Jumatatu, 12 Agosti 2019

SERIKALI YA TANZANIA KUIMARISHA TAFITI KWA AJILI YA KUKUZA NISHATI ENDELEVU NA KUIMARISHA TEKNOLOJIA YA MAJI

Serikali imeendelea kuongeza ubora  wa elimu na kukuza ujuzi ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza ajira nchini. Hii  imewezekana kwa kuweka sera, mifumo na miundo mbinu wezeshi kwa watanzania kuweza kupata ujuzi na umahiri unaohitajika katika kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya mpango wa  maendeleo 2025 na malengo endelevu ya milenia.

Kauli hiyo  imetolewa Jiji Arusha na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa tatu wa Kimataifa wa Nishati endelevu na Teknolojia ya maji (International Conference on Energy, Aquatech and Sustainability 2019, ICEAS) )wenye lengo la kujadili changamoto zinazokabili sekta  ya Nishati  hususan kukuza nishati mbadala na Teknolojia ya  Miundombinu ya maji na kuja na mapendekezo ya namna bora ya kutumia rasimali zilizopo katika jamii kukuza sekta hizo. 
 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa ufunguzi wa  Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa Nishati endelevu na Teknolojia ya maji (ICEAS) unaofanyika NM-AIST jijini Arusha.
Amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ambayo inajenga uchumi wa viwanda ni kuhakikisha kuwa elimu itolewayo inakuwa bora na kuendeleza ujuzi kwa watanzania ili waweze  kuongeza thamani katika mazao kutumia teknolojia ya kisasa, ambapo maji na nishati ni maeneo muhimu katika kutekeleza hili.

"Tunataka kuona  kama ni mkulima anakuwa na uwezo wa kuongeza thamani ya mazao kwa kutumia Teknolojia za kisasa na hasa kutumia tafiti zilizofanywa,"  alisema Waziri Ndalichako
Baadhi wa wajumbe wa Mkutano wa ICEAS wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mkutano huo jijini Arusha.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameipongeza Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kwa kuboresha kiwango  cha utafiti katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na programu wanazotoa.

"Mwaka 2017 hapa NM-AIST tumefanya uzinduzi wa vituo vinne vya umahiri vya Sayansi na Teknolojia katika elimu ya juu kwa lengo la kuhakikisha tunaboresha elimu yetu na kunakuwa na wigo mpana wa kufanya tafiti, tunaona sasa mnafanya vizuri na kuendana na moto wa Chuo ambao ni Taaluma kwa jamii na viwanda, na hata maji ya kunywa yanayotumika katika mkutano huu ni moja ya kazi za tafiti zinazofanyika hapa"aliongeza Waziri Ndalichako
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo ya tafiti zilizofanyika kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa Mkutano wa ICEAS unaofanyika katika Taasisi ya NM-AIST jijini Arusha.
Waziri Ndalichako kabla ya kutoa hotuba yake ametumia fursa hiyo kutuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, ndugu jamaa na marafiki kufuatia vifo vya watanzania vilivyosababishwa na ajali ya moto  jijini Morogoro Agosti 10, 2019. 

Naye Makamu Mkuu wa Chuo katika Taasisi ya Sayansi Teknolojia ya Nelson Mandela ambae pia ni  Mwenyekiti Mwenza wa ICEAS Profesa Emmanuel Luoga amesema mkutano huo umewaleta pamoja wataalamu wa nishati mbadala na endelevu na watafiti kutoka nchi mbalimbali ambapo mada 37 zitawasilishwa  wataalamu kutoka nchi 11 zilizoshiriki mkutano huo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akibadilishana mawazo na mmoja wa wajumbe wa mkutano wa ICEAS Jijini Arusha.
Mada zitakazojadiliwa  zitajikita katika maeneo ya mabadiliko ya tabia nchi, upatikanaji wa  maji, nishati mbadala na endelevu.

Aidha amesema Taasisi anayoingoza itaendelea kushirikiana na taasisi na vyuo vingine kutoka ndani na nje ya nchi kufanya tafiti zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii pamoja na kuendeleza viwanda.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akizungumza na uongozi wa Taasisi ya NM-AIST mara baada ya kuwasili katika Taasisi hiyo kwa ajili ya kufungua Mkutano wa ICEA unaofanyika katika Taasisi hiyo Jijini Arusha.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Afrika cha Nelson Mandela na Chuo cha Taifa cha Seoul cha  Korea chini ya uratibu wa Kituo cha Umahiri ambacho kinashughulika na  miundombinu ya maji na Nishati endelevu na Kituo cha umahiri cha ubunifu na Teknolojia ya Nishati na unafanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 12, 2019 katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Mkutano wa ICEAS mara baada ya kufungua mkutano huo unaofanyika kwa siku mbili katika Taasisi ya NM-AIST jijini Arusha.