Jumatano, 8 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA BODI YA HUDUMA ZA MAKTABA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Bodi mpya ya Huduma za Maktaba Tanzania kuhakikisha inaanzisha Maktaba za Wilaya ili kuwawezesha watanzania wengi kunufaika na Elimu na Maarifa yatokanayo na usomaji wa vitabu.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi hiyo na kusisitiza kuwa kuwepo kwa maktaba hizo kutaondoa changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata maktaba za mikoa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania Prof. Rwekaza Mkandala Sheria za Bodi hiyo. 

“Wananchi wanapenda kusoma vitabu sasa natoa rai kwenu Bodi mpya mshirikiane na Halmashauri za Wilaya, Miji na Manispaa kuanzisha Maktaba katika Wilaya zote, sisi kama Serikali tutaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha tunaimarisha utoaji wa huduma za maktaba nchini.” Alisisitiza Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mwenyekiti wa Baraza laUsimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Naomi Katunzi Sheria za Bodi hiyo. Ameiagiza Baraza hilo kuweka vigezo vitakavyotumika kutoa Elimu nje ya mfumo rasmi.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ametemblea Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na kuzindua Baraza la Usimamizi la Taasisi hiyo ambapo amelitaka  baraza hilo kuboresha vigezo vinavyotumika kusajili vituo vinavyotoa Elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi pamoja na kusimamia ubora wa elimu inayotolewa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiongea na Watumishi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (Hawapo Pichani) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Taasisi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Jumatatu, 6 Agosti 2018

AWAMU YA PILI MAFUNZO UTHIBITI UBORA YAANZA KATIKA KANDA TANO


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza awamu ya pili ya kutoa mafunzo kwa Wathibiti Ubora  wa shule kwa Kanda za Dar es Salaam, Arusha, Moshi, Morogoro  na Mtwara juu ya  kutekeleza mfumo mpya wa Uthibiti ubora wa shule.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya wathibiti ubora mkoani Arusha Naibu Waziri William Ole Nasha amewataka watumishi hao kusimamia mfumo na mxhakato wa utoaji wa Elimu kwa kuhakikisha Sera, kanuni , sheria na mongozo inazingatiwa na wadau wote katika sekta ya Elimu.

Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua mafunzo ya wathibiti ubora awamu ya pili yanayoendelea nchini.

 Naibu waziri ole Nasha amewataka wathibiti ubora kuhakikisha dhamira ya serikali inatimizwa kwa wathibiti ubora wa shule kuhama kutoka katika dhana ya ukaguzi kama wajuaji zaidi, au polisi kwa kukagua zaidi na badala yake wawe wathibiti ubora wa shule  kwa kuhakikisha kuwa wanawasaidia walimu, kwa lengo la kuhakikisha serikali inafikia malengo ya kuwa na uchumi wa viwanda.


Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa wizara hiyo, Euphrasia Buchuma amefungua mafunzo hayo jijini Dar es Salaam ambapo amewataka Wathibiti Ubora kuzingati mafunzo yanayotolewa ili kuwawezesha kufanyia kazi  yale yote yanayoelekezwa.
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo Elekezi ya Mfumo Mpya wa Uthibiti Ubora wa Shule wakimsikiliza Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchumu (Hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa shule ya sekobdari Zanaki Jijini Dar es Salaam

Buchuma amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wathibiti ubora wa shule kuweza kufanya  ukaguzi wa shule kwa kutumia mfumo mpya ambao ni shirikishi unaoangalia zaidi tendo la kujifunza, kufundisha na kufanya upimaji katika ngazi ya darasa.

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo  mthibiti ubora wa shule  kutoka Manispaa ya Ilala Diana Justine amesema mafunzo hayo yatawawezesha kutatua changamoto wanazokuta nazo  shuleni kwa kushirikiana na walimu, wanafunzi na jamii tofauti na awali walipokuwa wanakwenda kuangalia matatizo bila kutoa suluhisho la matatizo hayo.

Jumapili, 5 Agosti 2018

NDALICHAKO ATAKA SHULE YA SEKONDARI MANGA DELTA KUPANDISHA TAALUMA


Waziri wa Elimu, Sayamsi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amewataka walimu wa shule ya sekondari Manga Delta iliyoko wilayani Kibiti mkoani Pwani kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi kimasomo ili taaluma katika shule hiyo iweze  kupanda.

Waziri Ndalichako ametoa agiza hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule hiyo ambapo amesema hajaridhishwa na mwenendo wa taaluma katika shule hiyo.

Amesema pamoja na serikali kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo bado imekuwa ikishuka kitaaluma mwaka hadi mwaka.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalich ako akizungumza na wanafunzi, walimu na wazaza wa shule ya Sekondari Manga Delta iliyoko wilayani Kibiti mkoani Pwani. Waziri Ndalichako amewataka walimu wa shule hiyo kuhakikisha wanawasaidia wanafunzi kimasomo ili taaluma katika shule hiyo iweze  kupanda.

 “Serikali imeshatoa zaidi ya shilingi milioni 256 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya vyumba vya madarasa na bweni juhudi hizi ziende sambamba na ufundishaji ili taaluma ipande”  Alisisitiza Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi ufunguo wa pikipiki kwa mmoja wa Waratibu Elimu Kata ambapo amekabidhi Pikipiki kumi na sita katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Kibiti Mkoani Pani. Waziri Ndalichako amewataka Waratibu Elimu Kata hao kutumia Pikipiki hizo katika shughuli zitakazosaidia kuboresha Elimu.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kila mwezi imekuwa ikitoa kiasi cha silingi bilioni 20. 8 kugharamia Elimu bila malipo pamoja na kutoa shilingi laki mbili na nusu za posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata hivyo amewataka kuwajibika ili kupandisha taaluma ya shule hiyo.

Waziri wa Elimu amehitimisha ziara yake ya siku mbili ya kikazi wilayani Kibiti mkoni Pwani kwa kukabidhi gari ya Idara ya Udhibiti Ubora kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo pamoja na pikipiki kumi na sita kwa Waratibu Elimu Kata.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifungua gari kabla ya kumkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kibiti Alvera Ndabagoye kwa ajili ya Idara ya Udhibiti Ubora ya wilaya hiyo. Waziri Ndalichako amewataka Wadhibiti ubora nchini kufanya kazi zao kwa weledi

SHULE YA MSINGI KIOMBONI KUJENGEWA MIUNDOMBINU MIPYA


Waziri wa Elimu, Sayamsi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amehaidi kujenga na kuboresha miundombinu ya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi ya Kiomboni ambayo miundombinu yake kwa sasa ni chakavu.  

Waziri Ndalichako ametoa ahadi hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule hiyo iliyopo katika Kijiji cha Kiomboni Kata Salawe Wilayani Kibiti Mkoani Pwani.

Amesema kuwa shule hiyo pamoja na kuwa chakavu ina upungufu wa vyumba vya madarasa hvyo kupelekea hali ya ufundishaji na ujifunzaji kuwa ngumu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikaribishwa na baadhi ya viongozi na wananchi wa Kijiji wa Kiomboni Wilayani Kibiti mkoani Pwani alipowasili katika kijiji hicho ili kujionea changamoto zinazoikabili shule ya msingi ya Kiomboni. Waziri Ndalichako aliwahaidi wanakijiji hao kuwa serikali kupitia wizara yake watajenga miundombinu mipya katika shule hiyo

"Nimezinguka katika shule hii nimejionea kwa macho yangu jinsi miundombinu yake ilivyo kwenye hali mbaya na ninaahidi kuwa wizara yangu itafanya uboreshaji wa miundombinu hii ili mazingira ya kujifunzia yaweze kuwavutia watoto kupenda shule  " Aesema Ndalichako.

Waziri huyo amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamilia kuboresha miundombinu ya Shule kwa kukarabati na kujenga mipya ili kuwezesha watoto kjifunza katika mazingira rafiki.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na viongozi wa wilaya ya Kibiti wakikagua miundombinu ya madarasa na matundu ya vyoo  ya shule ya msingi kiomboni ambayo yamechakaa. Waziri huyo yupo wilayani Kibiti katika ziala ya kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa na wizara ya elimu kupitia programu ya EP4R

Ndalichako amewahakikishia walimu wa shule hiyo pamoja na wanakijiji kuwa ujenzi na Ukarabati huo utafanyika mapema kabla ya mvua za masika hazijaanza.

Awali katika taarifa yake Mkuu wa shule Musa Mapange  alimweleza Waziri kuwa Shule hiyo haina vyoo imara kwani vilivyokuwepo vimeharibika na kufungwa na sasa watoto wanajisaidia katika vyoo vilivyotengenezwa kwa dharula.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Mbunge wa Kibiti Ali Ungando na Mkuu wa Wilaya hiyo Philiberto Sanga wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi wa shule  msingi kiomboni. Ndalichako  amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

Waziri Ndalichako upo katika ziara ya siku mbili ya kikazi Wilayani Kibiti mkoani Pwaniku kagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na wizara Kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)


Ijumaa, 3 Agosti 2018

SERIKALI KUONGEZA RASLIMALI WATU WENYE UJUZI STAHIKI KATIKA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema nchi inahitaji rasilimali watu yenye ufahamu na ujuzi stahiki katika kujenga uchumi wa viwanda.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano na maonesho ya Wahandisi wanawake wa Taasisi ya Wahandisi Jijini Dar es Salaam Ndalichako amesema Wizara yake imeweka mikakati mbalimbali ili kuhakikisha nchi inakuwa na rasilimali watu ya kutosha, wenye ujuzi utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya Taifa.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wa washiriki wa Kongamano na Maonesho ya Wahandisi Wanawake wa Taasisi ya Wahandisi iliyofanyika Jijini Dar es Salaam. Amesisitiza Wahandisi hao kuweka katika vitendo tafiti zao ili kuwasaidia wananchi katika kutatua changamoto.


“Tunao mradi wa Mkakati wa Kukuza Staadi za Kazi (ESPJ unaotekeleza Mkakati wa Kujenga Ufahamu na Ujuzi katika maeneo muhimu ya kiuchumi kwa Taifa, miongoni mwa maeneo hayo ni kilimo na uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo; viwanda, usafirishaji, Tehama, nishati, ujenzi na maeneo ya utalii na huduma ambayo uhandisi una mchago mkubwa.” Amesisitiza Ndalichako

Aametoa wito kwa wahandisi hao kuhakikisha wanafanya jitihada zaidi ya kutafuta njia za kuendeleza matokeo ya tafiti wanazofanya na kuziweka katika vitendo ili ziweze kuchangia ipasavyo ukuaji wa sekta ya viwanda nchini. 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa zawadi kwa Mhandisi Mama Kinasha ambaye ni miongoni wa wahandisi wa wa kwanza kusajiliwa na Taasisi ya Waandisi wakati wa ufunguzi wa Kongamano na Maonesho ya Wahandisi Wanawake wa Taasisi ya Wahandisi iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Wahandisi Patrick Balozi amesema katika kufanikisha azma ya kuwa na  uchumi wa viwanda ni muhimu kama Taifa kuongeza idadi ya Udahili kwa wanaunzi wa fani za uhandisi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yatakayowavutia wanafunzi kupenda masomo ya sayansi

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa washiriki wa maonesho ya ubunifu katika toa ufunguzi wa Kongamano na Maonesho ya Wahandisi Wanawake wa Taasisi ya Wahandisi iliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WALIMU KUHAMASISHA WANAFUNZI KUSHIRIKI MAONESHO YA UBUNIFU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amewataka walimu wa shule za Sekondari kuwahamisha na kuwasaidia wanafunzi kuandaa bunifu zao  ili waweze kushiriki katika maonesho  mbalimbali ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanayofanyika nchini.

Akizungumza katika sherehe za utoaji wa zawadi kwa washindi wabunifu walioshiriki katika Monesho ya nane ya taasisi ya Wanasayansi Chipukizi (YST) Jijini Dar es Salaam Waziri Ndalichako amesema ushiriki wa wanafunzi katika maonesho hayo utawasaidia kuinua vipaji vyao na kupenda masomo ya sayansi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikabidhi zawadi kwa washindi wa maonesho ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Shule ya Sekondari Msalato. Waziri Ndalichako  amewahimiza wanafunzi nchini kushiriki katika maonesho mbalimbali ya namna hiyo ili kukuza vipaji vyao.

Ndalichako amesema anatambua kuwa maonesho hayo yamesaidia mamia ya wanafunzi wa shule za sekondari nchini kuonyesha bunifu zao ambazo zimewawezesha  kuendelea kutafuta  maarifa ya kisayansi yatakayosaidia nchi kufikia  uchumi wa viwanda.

Waziri Ndalichako amesema Wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH) itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo kuangalia namna bora ya kuinua vipaji na kuboresha tatifi zinazofanywa na wanafunzi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimpongeza mmoja wa washindi wa kwanza wa bunifu zilizoonyesho katika maonesho ya Sayansi , Teknolojia na Ubunifu kutoka Shule ya Sekondari Msalato.

Katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, Taasisi hiyo imeweesha zaidi wanafunzi elfu tano (5,000) kushiriki katika maonesho ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu zaidi ya 1000 wa shule za sekondari ya namna ya kusaidia na kuboresha tafiti zinazofanywa na wanafunzi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akishangilia na kufurahia pamoja na wanafunzi walioshinda zawadi mbalimbali katika maonesho ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyoshirikisha shule mbalimbali nchini.


Alhamisi, 2 Agosti 2018

NDALICHAKO: ANDAENI WANAFUNZI WENYE UJUZI NA UMAHIRI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako amekiagiza Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kuhakikisha kinaandaa wanafunzi mahiri na wenye ujuzi utakaowawezesha kuchangia katika uchumi wa Taifa.

Ndalichako ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa hosteli ya wanafunzi, uliofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na watendaji pamoja na wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (hawapo pichani) wakati wa kuzindua  hosteli ya wanafunzi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 720 kwa mara moja.

 Amesema kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza Dira ya Elimu ambayo inataka Taifa kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

 Waziri Ndalichako ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuingiza masomo ya uongozi, maadili na uzalendo katika mitaala ya ngazi zote za kitaaluma kwa kuwa ni muhimu katika kuwajengea vijana uzalendo, moyo wa kujituma na kulipenda Taifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizindua hosteli katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuwataka wanafunzi wa Chuo hicho kutunza miundombinu hiyo ili iweze kuwasaidia wanafunzi wengine watakaojiunga na Chuo hicho.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Profesa Shadrack Mwakalila amesema hosteli hiyo ni ya ghorofa 5 na ina uwezo kuchukua wanafunzi 720 kwa mara moja hivyo kupunguza tatizo la malazi ya wanafunzi katika chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya miundombinu katika hosteli mpya aliyoizindua katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.