Jumamosi, 26 Septemba 2020

UZINDUZI WA MKAKATI WA KITAIFA WA KUKUZA NA KUENDELEZA KISOMO NA ELIMU KWA UMMA

 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) imezindua Mkakati wa miaka mitano wa Kitaifa wa Kukuza na Kuendeleza Kisomo na Elimu kwa Umma.

Uzinduzi wa Mkakati huo ambao unaanza kutumika mwaka 2020 hadi 2025 umefanywa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe Jijini Dar es Salaam katika Ofisi za Tasisi ya Elimu ya Watu Wazima.(TEWW)

Akiongea katika uzinduzi huo, Prof. Mdoe amesema kuwa anaamini Mkakati huo utapunguza au kumaliza kwa kiasi kikubwa idadi ya Watanzania wasiojua Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

“Naamini Mkakati huu uliozinduliwa leo utakwenda kumaliza au kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu," amesema Prof. Mdoe.

Naibu Katibu Mkuu Mdoe pia ameitaka TEWW kuhakikisha kuwa wanaendesha programu ambazo zinaendana na mahitaji ya jamii na mabadiliko ya teknolojia.

"Niwaombe Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mjiongeze, muwe wabunifu, muendeshe programu zinazoendana na mahitaji ya jamii na mabadiliko ya teknolojia ambayo kwa sasa inakua kwa kasi," amesisitiza Prof. Mdoe.

Naye Mkurugenzi wa TEWW, Dkt. Michael Ng'umbi akiongea katika uzinduzi huo amesema Taasisi yake imeboresha mtaala ambapo sasa wanafunzi watakaosoma chuoni hapo watafanya mafunzo kwa vitendo kwa kipindi cha Semista nzima na watatakiwa kuanzisha vituo vya kufundisha vijana na watu wazima.

"Tumeboresha mtaala ambapo kwa sasa wataalamu wanaopata elimu hapa chuoni, kila mmoja atatakiwa kuanzisha kituo cha kufundisha elimu ya watu wazima. Hata kama kila mmoja atamfundisha mtu mmoja, tukiwa wanafunzi 6,000 tuna uhakika idadi kama hiyo ya watu wazima watapata mafunzo na kuondokana na kutokujua kuandika, kusoma na kuhesabu," amesema Dkt. Ng'umbi.

Jumatatu, 14 Septemba 2020

MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewataka wajumbe wa Baraza la  Wafanyakazi wa Wizara hiyo kutambua kuwa wana wajibu wa kuishauri Wizara na Serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na utekelezaji sahihi wa Dira, Dhima na Majukumu ya Wizara. 

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo Jijini Mwanza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 27 wa Baraza la 10 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ambapo amesema wajibu wa mabaraza kama vyombo vya ushauri na usimamizi ni kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao na wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo makubwa ya utendaji kazi yenye tija.

“Moja ya kazi za Baraza ni kuhakikisha kuwa watumishi wanatekeleza wajibu wao kwanza kabla ya kudai maslahi na wanapodai maslahi wanatakiwa kufuata misingi ya sheria na taratibu zilizopo,” alisema Dkt. Akwilapo.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa kuwepo kwa Baraza la wafanyakazi ni matokeo ya Sera ya kuwashirikisha Wafanyakazi katika uongozi wa pamoja mahali pa kazi na kwamba kufanyika kwa Mkutano wa Baraza ni kutekeleza maagizo, Sheria na Kanuni mbalimbali za ushirikishwaji na Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma za mwaka 2003, 2004 na 2005.

Dkt Akwilapo amewataka wajumbe wa Baraza pindi watakaporejea katika vituo vyao vya kazi kuwaelimisha watumishi wenzao umuhimu wa kutimiza wajibu wao ili kufikia malengo mapana ya wizara kwani njia pekee ya kufikia malengo hayo ni kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma. 

Katibu Mkuu Akwilapo ametumia fursa hiyo kuwapongeza Viongozi na Watumishi wa Wizara hiyo kwa kuwa sehemu kubwa ya kuwezesha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kuboresha Sekta ya Elimu hususan katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza Graciana Shirima  ameishukuru Menejimenti ya Wizara kwa kuhakikisha Mkutano wa Baraza unafanyika kwa wakati na kwamba Baraza jipya lina jumla ya wajumbe 66 waliopatikana kufuatia makubaliano yaliyosainiwa kwa  mkataba wa Baraza la Wafanyakazi kati ya Vyama vya Wafanyakazi TUGHE na CWT kwa upande mmoja  na menejimenti ya Wizara kwa upande mwingine.

KATIBU MKUU DKT AKWILAPO AAGIZA KUFANYIKA TATHMINI YA MAZINGIRA NA MIUNDO MBINU YA SHULE ZOTE

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo amewataka Wathibiti Ubora wa shule nchini kufanya tathmini ya mazingira na miundombinu ya shule katika kudhibiti majanga ya moto yaliyokithiri katika siku za hivi karibuni.

 Dkt Akwilapo amesema hayo kufuatia tukio la moto lililosababisha vifo vya wanafunzi 10 na kujeruhi wengine lililotokea katika shule ya Msingi Byamungu Islamic iliyoko Kyerwa Mkoani Kagera.

Akwilapo amewataka Wathibiti ubora wa shule kushirikiana na wataalamu kubaini vyanzo vya moto katika shule  na amesema sheria zipo na pindi shule itakapogundulika kukiuka taratibu wasisite kuzichukulia hatua.

 “Asubuhi ya leo tumepokea taarifa ya kuungua kwa shule ya msingi ya Byamungu  na watoto wamepoteza maisha, lakini matukio haya yamekuwa yanaongezeka hivyo kama Wizara tunawajibu kuhakikisha hili linapatiwa suluhisho kwa kutumia wataalamu,"aliongeza Dkt. AKwilapo

Aidha Dkt.Akwilapo amesema Wathibiti Ubora wa shule zaidi ya 400 wameajiriwa mmepewa ofisi na vitendea kazi, nataka kuona mabadiliko ya namna tunavyosimamia shule”alisisitiza Dkt. Akwilapo.

Katibu Mkuu Akwilapo ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa wazazi, walezi na Shule ya Msingi Byamungu iliyopo mkoani Kagera kwa kuondokewa na wanafunzi na kuwatakia uponyaji wa haraka majeruhi 6 ambao wanaendelea na matibabu.

Jumatano, 2 Septemba 2020

DR. LEONARD AKWILAPO ATAKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU KUANZISHA PROGRAMU ZA VIPAUMBELE VYA TAIFA

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ametoa wito kwa Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha vinaanzisha programu za masomo zinazoendana na vipaumbele vya kitaifa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akifungua  maonesho  ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam

Dkt. Akwilapo ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema kwa kuanzisha programu hizo nchi itaongeza ujuzi wa wataalamu na pato la taifa. 

Kiongozi huyo ametaja baadhi ya programu za kipaumbele kuwa ni mafuta na gesi, afya, hususani udaktari bingwa kwa ngazi za Uzamivu katika nyanja zote za magonjwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, upandikizaji figo, ini na uboho (bone marrow), tiba za ndani za moyo, na uhudumiaji wa wagonjwa wa dharura na mahututi (emergency medicine and critical care).


 “Tusingependa kama nchi kupeleka wagonjwa wetu nchi za nje kutibiwa, bali nchi za nje waje kutafuta tiba kwetu (medical tourism). Kwa kufanya hivyo tutaongeza ujuzi wa wataalamu wetu pamoja na pato la taifa,” amesisitiza Dkt. Akwilapo. 

Katibu Mkuu Akwilapo ameongeza kuwa pamoja na kuanzisha programu za vipaumbele, nchi kwa sasa inatekeleza miradi mingi mikubwa ambayo inahitaji wasomi wa kuendesha na kusimamia miradi hiyo, hivyo ni jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu kuhakikisha hili linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora na kwamba Serikali itaendelea kusomesha kwa wingi wataalamu katika fani na ujuzi adimu na maalum kwa mahitaji ya nchi. 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa vyuo mbalimbali vya elimu ya Juu nchini mara baada ya kufungua maonesho  ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam

“Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba hivi sasa baadhi ya vyuo vikuu vimeanza kuelekeza jitihada zao katika kutoa elimu ambayo inalenga kushughulikia changamoto za jamii na kuweka msisitizo katika maeneo ya kimkakati ya nchi kama vile Kilimo, Madini, Utalii, Uvuvi, Maliasili na Misitu na Afya,” amesema Dkt. Akwilapo.  

Katika hatua nyingine Dkt. Akwilapo ameendelea kuzitaka Taasisi za Elimu ya Juu kuona namna bora ya kupanua udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na ongezeko la udahili wa wanafunzi katika ngazi ya msingi na sekondari na kwamba wanapohitimu lazima wapate nafasi katika vyuo vya kati na vya juu ili kuweza kuwapa ujuzi wa kujiajiri na hivyo kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Mayunga Nkunya  amesema Tume pamoja na mambo mengine imefanikiwa kuimarisha mfumo wa utoaji ithibati ya mtaala, jambo ambalo lilionekana kuwa tatizo kwa muda mrefu na kwamba itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania katika sekta ya elimu ili kuhakikisha Watanzania wa ngazi zote wanapata elimu bora yenye kukidhi viwango vya ubora Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Charles Kihampa amesema lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujitangaza na kuonesha huduma na kazi wanazofanya pamoja na mchango wao katika ustawi wa elimu ya juu kwa mustakabali wa maendeleo ya sayansi, teknolojia na manuufaa yake kiuchumi na kijamii. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea maonesho hayo wamesema wamefurahishwa na kuwepo kwa maonesho hayo kwani yanatoa fursa ya kuonana na wahusika na kupata taarifa zinazowawezesha kuomba programu zinazoendana na ufaulu wao.

Jumla ya taasisi 67 za elimu ya juu zimeshiriki katika maonesho hayo.

Brass Band ikitumbuiza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Jijini Dar es Salaam

Jumanne, 1 Septemba 2020

WALIMU 100 NCHINI KUFUNDISHWA MBINU ZA KUFUNDISHIA LUGHA YA KIFARANSA

Serikali za Tanzania na Ufaransa zimeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundishia lugha ya Kifaransa kwa walimu 100 nchini ambao watakuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi 5,000 wa Kitanzania katika ngazi ya sekondari.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya Dola za Kimarekani 250,000 zitatumika ili kufanikisha mpango huo.
Katika kikao hicho wamekubaliana kufanyika kwa vikao vya kitaalamu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kituo cha Ubalozi wa Ufaransa (Alliance Francais) ili kupanga utekelezaji wa mafunzo hayo ya walimu.

Aidha, Balozi Clavier ameonesha kuwepo kwa fursa za Watanzania kusoma programu zisizopungua 2,000 za Kiingereza nchini Ufaransa. Ameeleza kuwa  Ufaransa inaandaa Maonesho ya Elimu ya Juu (Higher Education Fair) yatakayofanyika nchini Mei 2021 ambapo vyuo 20 vya Ufaransa vitashiriki kutafuta ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania na Sekta binafsi. 
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Akwilapo ameushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano katika kukuza na kuimarisha elimu ya Juu nchini kupitia ufadhili wa mafunzo hayo na kuagiza wahusika katika Wizara anayoisimamia kuhakikisha vikao vya kitaaluma vinafanyika ili mafunzo hayo yaweze kuanza kwa wakati uliopangwa.

Katibu Mkuu Akwilapo pia ameahidi kuweka wazi kwa Watanzania kuhusu kuwepo kwa fursa hiyo ya kusoma programu za Kiingereza nchini Ufaransa ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa hiyo.