Jumapili, 10 Oktoba 2021

BENKI YA DUNIA KUENDELEA KUFADHILI MIRADI YA ELIMU NCHINI

 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameishukuru Benki ya dunia kwa kuendelea kufadhili miradi ya elimu nchini ambayo imesaidia kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu na kuongeza Ubora.

Waziri Ndalichako amesema hayo jijini Dar es Salaam alipokutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick kwa lengo la kupitia taarifa ya tathmini ya miradi ambayo inatekelezwa kwa ufadhili wa benki ya Dunia katika Sekta ya Elimu nchini, kuainisha changamoto pamoja na kujua malengo ya mbele ya elimu ili kuhakikisha elimu inatoa mchango stahiki katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi wa nchi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick (hayupo pichani) wakati alipofika ofisi za Wizara jijini Dar es Slaam kufanya mazungumzo kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu inayofadhiliwa na Benki ya Dunia

Waziri Ndalichako ameelezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Mradi wa Lipa kulingana na Matokeo ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuwa ni kujenga Vyumba vya madarasa 10,409, matundu ya vyoo 20,507 mabweni 646, nyumba za walimu 91, majengo ya utawala 37, maktaba 49, maabara 29 na shule mpya 44.

Ametaja mafanikio mengine yaliyopatikana kutokana na kutekeleza Mradi huo kuwa ni kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa wathibiti ubora wa shule kwa kujenga ofisi mpya 155 na kufanya maboresho kwenye ofisi 31 na kuwapatia magari yanayowawezesha kuzifikia shule kwa ajili ya kuzikagua.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Viongozi wengine wa Wizara wakiwa katika picha ya pamoja  na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Mara Warwick mara baada ya mazungumzo ya pamoja yaliyohusu utekelezaji wa miradi ya elimu inayofadhiliwa na Benki ya Dunia  yaliyofanyika katika ofisi za Wizara Jijini Dar es Salaam

Mradi pia umewezesha, kuimarisha mifumo ya kuchakata takwimu kwenye sekta ya elimu ambapo kwa sasa takwimu zinakusanywa moja kwa moja kutoka shuleni jambo ambalo limeongeza ufanisi katika kupata takwimu za elimu kwa usahihi. Aidha mradi pia umewezesha kuimarisha uwiano kati ya kitabu na wanafunzi.

“Kwa kweli ninamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo na nchi marafiki, matunda yake tunayaona hasa watoto wa kitanzania wanapopata elimu bora, tutaendelea kufanya kazi kwa bidii li kuhakikisha kwa pamoja tunaleta maendeleo kwa watanzania,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimia na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick alipofika ofisi za wizara jijini Dar es Salaam kwa ajili kufanya mazungumzo  na Waziri huyo kuhusu masula ya elimu

Waziri Ndalichako ametaja miradi mingine inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kuwa ni Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambapo tayari benki ya Dunia imetoa USD milioni 74 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Mradi huo. Miradi mingine ni Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP) wenye lengo la kuongeza fursa na ubora wa program za mafunzo ya ufundi stadi, Mradi wa Kukuza na Kuendeleaza Ujuzi (ESPJ)  pamoja na Mradi wa HEET ambao utekelezaji wake unakwenda kuanza ukilenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika Vyuo Vikuu ili viweze kuchangia katika kukuza uchumi.

Mkurugenzi  Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick akizungumza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati alipofika ofisi za Wizara jijini Dar es Slaam kufanya mazungumzo na Waziri huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi Mara Warwick amesema wapo tayari kuendelea kufadhili miradi ya elimu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kuipongeza Serikali kwa kutimiza vigezo vilivyowezesha vya Mradi wa Elimu ya Juu kwa mabadiliko ya kiuchumi (HEET) kuanza utekelezaji.

Jumamosi, 29 Mei 2021

CHUO KIPYA CHA UFUNDI KUANZA KUJENGWA DODOMA​

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inajenga Chuo cha Ufundi katika Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 5000 ili kuongeza wigo na fursa za upatikanaji wa ujuzi na maarifa.​


Akizungumza katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa chuo hicho uliofanyika Jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema ujenzi wa chuo hicho utagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 17 kupitia mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) unaosimamiwa na Wizara.​

Katibu Mkuu huyo ameitaka kampuni iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa chuo hicho, CRJE East Africa Ltd. kuhakikisha inakamilisha ujenzi huo ndani ya miezi 18 kama Mkataba unavyoonyesha.​


“Leo tumesaini mkataba wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Dodoma, ni matarajio yangu kitakamilika kwa wakati na​ubora unaotakiwa ili malengo ya kuanzishwa kwa chuo hiki yaweze kutimia,” amesema Dkt. Akwilapo.​

Naye Meneja wa kampuni ya CRJE East Africa Ltd. tawi la Tanzania, Xu Cheng ameahidi kutekeleza mradi huo​ kwa ubora unaokubalika na kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.​


Mradi huo utahusisha ujenzi wa miundombinu ya Jengo la Utawala, Ofisi za Idara, nyumba za watumishi, mabweni, Zahanati, Vyoo vya wanafunzi na watumishi, karakana tatu na kituo cha kupoza umeme.​

Jumatano, 26 Mei 2021

Vyuo Vikuu vyahimizwa kufanya tafiti zenye tija kijamii na kiuchumi

 Vyuo Vikuu nchini vimehimizwa kujikita katika tafiti na bunifu endelevu zitakazosaidia kutatua changamoto mbalimbali za jamii pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.


Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.Leonard Akwilapo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Joyce Ndalichako wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Sita ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu yaliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema kuwa vyuo hivyo vinatakiwa kufanya tafiti zitakazoweza kujitofautisha na taasisi zingine za elimu na kwamba zilenge katika kuisaidia jamii kupunguza changamoto na kuleta maendeleo.

" Vyuo Vikuu lazima vifanye tafiti za kuilenga jamii visipofanya vitakuwa havina utofauti na shule za kawaida tafiti ziibue majibu kusaidia nchi kimaendeleo," amesema Dkt. Akwilapo.

Amebainisha kuwa tafiti zinazofanywa na vyuo vikuu huvisaidia kujiweka karibu na jamii pamoja na kujitangaza kimataifa kwani matokeo ya tafiti husambazwa sehemu mbalimbali.

Amekipongeza chuo hicho kwa kuandaa maadhimisho hayo kwa kutenga fedha zake za ndani huku kwani kinaonyesha dhahiri kilivyojipanga kutatua kero za jamii na kuchochea maendeleo ya viwanda.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema maadhimisho ya kilele cha wiki hiyo yamelenga kuonyesha jinsi gani UDSM haijajitenga na jamii kupitia tafiti na bunifu zilizowasilishwa.

Amesisitiza kuwa wiki hiyo ni kiungo muhimu kati ya chuo na umma huku akiwapongeza washindi na walioshinndwa kuendelea kutafuta kuendelea kutafuta mawazo mengine ya utafiti na ubunifu.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Utafiti wa chuo hicho Profesa Bernadeta Killian amesema maadhimisho hayo yalianza mwaka 2015 na sasa yanejikita katika kuhimiza rafiki za kiuchumi kulingana na uhitaji katika kukuza uchumi wa Nchi kupitia Viwanda. 

Katika kilele hicho tuzo na hundi za fedha taslimu zilizotolewa ikiwemo ya Jarida bora la mwaka 2021, Tuzo ya Idara iliyoleta fedha nyingi za utafiti chuoni hapo ilikwenda kwa Shule ya Biashara iliyoleta Sh Bil 2.5,  tuzo ya Mtafiti hodari wa mwaka 2021 imechukuliwa na Dkt.Samwel Lyimo na 

Tuzo ya Mbunifu hodari amepta Dkt.Budeba kutoka Chuo cha Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam DUCE.