Ijumaa, 30 Novemba 2018

DKT. AKWILAPO AWATAKA WAHITIMU WA ADEM KUBORESHA UTENDAJI KAZI

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewataka Walimu waliohitimu mafunzo  katika fani za uongozi katika Elimu na Uthibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanatumia maarifa na mbinu sahihi katika kutekeleza majukumu kwa lengo la kuboresha utendaji kazi ili kuliletea Taifa maendeleo.


Katibu Mkuu Wizara y Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wakati wa Mahafali ya 26 yaliyofanyika katika Chuo Cha ADEM, Bagamoyo mkoani Pwani

Dkt Akwilapo ameyasema hayo wakati wa mahafali ya 26 ya Chuo Cha Maendeleo ya Uongozi wa Elimu, ADEM Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo zaidi ya wahitimu 1000 wamehitimi mafunzo yao.

Amewataka wahitimu hao kuhakikisha kuwa wanaenda kufundisha pamoja na kuhakikisha wanawalinda na kusimamia haki za watoto  kwa mujibu wa Sheria.

“Mategemeo ni kuongezeka kwa utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na wanafunzi kuhudhuria shule, kiwango cha ufaulu kuongezeka   pamoja na kubaini changamoto zinazowakabili wanafunzi na kuzipatia ufumbuzi kwa utaratibu unaofaa,”alisema Dkt. Akwilapo.
Katibu Mkuu akizungumza na wahitimu hawapo pichani wakati wa mahafali ya 26 katika Chuo cha ADEM, Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.

Dkt. Akwilapo amewataka wahitimu hao  kujenga mahusiano na  mazingira mazuri kati ya shule na Jamii, kuhakikisha  umoja unakuwepo kati ya pande  zote tatu kwa maana ya walimu, wanafunzi na wazazi na  eneo hilo likifanikiwa basi Elimu yetu itakuwa imefanikiwa. 


Akizungumza katika mahafali hayo  Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Siston Masanja  amesema Chuo hicho kinawajibu wa kutoa mafunzo na   ushauri wenye lengo ka kuboresha Elimu nchini, huku akiendelee kuiomba Wizara kutenga fedha  kwa ajili ya  kuboresha miundombinu ya Chuo hicho.


Wahitimu wa mafunzo katika Chuo cha ADEM  wakati wa mahafali ya 26 yaliyofanyika chuoni Bagamoyo Mkoani Pwani


Dkt. Masanja pia amewataka wahitimu kuacha kubweteka kwa Elimu waliyoipata ADEM, na badala yake waende wakajiendeleze zaidi  kama  vitabu vya dini vinavyoelekeza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa na Mtendaji Mkuu wa ADEM Dkt. Siston Masanja wakati wa Mahafali ya 26 yaliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.