kazi katika viwanda.

Waziri huyo mwenye dhamana ya kusimamia Elimu, Sayansi na Teknlojia amesema uchumi wa viwanda unategemea Sayansi  na wataalamu wenye ujuzi wakutengeneza na kubuni bidhaa mbalimbali zitakazotumika   viwandani lakini pia kuiletea jamii Maendeleo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Shule ya St Jude Erick Laizer kuhusu ubunifu wa mtambo wa ulinzi dhidi ya moto na wizi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH  Dkt. Amos Nungu, amesema Kongamano hilo la siku tatu Lina lengo la  kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi, ikiwa ni pamoja  na kuanzisha na kuendeleza viwanda.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Abubakari Amani mtaalam aliyetengeza mashine ya kupurura ama kupura maharage katika   kongamano la sita la  Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linaloendelea jijini Dar es Salaam.

SERIKALI YAANZA KUKARABATI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI.


·         PROFESA MDOE ASISITIZA MATUMIZI YA FORCE AKAUNTI

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wakuu wa Vyuo vya maendeleo ya Jamii nchini na Maboharia kutumia kikamilifu utaalamu watakaoupata katika mafunzo ya namna ya kutumia Force Account na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu shughuli za ujenzi na ukarabati katika vyuo hivyo.

Profesa Mdoe ametoa kauli hiyo Mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa washiriki hao na kusisitiza kuwa   Serikali kwa sasa inakarabati vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, hivyo mafunzo watakayoyapata yakawe chachu ya kusimamia kazi hiyo kwa umakini na uadilifu ili thamani ya matumizi ya fedha iweze kuonekana.

“Ni vizuri mkashiriki mafunzo haya kikamilifu kwa kuwa matokeo ya mafunzo haya yataonekana katika utekelezaji wa miradi na kila mtu atawajibika kwa nafasi yake, thamani ya Fedha lazima iende ikaonekana katika utekelezaji wa uboreshaji wa vyuo hivi vya FDCs,” alisisitiza Profesa Mdoe.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe akizungumza na wajumbe (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya matumizi ya Force Account Mjini Morogoro. Amewataka wajumbe kutumia utaalamu watakaoupata katika kusimamia ujenzi na ukarabati katika vyuo vyao.

Profesa Mdoe amesema matumizi ya utaratibu wa Force Akaunti ni mzuri kwa kuwa gharama zinazotumika katika ujenzi na ukarabati ni ndogo na hii inatokana na kutumia wataalam na vifaa vya vinavyonunuliwa na kusimamiwa Taasisi husika.

Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Ajira umeanzishwa kwa lengo la kutekeleza vipaumbele vya Serikali vilivyoainishwa katika mkakati wa Serikali wa kufikia Tanzania ya Viwanda ifikapo 2025, lakini pia kuwezesha vijana kupata ujuzi kwa vitendo kuliko nadharia pamoja na kujengea uwezo vyuo vya kati.
Wajumbe wa Kikao wakifuatilia hotuba ya Kaimu Katibu Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia Profesa James Mdoe wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya Force Account kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maboharia na Wahasibu yaliyofanyika mjini Morogoro.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanahusisha Wakuu wa vyuo vya FDCs 11, Wahasibu na maboharia na yanatarajiwa kukamilika kesho kutwa.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia Profesa James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya namna ya kutumia force Account yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jumanne, 3 Julai 2018

SERIKALI IMEKABIDHI PIKIPIKI ZAIDI YA 2500 KUBORESHA ELIMU NCHINI


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leo imekabidhi Pikipiki zaidi ya 2500 kwa  Waratibu Elimu Kata ili ziwasidie katika kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuimarisha Elimu hapa nchini.

Pikipiki hizo zinakabidhiwa Leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Joyce Ndalichako ambapo amesema Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES)  umenunua Pikipiki hizo 2894 kwa zaidi ya shilingi bilioni  Nane.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo wakikata utepe kuashiria makabidhiano ya Pikipiki zilizotolewa na Wizara ya Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) wanaoshuhudia tukio hilo ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pfor. James Mdoe na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda 

Waziri Ndalichako amesema pikipiki hizo zitasambazwa nchi nzima kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI.
"Rais alipoingia madarakani alihaidi kuimarisha ubora wa Elimu, sasa moja ya mikakati ya kutekelez hilo ndiyo maana hii Leo tunashuhudia vitendea Kazi hivi ambavyo vitasambazwa nchi nzima, lengo hapa ni kuhakikisha Elimu  inayotolewa inakuwa bora na kuhakikisha  nchi inakuwa na matokeo chanya kiuchumi” amesema Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amewataka waratibu elimu Kata hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatumika kwa ajili yakusimamia elimu katika maeneo yao na kupandisha ufaulu na si vinginevyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo wakizijaribu Pikipiki zilizotolewa kwa Waratibu Elimu Kata nchini Kata ili ziwasidie katika kutekeleza majukumu yao wengine katika picha ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pfor. James Mdoe na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda

Kwa upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amewataka waratibu elimu kata kuhakikisha wanasimamia taaluma katika maeneo yao.

Aidha, Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Mikoa, Halmashauri, Manispaa na Majiji kuweka utaratibu wa kuzihudumia pikipiki hizo katika maeneo yao.


Mmoja wa Waratibu Elimu Kata akijaribu kuendesha Pikipiki iliyokabidhiwa kwake kwa ajili ya kumsaidia kusimamia elimu katika kata yake huku akishuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha