Jumanne, 21 Januari 2020

TANGAZO LA KUJIUNGA NA VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatangaza nafasi za kujiunga katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) kwa mwaka 2020.
Sifa za Mwombaji ni mwananchi yeyote mwenye nia ya kupata ujuzi na maarifa mbalimbali.
Aina ya Mafunzo yanayotolewa ni:
1. MAFUNZO YA UFUNDI STADI- NGAZI YA I, II &III
  1. Ufundi Umeme wa Magari : (Ifakara, Katumba, Nzovwe, Rubondo, Same, Sofi, Kisangwa, Mto wa Mbu,Chala,Handeni, Ikwiriri, Karumo, Kilosa, Katumba, Kibondo, Kilwa Masoko, Kihiga, Mamtukuna, Malampaka, Kiwanda,Malya).
  1. Ufundi Mekanika, (Vyuo vyote vinavyofundisha Ufundi Magari).
  1. Ufundi Umeme wa Majumbani, (Vyuo vyote vinafundisha kozi hii).
  1. Ufundi  Magari : (Bigwa, Chala, Chilala, Handeni, Ifakara, Ikwiririri, Karumo, Kilosa, Kisarawe, Katumba, Kibondo, Kilwa Masoko, Kisangwa, Kihinga, Singida Mamtukuna, Malampaka, Malya, Masasi, Mbinga, Msinga, Mtawanya, Musoma, Mwanhala, Mwanva, Mto wa Mbu, Munguri, Nandembo, Newala, Ngara, Njombe, Nzega, Nzovwe, Rubondo, Same, Sengerema, Sofi, Urambo).
  1. Useremala: (Bariadi, Mtawanya, Chala, Chilala, Chisala, Handeni, Ifakara, Ilula, Ulembwe, Kiwanda).
  1. Uashi: (Vyuo vyote vinavyofundisha Uashi isipokuwa Mtowambu, Nzega, Ikwiriri, Buhangija, Kiwanda, Chilala, Bigwa na Sikonge).
  1. Ushonaji: (Vyuo vyote vinafundisha ushonaji isipokuwa, Arnatouglu, Handeni, Sofi).
  1. Upishi: (Urambo, Sofi, Singida, Same, Nzovw, Nzega, Njombe, Mto wa Mbu, Mwanhala, Mtawanya, Msanginya, Masasi, Mamtukuna, Kiwanda, Kisarawe, Kilosa, Ilula, Ikwiriri, Ifakara, Handeni, Arnatouglu, Bigwa na Bariadi).
  1. Uchomeleaji: (Gera, Ifakara, Karumo, Kisarawe, Kisangwa, Kiwanda, Malya, Mtawanya, Mwanhala, Munguri, Newala, Njombe, Nzovwe, Sikonge, Nzega, Sengerema, Sikonge, Sofi, Ulembwe na Urambo).
  1. Kompyuta: vyuo vyote vinafundisha isipokuwa, (Sofi, Sikonge, Same, Newala, Nandembo, Munguri, Mto wa Mbu, Musoma, Mtawanya, Msingi, Msanginya, Muhukuru, Masasi, Mamtukuna, Kiwanda, Kisangwa, Kisarawe, Ifakara, Handeni, Gera, Chilala na Arnatouglo).
  1. Kilimo na Ufugaji: (Chisalu, Gera, Kiwanda, Handeni, Ifakara, Ikwiriri, Kilosa, Kilwa Masoko, Kisangwa, Mamtukuna, Malampaka, Mamtukuna Malampaka, Malya, Muhukuru, Msanginya, Msingi, Mwanhala, Njombe, Nzovwe, Same, Singida, Bigwa, Tango, Urambo).
  1.  Utunzaji wa watoto (Day care): (Nzovwe, Bigwa, Mtawanya, Msingi, Mtawanya, Msinga, Masasi, Katumba, Chisalu).
  1. Elimu haina mwisho (Sekondari nje ya mfumo rasmi kwa wasichana tu): (Chilala, Ilula, Karumo, Katumba, Malya, Masasi, Muhukuru, Msanginya, Msinga, Msingi, Mtawanya, Mwanva, Mputa, Mto wa Mbu, Ngara, Njombe, Nzega, Nzovwe, Bigwa, Rubondo, Sengerema).
  1. Mpira fursa kwa Wanafunzi wa kike tu: (Sengerema, Nzovwe, Mputa, Masasi, Katumba, Bigwa na Nzega).
  1. Uongozaji Watalii: (Kilwa Masoko, na Ngara).
  1. Udereva: (Tarime, Kiwanda, Tango, Sofi, Sikonge, Rubodo, Nzega, Malya, Kilwa Masoko, Ikwiriri, Chala).
  1. Ufundi Bomba: (Kiwanda).

2. MAFUNZO MAALUM
    Muda hulingana na Mahitaji ya Wahusika
                i.                 Elimu ya Sekondari Nje ya Mfumo Rasmi (Elimu haina Mwisho)
              ii.                  Utunzaji wa Watoto Wadogo (Day Care)
            iii.Mpira fursa (Michezo)

3. MAFUNZO YA MUDA MFUPI
Mafunzo haya hutolewa kwa wananchi mbalimbali sambamba na vikundi mbalimbali kulingana na mahitaji yao.

Aidha, pamoja na mafunzo haya yaliyoainishwa hapo juu, washiriki watajifunza masomo yafuatayo ya Uelewa kulingana na mahitaji ya wahusika. Masomo hayo ni pamoja na: Kiingereza, Uraia, Uchumi, Hifadhi ya Mazingira, Ujasiriamali na Afya ya Jamii.

GHARAMA YA WASHIRIKI
Gharama kwa Mafunzo ya Ufundi Stadi na Mafunzo Maalum kwa mwanachuo wa Bweni na Kutwa malipo ni kama ifuatavyo:-
a)     Gharama kwa Wanachuo wa Bweni ni shs. 250,000/=

    1. Ada ya Mafunzo                     -TShs.  100,000/=
    2. Gharama nyingine                   -TShs. 150,000/=
Jumla                                        TShs. 250,000/=

NB: Gharama nyingine inajumuisha:

i)   Kitambulisho                                  -TShs      5,000/=
ii)  Fedha ya ukarabati             -TShs.   25,000/=
iii) T-shirt (sare)                      - TShs.   15,000/=
iv) Godoro                               - TShs.     5,000/=
v)  Vifaa vya mafunzo             - TShs    100,000/=


b)    Gharama kwa Wanachuo wa Kutwa ni shs. 245,000/=;

a)     Ada ya Mafunzo                 -TShs.  100, 000/=
b)    Gharama nyingine              -TShs.  145,000
       Jumla                                     -TShs- 245,000/=

NB: Gharama nyingine inajumuisha:

i)   Kitambulisho                    - TShs    5,000/=
ii)  Fedha ya ukarabati            -TShs.  25,000/=
iii) T-shirt (sare)                     - TShs. 15,000/=
iv) Vifaa vya mafunzo           - TShs 100,000/=
                                   - TShs 145,000/=

c)                       Kwa mafunzo ya Muda Mfupi ni Tshs 20,000/= kwa mshiriki kwa mwezi.

N.B - Ada kiasi cha Tshs. 100,000/- ilipwe kwenye mfumo wa Serikali na mwanafunzi atalazimika kupata Namba ya Malipo (Control Number) toka chuoni ili afanye malipo na gharama nyingine zilipwe kwenye akaunti ya Chuo na zitakatiwa risiti ya Chuo.  Ada inaweza kulipwa kwa awamu mbili (2) tu.

Imetolewa na:


KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Jumatatu, 20 Januari 2020

MKUTANO WA KIMATAIFA WA ELIMU JIJINI LONDON UINGEREZA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako na baadhi ya wataalamu wa elimu kutoka Tanzania  wakiwemo kutoka  Washirika wa Maendeleo kutoka "DFID" Tanzania na British Council Tanzania wanashiriki Mkutano wa Kimataifa wa Elimu jijini London, Uingereza ambapo ajenda kuu ya mkutano huo ni nini kifanyike kuboresha Elimu ndani ya kizazi kimoja "One Generation."


Mkutano huo unawaleta pamoja Mawaziri wenye dhamana ya Elimu na wataalamu katika Sekta ya Elimu kutoka nchi 120 ambapo pia watajadili kuhusu mfumo sahihi wa upimaji uelewa wa wanafunzi na iwapo matokeo ya mwanafunzi yanatokana na mwanafunzi mwenyewe, Mfumo, Walimu au Mitaala.


Mengine yatakayojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na uboreshaji Mazingira  ya utoaji elimu kwa ajili ujifunzaji, uboreshaji Elimu jumuishi, uimarishaji Elimu ya Ufundi katika kuongeza Vijana wenye ujuzi, umuhimu wa vipaumbele vya elimu katika ngazi zote za elimu  kuwiana, maendeleo ya Teknolojia  yanavyochagiza na kutumika katika ujifunzaji na ufundishaji, umuhimu wa  kuwa na takwimu sahihi za Kitaifa za Sekta na pia umuhimu wa uwekezaji katika elimu ya awali katika ujifunzaji.

Jumapili, 19 Januari 2020

NDALICHAKO AKABIDHIWA MAGHOROFA YA NSSF KWA AJILI YA HOSTELI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako Jumamosi Januari 18, 2020  amekabidhiwa rasmi maghorofa 32 ya NSSF yatakayotumika kwa ajili ya kutoa huduma ya Hosteli kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Watu wenye Ulemavu Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema mpango huo wa NSSF umetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli ambapo Wizara yake ilisimamia utekelezaji wake huku akieleza kuwa awamu ya pili NSSF watakamilisha majengo ambayo yatawezesha wanafunzi wengine zaidi ya 4000 kuishi.

Nae Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Joyce Ndalichako amemshukuru na kuwapongeza  Rais kwa uamuzi huo na kuongeza kuwa hiyo ni moja tu ya hatua kubwa anazoendelea kuchukua katika kuboresha Sekta ya Elimu.
Profesa Ndalichako amesema hatua hiyo itapunguza changamoto ya uhaba wa Hosteli za wanafunzi wa Elimu ya juu hapa Dar es Salaam na ameishukuru na kupongeza Bodi na Uongozi wa NSSF kwa utekelezaji wa haraka wa agizo hilo na kukamilisha mahitaji muhimu ya miundo mbinu katika Majengo hayo kwa wakati.

Majengo hayo yako eneo la Mtoni Kijichi, Wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam na yatahudumia wanachuo  4,317 kutoka Chuo cha Kumbukumbu  ya Mwalimu Nyerere, Chuo cha Usimamizi wa fedha IFM, Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA)Chuo cha Diplomasia  na Taasisi ya Teknolojia  Dar es Salaam.

Jumamosi, 18 Januari 2020

MAHAFALI YA 11 YA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA

Naibu Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amewataka vijana wanaohitimu katika vyuo vya ufundi kujikita katika kuanzisha ajira mpya kwa kujiajiri badala ya kusubiria nafasi chache za ajira zilizopo ikiwa ni pamoja na kutumia ujuzi wao na taalamu katika kuihudumia jamii na kupata manufaa ya kiuchumi.


Akizungumza katika Mahafali ya 11 ya Chuo​ cha Ufundi Arusha yaliyofanyika Jijini Arusha Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wahitimu hao kuwa na uthubutu wa kuanzisha ajira zao wenyewe hata katika kiwango cha chini kwani zitaweza​ kukua na kuwafanikisha malengo yao.

Nasha amewataka wahitimu hao wasikae majumbani wakisubiri ajira bali waanzishe miradi midogo midogo itayowasaidia na kusaidia jamii zao hivyo kusukuma gurudumu la maendeleo.

“Hakika Mafanikio katika maisha yenu hayatategemea tu elimu ya ufundi bali yatatokana na nidhamu na uthubutu .Ninafahamu zipo changamoto katika kujiajiri lakini muhimu kuliko yote ni kuwa na nia na uthubutu .Eneo​ la ufundi lina fursa nyingi sana,” anaeleza Naibu Waziri wa Elimu.

Naye Balozi wa Norway nchini Tanzania, Elisabeth Jacobsen ​ amesema kuwa Norway itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha elimu ya Ufundi ambayo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo katika kufikia uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda kama iliyo azma ya serikali.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Dr. Masudi Senzia amesema kuwa chuo hicho kimeongeza udahili wa wanafunzi wa kike katika masomo ya kike kutokana na idadi ndogo ya​ vijana wa kike wanaojiunga na elimu ya Ufundi .

Masudi ameiomba serikali iwapatie fedha za kujenga shule za bweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike ambao asilimia kubwa wanaishi nje ya chuo.

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ufundi ​ Arusha (ATC, Chacha Makamba Wambura ​ amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano katika kuboresha elimu ya ufundi na kujenga miundombinu rafiki na vifaa vya kisasa vya kujifunzia suala linalopelekea kupata wahitimu waliobobea katika fani zao.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo kuhusu mitambo ya kisasa inayotumika kufundishia katika Chuo cha Ufundi Arusha kabla ya kuanza mahafali ya kumi na moja ya Chuo hicho.

Jumla ya wahitimu 436 wamemaliza katika Chuo cha Ufundi Arusha na kutunukiwa vyeti katika ngazi ya Astashahada, Stashahada, Shahada ya juu na Shahada.

UZINDUZI WA KITUO CHA MAFUNZO YA KUFUA UMEME

zaidi ya shilingi bilioni 8.5 zimetumika katika kukarabati na kujenga  majengo mpya katika kituo cha mafunzo ya kufua umeme wa nguvu ya maji cha Kikuletwa kinachomilikiwa na Chuo cha Ufundi Arusha


Akizungumza kabla ya kuzindua kituo hicho  Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amesema kituo hicho ni sehemu ya mpango mkakati mkubwa wa Serikali wa kuleta mapinduzi katika utoaji wa Elimu ya Ufundi nchini na Afrika Mashariki kutokana na kutoa mafunzo kwa vitendo yatakayosaidia kupata mafundi mahiri waliobobea katika fani yaa kufua umeme.

“Elimu itakayopatikana hapa itawasaidia vijana kuitumia elimu hiyo kujiajira kwani kuna fursa nyingi kwenye kujiajiri kuliko kusubiri fursa chache zilizopo za kuajiriwa, nani uhakika vijana wanaotoka hapa watakuwa mahiri katika kufua umeme na wataweza kujiajiri na kuajiri wenzao” amesema Ole Nasha

Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa uanzishaji wa Kituo cha mafunzo cha kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji hapa Kikuletwa umelenga kuhakikisha kuwa watalaamu; hasa mafundi stadi (artisans) na mafundi sanifu (technicians) wanapatikana ili kuongeza ufuaji wa umeme kutoka nyanzo vidogo vidogo vya maji na vikubwa pamoja kufanya tafiti juu ya nishati jadidifu (Research in renewable energy) ikiwemo uzalishaji umeme kutokana na nguvu ya maji.


Ole Nasha amesema serikali inatambua umuhimu wa Elimu ya ufundi kuelekea Tanzania ya viwanda ambapo inaendelea kufanya uwekezaji mkuwa katika vyuo vya ufundi, uwekezaji ambao umeongeza udahili na ubora katika Elimu ya ufundi. Kutokana na uwekezaji unaoendelea idadi ya wanafunzi wanaojiunga na mafunzo ya ufundi imeongezeka kutoka 30,000 mwaka 2015 hadi 151,969 mwaka 2019 pia inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya vya ufundi stadi 43 kwa gharama ya shilingi bilioni 92 katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na ujenzi wa chuo kipya Jijini Dodoma chenye hadhi sawa na ATC au DIT kwa gharama ya shilingi bilioni 18.

Aidha, Naibu Waziri ameongeza kuwa serikali imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa Elimu ya Ufundi Afrika Mashariki (EASTRIP) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 75 unaolenga kuleta mapinduzi katika Elimu ya ufundi nchini kwa kuvijengea vyuo uwezo ili viweze kuzalisha wanafunzi wenye ujuzi stahiki wa kuwawezesha kujiajiri ama kuajiriwa utawezesha ujenzi wa miundombinu bora na kuweka vifaa pamoja na kuwajengea uwezo wakufunzi.

Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Dkt.Masudi Senzia amesema kuwa tayari kituo hicho kimeanza kupokea wanafunzi ambao wanapata mafunzo katika fani mbalimbali za kufua umeme ambapo vijana wanaouzunguka eneo la Kikuletwa wamejitokeza kwa wingi​ kwa ajili ya kupata elimu itayowaezesha kujikwamua kimaisha.

Masudi amesema kuwa benki ya dunia ina mpango wa kutoa fedha kwa ajili ya kukiboresha kituo hicho cha mafunzo ili nchi za Afrika Mashariki ziweze kutumia chuo hicho kama kituo cha umahiri .

Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania Elizabeth Jacobsen amesema kuwa Norway itaendelea kuimarisha ushirikiano mwema uliopo baina ya nchi hizo ikiwa ni pamoja na kuijengea Tanzania uwezo katika masuala ya nishati jadidifu itakayosaidia kufikia uchumi wa kati na Tanzania ya Viwanda.

Balozi Elizabeth amesema kuwa kituo hicho kitasaidia katika mafunzo ya jinsi ya kuongeza uzalishaji wa umeme unaotokana na maji katika maeneo mbalimbali nchini huku ukilenga kujenga wataalamu waliobobea katika kufua umeme.

Mkuu wa Wilaya ya Hai,Lengai ​ Ole Sabaya amewataka wananchi kushirikiana na kituo hicho katika kulinda miundombinu iliyoko ili iweze kuwanufaisha vyema watu wa Hai,Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.