Jumatano, 31 Oktoba 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz



  
Chuo cha Masomo ya  Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S. L. P. 10,
40479 DODOMA.           



TAARIFA KWA UMMA
KUFANYA MALIPO KUPITIA MFUMO MPYA WA SERIKALI WA GePG
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kuutaarifu Umma ya kwamba kuanzia tarehe 01 Novemba 2018, itahamia rasmi katika mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali kwa njia ya kieletroniki ujulikanao kama ‘Government e-Payment Gateway’ (GePG) kwa matakwa ya Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348.

Wizara, itaanza kutumia mfumo huu kwenye makusanyo yake yote ya mapato kwa Vyuo vya Ualimu vya Serikali, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Kanda za Uthibiti Ubora wa Shule. Hivyo mteja atapaswa kufika au kuwasiliana na kituo husika anachotaka kufanya malipo ili kupata namba ya utambulisho wa malipo husika (Payment Control Number) kabla ya kufanya malipo.

Wizara kwa kushirikiana na Wataalamu wa mfumo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango itahakikisha mfumo huu unafanya kazi bila kuathiri utoaji wa huduma. Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaungana na Wizara na Taasisi nyingine za Serikali zinazotumia mfumo huo kwa mafanikio. Baadhi ya Wizara na Taasisi hizo ni Polisi, Brella, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, TRA, Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) pamoja na Mamlaka ya Maji.
Namna ya kulipa kwa kutumia mfumo wa kieletroniki (Government e-Payment Gateway);
1.   Malipo yanaweza kufanywa kwa njia ya kibenki kwa kufuata hatua zifuatazo;
a)     Unapopata kumbukumbu ya malipo (Control Number);
b)     Tembelea Tawi lolote la Benki ya CRDB, NMB na NBC;
c)      Baada ya kuwasili kwenye benki, mpe mtoa huduma wa dirishani namba kumbukumbu ili kukamilisha mchakato wa malipo yako.

2.    Malipo yanaweza pia kufanywa kwa njia ya mtandao wa simu za mikononi (M-pesa, Tigo Pesa na Airtel Money) kwa kufuata hatua zifuatazo;
a)     Kupitia simu yako, piga *150*00#, au *150*01# au *150*60#;
(Kupata M- pesa, Tigo Pesa na Airtel Money);
b)     Chagua ‘Lipia malipo (Pay-Bills)’;
c)      Chagua ‘Malipo ya Serikali’;
d)    Chagua ‘Ingiza namba ya malipo’ na uingize namba ya kumbukumbu ya malipo (Control Number);
e)     Weka kiasi cha fedha unachotaka kulipa;
f)      Thibitisha muamala wako kwa kuingiza neno au namba yako ya siri; na
g)     Hifadhi ujumbe wa simu uliopokea kama ushahidi wa malipo endapo utahitajika kuonyesha kwa kituo husika.

Imetolewa na;

Dkt. Leonard D. Akwilapo
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


Jumanne, 30 Oktoba 2018

WABUNGE WAIPONGEZA WIZARA YA ELIMU KUSIMAMIA VIZURI PROGRAMU YA LIPA KULINGANA NA MATOKEO


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo leo amewasilisha taarifa ya tathmini ya Ubora wa elimu kutokana na Utekelezaji wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.


Akiwasilisha tathmini ya programu ya EP4R kwenye Kamati hiyo ya Bunge Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa programu imekuwa na mafanikio tangu ilipoanza kutekelezwa mwaka 2014.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwasilisha taarifa ya tathmini ya ubora wa Elimu kutokana na utekelezaji wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo wakati wa kikao na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii jijini Doodma.

Dkt. Akwilapo amesema fedha zinazopatikana kutokana na utekelezaji wa vigezo (DLRs) katika ngazi ya Serikali kuu na serikali za Mitaa ni kuwa fedha hizo hutumika katika kuboresha utoaji wa elimu nchini kwa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ikiwemo ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya.

Dkt. Akwilapo ameieleza kamati hiyo ya Bunge kuwa programu ya EP4R ni ya miaka minne na inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Serikali ya Sweden (SIDA) na Serikali ya Uingereza (DFID) na kuwa mradi huo utakamilika 2020.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge Peter Serukamba na Mbunge wa Nzega Mhe. Hussein Bashe wameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa mradi huo wa EP4R ambao umekuwa na matokeo chanya katika nchi.

“Katika kusimamia Programu hii ya EP4R, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya kazi nzuri na matokeo yanaonekana. Miundombinu imeboreka sana,” alisema Mhe. Hussein Bashe.

Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii wakifuatilia Taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) Jijini Dodoma


Taarifa zinazowasilishwa kwenye kamati hiyo ni pamoja na ile ya mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo, taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa na utekelezaji wa shughuli za Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni, jijini Dar es salaam.

Kikao hicho cha siku tatu kimeanza leo na kitakamilika Novemba 1, mwaka huu.

PROF NDALICHAKO: TATUENI CHANGAMOTO ZENU KIMIFUMO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewashauri watumishi wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto za mikopo ya Wanafunzi kwa njia ya mifumo.
Waziri Ndalichako amesema hayo jijini Dar Es Salaam alipotembelea ofisi ya HESLB lengo la kujiridhisha na hali ya mwenendo wa utoaji mikopo kwa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2018/2019.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (mwenye koti la samawati) akiongea na wateja waliofika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es Salaam kurejesha madeni yao ya mikopo ya Elimu ya juu.
Katika ziara hiyo licha ya kukutana na Menejimenti ya HESLB, Prof. Ndalichako pia aliongea na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) Profesa Charles Kihampa kuhusu hali ya udahili wa Wanafunzi wa Elimu ya juu ambapo Kihampa alitumia nafasi hiyo pia kukabidhi orodha ya Wanafunzi 2,600 ambao udahili wao umethibitishwa.
Awali katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru ilisema kiasi cha shilingi bilioni 98.12 mpaka sasa kimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 27,929 kati ya wanafunzi 40,485 wa mwaka wa kwanza waliotarajiwa kupatiwa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Katikati) akitambulishwa kwa Maafisa Mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdul-Razaq Badru.
Badru alisema kuwa idadi ya wanafunzi waliobaki wapatao 12,556 watapangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 42 katika awamu inayofuata ili kukamilisha idadi iliyokusudiwa.

Aliongeza kuwa idadi ya wanafunzi 27,929 waliokwishapangiwa mikopo na ambao wamedahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vinavyotambulika ni asilimia 69 ya wanafunzi 40,485 wanaotarajiwa kunufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019.

Orodha ya majina ya wanafunzi hao  27,929 (Awamu ya kwanza 25,532 na awamu ya pili 2,397) waliokwishapangiwa mikopo inapatikana kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz  na itatumwa kwenye vyuo husika kwa ajili ya hatua zaidi za kukamilisha malipo ya mikopo hiyo.

Jumamosi, 27 Oktoba 2018

DHAMIRA YA SERIKALI YA KUWA NA CHUO KIKUU CHA KILIMO BUTIAMA IKO PALEPALE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema dhamira ya Serikali ya kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere kwa kuwa na Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia, (MJUNAT) iko palepale.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo akiwa Wilayani Butiama mkoani Mara mara baada ya kutembelea Chuo hicho kwa lengo la kukagua miundombinu yake, pamoja na kuzungumza na watumishi wanaofanya kazi chuoni hapo.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima wakitoka nje mara baada ya kukagua  bwalo la chakula katika Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na Watumishi wa Chuo hicho pamoja na viongozi wa Mkoa na wale wa Wilaya ya Musoma na Butiama amesema hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za makabidhiano ya miundombinu hiyo kutoka kwa aliyekuwa mmiliki wa majengo hayo Nimrod Mkono.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Moshi Kabengwe na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia CPA (T) Rose Waniha wakifuatilia jambo wakati wa kikao cha Waziri kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani BUTIAMA mkoani Mara.

Waziri Ndalichako amesema lengo la kuwa na Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia ni kumuenzi baba wa Taifa kwa kutambua mchango wake katika suala la kilimo na kuwa suala hili pia limeanzishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi.


“Mchakato huu ulianza mwaka 2016 na kuwa hapo awali majengo haya yalikuwa yanamilikiwa na Nimrod Mkono, hivyo Serikali haiwezi kujenga au kuboresha bila kuwa na maandishi ya kisheria ya umiliki halali. Napenda kueleza kuwa makabidhiano yako katika hatua za mwisho ili Serikali iweze kuendelea na taratibu nyingine” alisema Ndalichako.
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokelewa na Watumishi katika Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere, kilichopo Butiama, Mkoani Mara.

Ijumaa, 26 Oktoba 2018

SERIKALI YAAHIDI KUTOA MILIONI 700 KUBORESHA SHULE ALIYOSOMA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE


Serikali imeahidi kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kujenga na kukarabati Miundombinu mbalimbali katika shule ya msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere iliyopo manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako mara baada ya kutii maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli ya kuitembelea shule hiyo na kufanya tathmini kwa lengo la kuikarabati ili iendane na hadhi ya Baba wa Taifa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima wakiwa wamekaa kwenye dawati alilokuwa anatumia Baba wa Taifa Mwalimu Jullius Nyerere wakati akisoma katika shule ya Msingi Mwisenge iliyopo manispaa ya Musoma, Mkoani Mara.


Waziri Ndalichako amesema, kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Tano ni Elimu, hivyo amemwelekeza Mkuu wa mkoa huo Adam Malima kuhakikisha kuwa fedha ambazo zitaelekezwa katika shule hiyo basi zisimamiwe ili zifanye kazi iliyokusiduwa na si kutumika vinginevyo.

“Rais John Magufuli akiwa katika ziara zake alifika na kuona kuwa shule hii inahitaji kuboreshwa hivyo alinielekeza nifike na kufanya tathmini kwa lengo la kuboresha Miundombinu ya Shule hii, sasa Mkuu wa mkoa mimi na wewe tuhakikishe uboreshaji unafanyika tena kwa kiwango kitakachoendana na hadhi ya Baba wa Taifa letu,” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri wa Elimu  na Mkuu wa mkoa wa Mara wakiwa nje ya bweni alilokuwa analala Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere katika shule ya msingi aliyokuwa anasoma ya Mwisenge iliyopo manispaa ya Musoma.


Waziri Ndalichako amesema fedha hizo zitatumika kujenga mabweni mawili mapya, vyumba vitano vya madarasa, kukarabati Nyumba za walimu na kuboresha Miundombinu ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo Adam Malima ameahidi kusimamia fedha zitakazotolewa kwa ajili ya kuboresha Miundombinu katika shule hiyo na kuwa shule hiyo itakuwa mfano na pia kumbukumbu nzuri kwa Taifa.

Waziri Ndalichako pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa huo pia wametembelea Shule ya sekondari ya Ufundi Musoma, Shule ya sekondari Mara na Chuo Kikuu Cha kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Butiama kwa lengo la kukagua hali ya Miundombinu katika Taasisi hizo.
Darasa ambalo Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere alilitumia kwa ajili ya kusoma kuanzia mwaka 1934 - 1936, shule hiyo ipo kwenye manispaa ya Musoma mkoani Mara.


Alhamisi, 25 Oktoba 2018

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA WATU WENYE ULEMAVU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 2 ya bajeti zao kwa ajili ya kuhudumia watu wenye ulemavu na kuwa suala hilo lipo kisheria.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe duniani ambayo Kitaifa hapa nchini yamefanyikia Mkoani Mwanza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya           Elimu Maalumu wa Wizara hiyo Adamson Shimbatano aliyeshika Fimbo Nyeupe wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe duniani ambayo kitaifa yamefanyikia mkoani Mwanza.

Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Magufuli imeendelea  kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa ajira na kuwa katika ajira za mwaka jana  walimu 70 wasioona waliajiriwa.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa Rais John Magufuli ni kiongozi anaejali sana watu wenye ulemavu ndiyo maana wapo viongozi wenye ulemavu aliowateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali yake wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Mabalozi, na wengine ili wamsaidie katika kutekeleza majukumu ya kuliletea Taifa Maendeleo,” alisema Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amewataka Wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wasioona na badala yake wahakikishe watoto wote waliofika umri wa kwenda Shule wanaandikishwa kwa kuwa hivi sasa Elimu msingi inatolewa bila malipo na kuwa ulemavu siyo kikwazo cha Maendeleo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea msaada wa Fimbo Nyeupe kutoka kwa mmoja Wafanyabiashara mkoani Mwanza, ili fimbo hizo zigaiwe kwa watu wasioona walioshiriki maadhimisho hayo mkoani Mwanza.

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu nchini Tanzania Benedict Louis amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa kutambua jitihada na uwezo wa watu wenye ulemavu na hivyo kuwateua wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali.

Louis ameeleza kuwa Siku ya Fimbo Nyeupe ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa wasioona kutathmini jitihada zinazofanywa na serikali katika kuleta ustawi kwa watu wenye ulemavu na kuwa Fimbo hiyo ni nyenzo muhimu ambayo inamsaidia asiyeona kutambua vikwazo vilivyo mbele yake.

Kauli mbiu  ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni “ Mafunzo ya TEHAMA kwa wasioona ni nyenzo Shirikishi ya uchumi wa Viwanda.”
Watu wasioona wakicheza mziki pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe ambayo kitaifa yamefanyikia mkoani Mwanza na kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni mafunzo ya TEHAMA kwa wasioona ni nyenzo shirikishi ya uchumi wa Viwanda.