Jumapili, 7 Julai 2019

UJENZI WA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SHULE WAANZA KWA KASI WILAYANI MISUNGWI


·        Naibu Waziri Ole Nasha afanya ziara kukagua asisitiza viwango katika utekelezaji wa mradi huo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kwa usimamizi mzuri wa mradi wa ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule wa wilaya hiyo inayojengwa katika kata ya Igokelo kijiji cha Mapilinga mkoani humo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa pongezi hizo alipofanya ziara katika Wilaya hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo ambapo amesema ameridhishwa na hatua ambayo ujenzi umefikia huku mkazo ukiwa kuzingatia ubora wa ujenzi wa jengo hilo.

“Kwa kweli mnakwenda vizuri, kama fedha mmepokea mwezi Mei mwaka huu tokea ujenzi uanze michakato yote ni kama mmetumia mwezi mmoja na tayari mmeshapaua ni jambo jema. Lakini niwapongeze zaidi kwa kuwa ujenzi huu miundombinu yake imezingatia watu wenye mahitaji maalum zingatieni ubora wa jengo katika kukamilisha kazi hii,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Saysnia na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Uthibiti ubora wa shule Wilaya ya Misungwi Jijini Mwanza.
Alisema ujenzi wa Ofisi za Uthibiti ubora wa shule ni mwendelezo wa nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuamua kuimarisha Idara ya Uthibiti Ubora wa shule ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa lengo la kuinua ubora wa elimu nchini.

Ole Nasha ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Elimu kwa kuwa zina lengo la kuimarisha elimu ya watoto wetu lakini pia kutumia fursa zinazokuja na miradi hiyo kujiingizia kipato kwani kwa sasa Serikali imeamua kutumia utaratibu wa Force Akaunti katika utekelezaji wa miradi yake kwani utaratibu huo umeonesha kuwa na mafanikio lakini pia unawanufaisha wananchi walio karibu na mradi unapotekelezwa.

“Wanamisungwi 34 wamefaidika na ujio wa mradi wa ujenzi wa ofisi hii ya Uthibiti ubora wa shule wapo waliopata nafasi ya kufanya kazi za ujenzi na wale wanaofanya bishara ya chakula na vinywaji na hili ndilo lengo la Serikali,’aliongeza Naibu Waziri ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo ya namna mradi wa ujenzi wa ofisi ya uthibiti ubora wa shule wilaya ya Misungwi unavyotekelezwa kutoka kwa Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule wa Wilaya ya Misungwi Faustin Salala.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa Ofisi hiyo Mthibiti Mkuu wa ubora wa Shule Wilaya ya Misungwi Faustini Salala alisema ujenzi wa ofisi hizo umeanza mwishoni mwa mwezi Mei 2019 na unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Agosti, 2019 na utatumia zaidi ya shilingi milioni 150.

Mradi wa Ujenzi wa ofisi ya Uthibiti Ubora wa shule katika wilaya ya Misungwi ni moja  ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa ofisi 100 za aina hiyo zinazojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchi nzima ili kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watendaji wa Idara hiyo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na baadhi ya Walimu pamoja na wananchi mara baada ya kukagua ujenzi wa ofisi za Uthibiti ubora Wilaya ya Misungwi. Amewataka kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu kwani inalenga kuboresha elimu ya watoto wetu.

Jumamosi, 6 Julai 2019

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM.


Serikali imesema inatambua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum na ndio maana inachukua juhudi za makusudi kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ili yawe rafiki kwao kupata elimu.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi walio katika Kambi ya Joto (Summer Camp) inayoratibiwa na Taasisi ya Under the Same Sun.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi walio kwenye ‘summer camp’ katika Chuo cha Ualimu Butimba Jijini Mwanza. Ametumia fursa hiyo kuelezea juhudi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya katika kutatua changamoto za watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu.

Naibu Waziri Ole Nasha alisema katika kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa sasa Wizara anayoiongoza inatekeleza Programu ya Elimu Jumuishi ambayo inamuweka shuleni mtoto mwenye ulemavu na yule asie na ulemavu kwa lengo la kuondoa fikra za kunyanyapaliwa lakini pia kujenga umoja upendo na urafiki baina yao utakaowawezesha kulindana kwani siku zote mlinzi mzuri ni rafiki na ndugu hivyo inasaidia kuondoa changamoto zilizopo.

Aidha, Serikali pia inatoa mikopo kwa asilimia mia moja kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma elimu ya juu kwa lengo la kuwasadia waweze kupata elimu zaidi kwani watu wenye ulemavu wakipata elimu wanaweza sio tu kujikomboa wenyewe lakini kuwasaidia watu wengine wenye changamoto hizo.

“Ninyi wenyewe mtakuwa mashahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika Serikali yake kuna viongozi ambao wana ulemavu lakini kutokana na umahiri na uwezo walio nao katika utendaji wameteuliwa katika nafasi hizo. Tambueni kuwa watu wote wana haki sawa na hilo liko wazi,” alisema Naibu Waziri ole Nasha.

Kiongozi huyo amewataka wanafunzi hao kutambua kuwa wao ni watoto wa kitanzania hivyo wanatakiwa kuwa huru kwenye nchi yao na kwamba Serikali itaendelea kuwalinda  ili waweze kuishi lakini pia kusoma kama watu wengine bila kudhuriwa na kitu chochote.

”wote ni mashahidi kwamba kwa  sasa Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba mnakuwa na usalama wa maisha yenu, sidhani kama kuna kosa ambalo sasa ukipatikana nalo unachukuliwa hatua kubwa zaidi kama kujaribu kuwadhuru watu wenye ualbino, na ndio maana sasa mnapata ulinzi kaeni mkiwa huru kwa kuwa serikali inawajali,”aliongeza Naibu  Waziri Ole Nasha.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha amelitaka Shirika la Under The Same Sun   kutambua kuwa Serikali inathamini mchango mkubwa wanaoutoa katika kuwasaidia  wanafunzi na watoto  wenye mahitaji maalum hasa watoto ambao wana changamoto ya ulemavu wa ngozi na kuwataka kuhakikisha mafunzo wanayoyatoa katika kambi za joto (summer camp) kila wanapokutana  pamoja na mambo mengine yalenge katika kuwaonesha watoto hao kuwa jamii inawajali na sio vinginevyo.
Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha wakati alipokutana nao kuzungumzia juhudi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya kutatua changamoto za watoto wenye ulemavu katika kupata elimu.

Nae Afisa kutoka Idara ya Elimu ya Shirika la Under the Same Sun Omary Mfaume amesema Shirika hilo linafadhili wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kupitia programu za elimu zinazojihusisha na ufadhili wa elimu na ile ya uhamasishaji jamii ambayo inayowafundisha kwanini mtu anazaliwa na ualbino, changamoto zake na namna ya kuzikabili changamoto hizo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Clara Maliwa ameiomba Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatambua Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wanaofanya vizuri katika masomo ili kutoa changamoto kwa wengine ili waweze kufanya vizuri zaidi.

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ATAKA CHUO CHA UALIMU BUTIMBA KUREJESHA MASOMO YA SANAA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amekitaka Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kufanya tafakari ya namna gani kinakuwa chachu ya mabadiliko katika kuandaa walimu wanaoendana na mahitaji ya sasa.

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 80 ya kuanzishwa Chuo hicho ambapo amesema mijadala itakayoendeshwa ijikite zaidi katika kujua ni namna gani wanabadili mfumo wa kufundisha ili wanafunzi waweze kuwa wabunifu na wanaojiamini.

“Nimeona katika maonesho yenu mna jaribu kufanya masuala ya ubunifu, ubunifu unaanza mwanafunzi akiwa mdogo na ndio maana tunasema lazima kufanya ufundishaji ambao toka mwanzo unampa mwanafunzi nafasi ya kuwa mbunifu. Usimbane mwanafunzi jaribu kumfungulia fursa mbalimbali kwani anapozaliwa anakulia katika mazingira mbalimbali ya ubunifu hapo utatoa nafasi ya kuweza kuendeleza ubunifu alio nao,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akizungumza katika Kumbukizi ya Miaka 80 ya Chuo cha Ualimu Butimba iliyofanyika katika  chuoni hicho  Jijini Mwanza.

 Alisema Chuo cha Butimba pamoja na kwamba ni chuo cha ualimu historia yake hasa iko katika ualimu ule wa Sanaa za maonesho, Sanaa za ufundi ni vizuri kuangalia ni namna gani Chuo hicho kinarudi katika msatri na kuendelea kutoa walimu ambao watasaidia katika kufundisha masomo hayo.

“Kwa bahati mbaya kuna mahali tulikosea kufikiri kwamba music, ufundi, Sanaa za maonesho hazina nafasi katika elimu, sio vibaya tukarekebisha sababu kama unataka kumfundisha mwanafunzi ubunifu huwezi kukwepa kutumia Sanaa za maonesho, music na tamaduni zake zote kwani zinamsaidia kuwa mwanafunzi kamilifu anaeweza kubuni,” aliongeza Naibua Waziri Ole Nasha.
Washiriki wakifuatilia hotuba ya Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kuadhimisha kumbukizi ya miaka 80 ya Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo Wilaya ya Nayamagana  Jijini Mwanza

Akizungumzia Jitihada zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia Ole Nasha amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeweka historia ya kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu kwa kujenga, kukarabati na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwenye shule.

Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine Serikali kuanzia mwaka 2016 inatekeleza Mpango wa Elimu bila malipo, mpango ambao haujawahi kuwepo ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu ambapo inatumia zaidi ya shilingi bil. 20 kila mwezi kugharamia elimu bila malipo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo  kutoka kwa wakufunzi wa Chuo cha Ualimu Butimba ya  namna wanavyotumia vifaa vinavyopatikana katika mazingira wanayoishi kufundishia.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Butimba Huruma Mageni amesema katika kuadhimisha miaka 80 ya Chuo hicho kinajivunia mambo mengi ikiwemo eneo la chuo kupimwa na kwamba rasimu ya hati ya chuo iko tayari. Pia inajivunia kuwa na vitengo ambavyo vinachangia kuboresha elimu nchini.

Alhamisi, 4 Julai 2019

UKARABATI CHUO CHA MAENDELEO YA MWANANCHI ILULA

OLE NASHA ATAKA COSTECH KUSIMAMIA HAKI MILIKI ZA KAZI ZA WABUNIFU


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini kusimamia wabunifu kupata haki ya umiliki wa bunifu zao.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo jijini Dar es Salaam, wakati alipotembelea mabanda ya Taasisi za Elimu zilizo chini ya Wizara zilizoshiriki maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa maarufu kwa jina la Sabasaba na kukutana na mmoja wa wabunifu aliyeomba serikali imtambue kwa kuwa amebuni nyenzo ya kufundishia mfumo wa sayari shuleni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha akipata maelezo ya bunifu mbalimblai zilizopo katika banda la VETA wakati alipotembelea maonesho ya 43 ya biashara za kimataifa jijini Dar es Salaam.
Alisema ni vizuri wabunifu wanapoandaa kazi zao zikatambuliwa na kupatiwa haki miliki ya bunifu au ugunduzi walioufanya lakini pia kuendelea kuwafadhili ili waweze kukuza bunifu zao.

“Ninyi COSTECH hakikisheni bunifu mbalimbali nilizoziona hapa sabasaba katika mabanda yetu haziishii katika maonesho tu, bali zikuzwe na tumieni nafasi hii ya maonesho kuwakutanisha wabunifu na wafanya biashara kwa ajili ya uzalishaji,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiangalia moja ya bidhaa zinazozalishwa na VETA wakati alipotembelea banda la Taasisi hiyo katika maonesha ya bishara za kimataifa Jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine Waziri Ole Nasha ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kukuza ubunifu na ujuzi na kuwataka kuendelea kusimamia bunifu mbalimbali za wanafunzi ili ziingie katika soko na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo ya matumizi ya vitabu kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba wakati alipotembelea banda la TET katika maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizoshiriki maonesho ya Sabasaba kwa mwaka 2019 ni pamoja na Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Mzumbe, Tume ya Nguvu za Atomiki nchini (TAEC), Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

NDALICHAKO AWASHUKIA VIKALI SKAUTI TANZANIA