Ijumaa, 21 Desemba 2018

OLE NASHA: NI KOSA KUSAMBAZA NYARAKA ZA SERIKALI BILA IDHINI KWENYE MITANDAO


Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amesema ni kosa kusambaza nyaraka za serikali katika mitandao ya kijamii bila idhini ya Mamlaka husika, hivyo ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu na za kisheria kwa watumishi watakaobainika kusambaza nyaraka hizo.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Morogoro wakati akifunga semina ya mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo na kusisitiza kuwa hakuna mtumishi yeyote wa serikali asiyefahamu kuwa kutoa nyaraka za serikali bila idhini ni kosa la jinai.

“Kumekuwa na usambazaji wa nyaraka za serikali katika mitandao ya kijamii bila idhini na kwa bahati mbaya wakati mwingine unakuta nyaraka imewekwa mhuri wa siri lakini bado unaikuta huko, watumishi wa serikali lazima watambue kuwa kuna utaratibu wa kutoa nyaraka za serikali na kuna sheria ambazo zinawabana wale wote wanaotoa taarifa hizo bila kuidhinishwa”alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akizungumza na washiriki wa Wizara hiyo (hawapo Pichani) waliohudhuria mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu ambayo yamekamilika leo mkoani Morogoro.

Mhe. Ole Nasha amewataka watumishi hao kutambua kuwa hakuna taasisi yeyote inayoweza kufanya kazi bila kuwa na kumbukumbu au nyaraka hivyo amewataka kuhakiksha utunzaji mzuri na salama wa nyaraka hizo kwani ni nguzo muhimu katika kufanikisha utendaji wa majukumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali watu, Moshi Kabengwe amesema mafunzo hayo yametolewa ili kusaidia watumishi kufanya kazi ambazo zitaleta tija kwa jamii inayohudumiwa na kuondoa changamoto ambazo zimebainika katika utoaji wa huduma.



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya siku tano ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu ambayo yamefungwa leo mkoani Morogoro.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku tano na yameshirikisha watumishi zaidi ya 50 kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Makao Makuu, Vyuo vya Ualimu vilivyopo Morogoro na baadhi ya watumishi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA).
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu.

Alhamisi, 20 Desemba 2018


UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINISTRY OF EDUCATION, SCIENCE AND TECHNOLOGY

MASTERS’ STUDY OPPORTUNITIES TENABLE IN BELGIUM FOR 2019/2020 ACADEMIC YEAR

Call for Application

The Ministry of Education Science and Technology would like to inform the General Public about M
.asters’ study opportunities tenable in Belgium.  The Institute of  Development policy (IOB) of the University of Antwerp offers three fulltime one year Masters programmes each  with a high degree of specialization  in:-
 (a) Development Evaluation and Management;
 (b) Governance and Development; and
(c) Globalization and Development.

Interested and qualified Tanzanians are encouraged to apply.

Mode of application
Applicants are required to apply online.  Detailed information about the application procedures and scholarships can be accessed at:-

Note that the deadline for submission of the application is 1st April 2019.

Issued by
Permanent Secretary,
Ministry of Education, Science and Technology,
P.O. Box 10,
DODOMA.

Jumanne, 18 Desemba 2018

KATIBU MKUU DKT. AKWILAPO AWATAKA WATENDAJI WA WIZARA YA ELIMU KUBORESHA UTOAJI HUDUMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt.  Leonard Akwilapo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuboresha utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wadau wote wanaofika  katika Wizara hiyo.


Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua Semina ya Mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa baadhi ya Maafisa wa Wizara hiyo lengo likiwa ni kuwakumbusha Maafisa namna bora ya utoaji wa huduma ili kuleta ufanisi na tija wakati wa kuwahudumia wadau.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo (Hawapo pichani) wanaohudhuria mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa Maafisa wa Wizara hiyo, mafunzo hayo yanafanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Akwilapo amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina idara na vitengo hivyo amewataka watendaji wote kuzingatia kanuni, taratibu za za utumishi muda wote wanapokuwa wanawahudumia watu kutoka nje ya ofisi hiyo.

"Utumishi wa umma una maadili yake, sasa ni vyema mkayazingatia wakati mnapokuwa mnatekeleza majukumu yenu katika kuwahudumia wananchi, tumieni lugha nzuri na mhakikishe mteja anaridhika naamini kuwa baada ya mafunzo haya nahitaji kuona mabadiliko katika kuhudumia wateja na huduma anayopewa mteja ili kuepuka malalamiko,”alisisitiza Dkt. Akwilapo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimali Watu Sebastian Inoshi akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo (Hawapo Pichani) kuhusu Mafunzo ya Huduma kwa Wateja na Utunzaji wa Kumbukumbu.

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 toleo la tatu kifungu cha G 20 kinachoelekeza mtumishi kupatiwa mafunzo kazini ili kuboresha utendaji kazi wake.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Raslimali Watu Sebastian Inoshi amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watumishi wa Wizara kwa  kuwakumbusha umuhimu wa huduma kwa wateja na utunzaji wa kumbukumbu ili kuwawezesha kufanya kazi kwa weledi.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornad Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wanaoshiriki mafunzo ya Huduma kwa Mteja na Utunzaji wa Kumbukumbu kwa Maafisa wa Wizara hiyo yanayofanyika mjini Morogoro

Jumatatu, 17 Desemba 2018

WAZIRI NDALICHAKO AZITAKA TAASISI ZA UFUNDI KUFUNDISHA KWA VITENDO.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameziangiza taasisi zote zinazotoa Elimu ya Mafunzo ya Ufundi zilizo chini ya Wizara hiyo kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo ili kuwawezesha wanafunzi hao wawe wabunifu na waweze kujiajiri.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo wakati wa Mahafali 12 ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo amekagua miradi mbalimbali iliyobuniwa na wanafunzi wa taasisi hiyo pamoja na kuzindua jengo la mradi wa wanafunzi linalojengwa na wanafunzi kupitia mafunzo kwa vitendo.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi mfano wa hundi mmoja wa wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam aliyeshinda katika kuandaa mradi wa ubunifu wakati wakati wa Mahafali ya 12 ya Taasisi hiyo.

Waziri Ndalichako amesema lengo la serikali kutoa Mafunzo ya Ufundi ni kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi kwa kuwapa ujuzi utakaowasaidia kutatua changamoto zilizopo katika Jamii na kuwawezesha kuchangia katika ukuaji kwa uchumi nchini pamoja na kushiriki katika kujenga uchumi wa viwanda.

"Nimepata fursa ya kutembelea miradi mbalimbali iliyobuniwa na kutengenezwa na wanafunzi wakati wa mafunzo kwa vitendo inatia moyo kwani bunifu zote zimelenga kutatua matatizo yaliyopo katika jamii." alisema Waziri Ndalichako
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wanalojenga kupitia mafunzo kwa vitendo wakati wa Mahafali ya 12 ya Taasisi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Waziri Ndalichako pia amewataka wahitimu hao kuwa na nidhamu wanapokwenda kwenye soko la ajira na kuhakikisha bunifu zao zinawafikia wananchi na kutatua changamoto zilizopo badala ya kuishia katika maonesho.

Akizungumza katika Mahafali hayo Mkuu wa Taasisi hiyo Prof. Preksedis Ndomba amesema Taasisi ya DIT inajivunia bunifu mbalimbali ambazo taasisi hiyo  imezibuni, pia zimesaidia kuondoa  kuondoa changamoto katika Jamii ikiwemo mradi wa taa za barabarani ambazo zimewekwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo Simiyu na Dar es Salaam.

Kabla ya kushiriki sherehe za Mahafali hayo Waziri Ndalichako alizindua jengo la mradi wa wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wanalojenga kupitia mafunzo kwa vitendo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua jengo la mradi wa wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam wanalojenga kupitia mafunzo kwa vitendo wakati wa Mahafali ya 12 ya Taasisi hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.


Ijumaa, 14 Desemba 2018

OLE NASHA ASEMA KUSTAAFU SIYO ADHABU NI MAFANIKIO


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ameitaka Wizara hiyo kuweka mkakati endelevu wa kutoa mafunzo kwa watumishi kuhusu masuala ya kustaafu na sio kusubiria kutoa mafunzo hayo wakati mtumishi anakaribia kustaafu.

Mhe. Ole Nasha ametoa agizo hilo jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo wanaotarajia kustaafu ambapo amesema kustaafu ni mchakato ambao unaanza pale mtumishi anapoajiriwa hadi anapofikia umri wa kustaafu.

“Idara ya Utawala na Rasilimali watu mnapaswa kutambua kustaafu ni mchakato unaoanza tangu mtumishi anapoajiriwa.  Kama unataka kumtayarisha mtumishi aweze kustaafu vizuri au kumpa maarifa ya kumwezesha kuishi vizuri baada ya kustaafu unapaswa kuanza mapema na sio kusubiri kutoa mafunzo wakati mtumishi amebakiza mwaka mmoja au miezi sita kustaafu,”  alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akimkabidhi cheti mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kustaafu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mafunzo hayo yameandaliwa na Wizara hiyo ili kuwapatia maarifa ya ubunifu na uendeshaji wa miradi ya uzalishaji mali baada ya kustaafu.

Ole Nasha ameitaka Idara ya Utawala ya Wizara hiyo kuhakikisha inaweka kumbukumbu za watumishi vizuri na kwa usahihi ili kuepuka ucheleweshaji wa mafao unaosababishwa na kutotunza kumbukumbu za watumishi hao ipasavyo.

Naibu Waziri huyo pia amewataka watumishi kuelewa kuwa kustaafu siyo adhabu ni mafanikio hivyo wanapaswa kujitambua na kutumia taaluma waliyo nayo na maarifa waliyoyapata katika mafunzo kuendeleza maisha yao baada ya kustaafu.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya watumishi wanaotarajia kustaafu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mafunzo hayo yamefanyika Jijini Dodoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu, Gaudencia Mmasi amesema mafunzo hayo yamehusisha watumishi wanaotarajia kustaafu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na wale walio kwenye Vyuo Vya Ualimu, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Ofisi za Uthibiti Ubora wa Shule.

Akizungumza kwa niaba ya Washiriki wa Mafunzo hayo. Katibu wa washiriki wa mafunzo ya kustaafu, Peter Kyabwazi aliiomba Wizara kuyafanya mafunzo hayo kuwa endelevu ili kuwasaidia wastaafu.

Mafunzo hayo kwa watumishi ambao wanatarajiwa kustaafu yamefanyika kwa siku tano kuanzia Desemba 10 na kuhitimishwa leo.
Washiriki wa mafunzo ya kustaafu wakifuatlia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga mafunzo kwa watumishi wa Wizara hiyo wanaotarajia kustaafu.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz




Chuo cha Masomo ya Biashara
na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S.L.P. 10,
40479 DODOMA.

Tarehe: 14 Desemba, 2018.


WARAKA NA. 1 WA MWAKA 2018
MWONGOZO WA UUNDAJI NA UENDESHAJI WA KAMATI NA BODI ZA SHULE
Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Na. 25 ya mwaka 1978 na Rekebisho lake Sura 353 ya mwaka 2002 kila Shule ya Msingi na Sekondari sharti iwe na Kamati ya Shule (kwa shule za Awali na Msingi) au Bodi ya Shule (kwa shule za Sekondari) iliyo hai. Aidha, Serikali imekuwa ikitoa miongozo juu ya utaratibu wa kuunda na kuendesha Kamati na Bodi hizo.
Waraka huu unalenga kutoa mwongozo mahsusi kuhusu muundo, wajibu na uendeshaji wa Kamati na Bodi za shule.

1.0        KAMATI ZA SHULE ZA AWALI NA MSINGI/BODI ZA SHULE ZA SEKONDARI
1.1     Kamati za Shule za Awali na Msingi za Serikali na Zisizo za Serikali
Shule zote zitakuwa na Kamati (Kwa Shule za Awali na Msingi) na Bodi kwa Shule za Sekondari).

1.2   Sifa za Wajumbe na Utaratibu wa Uundaji wa Kamati na Bodi za Shule
a)            Itaundwa na wajumbe wasiopungua tisa (9),
b)            Diwani, Mwenyekiti na Katibu wa Serikali ya Kijiji/Mtaa (wa eneo shule ilipo) hawatakuwa na sifa ya kuwa wajumbe wa Kamati/Bodi ya shule. Hii ni kuepusha mgongano wa kiutendaji kutokana na jukumu lao la kuiwakilisha Serikali katika ngazi zao za utawala,
c)            Kamati itakuwa na vikao visivyopungua viwili (2) kwa mwaka. Mwenyekiti anaweza kuitisha kikao cha dharura kama kuna suala linalohitaji kujadiliwa,
d)            Wajumbe wa Kamati/ Bodi wanatakiwa wawe na sifa zifuatazo:
                                                  i.Wawe na elimu ya Kidato cha Nne au zaidi,
                                                ii.Wawe na shughuli halali za kujipatia kipato,
                                              iii.Uwiano wa wajumbe uzingatie jinsi zote mbili,
                                              iv.Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti achaguliwe na Wajumbe wa Kamati kutoka miongoni mwao.
e)            Kamati ya Shule itakuwa na kamati ndogondogo tatu (3) zifuatazo:
                                                i.     Kamati ya Taaluma, Malezi na Unasihi,
                                                ii.Kamati ya Fedha, Mipango na Miundombinu, na
                                              iii.Kamati ya Mazingira, Afya na Chakula.
f)              Wajumbe wa Kamati/Bodi za Shule watathibitishwa na Afisa Elimu wa Wilaya.


1.3 Wajibu na Majukumu ya Kamati ya Shule
a)            Kuandaa/kuidhinisha Mpango wa Maendeleo ya shule na mikakati ya utekelezaji wake,
b)            Kuitisha na kuendesha vikao vya wazazi na kutoa taarifa ya maendeleo ya shule,
c)            Kwa shule za serikali kuidhinisha matumizi ya fedha za shule na kusimamia matumizi bora ya fedha za uendeshaji na maendeleo ya shule,
d)            Kwa shule zisizo za serikali, kushauri namna bora ya matumizi ya fedha  kwa miradi ya maendeleo ya shule ikiwemo ukarabati wa miundombinu,
e)            Kuhimiza ujenzi wa shule na usafi wa mazingira ya shule na wanafunzi,
f)             Kwa shule za serikali, kusimamia ujenzi na ukarabati wa madarasa na miundombinu mingine na utunzaji wa mazingira ya shule,
g)            Kusimamia ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kuhakikisha kuwa walimu wanafanya kazi zao kwa ufanisi,
h)            Kuhakikisha wanafunzi wote wanahudhuria masomo kwa mujibu wa sheria,
i)             Kuhakikisha shule inakuwa na Sanduku la Huduma ya Kwanza na pia shule inadumisha elimu ya afya shuleni kwa njia mbalimbali,
j)             Kuhakikisha huduma za Malezi na Unasihi kwa wanafunzi zinaendeshwa kwa ufanisi shuleni,
k)            Kutathmini uhalali wa kumsimamisha/kumfukuza shule mwanafunzi bila upendeleo wala kushawishiwa na mtu au kikundi chochote kabla ya kuhalalisha uamuzi huo,
l)             Kuhakikisha Kamati inakutana ndani ya wiki mbili inapotokea shule imependekeza kumsimamisha/kumfukuza mwanafunzi ili uamuzi sahihi utolewe kwa wakati kuepusha ucheleweshaji unaoweza kuathiri haki za kielimu za mwanafunzi husika pasipo sababu za msingi, na
m)         Kamati itafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu (3).


2.0 MUUNDO WA KAMATI/BODI ZA SHULE
Katika kuunda Kamati na Bodi za Shule za Serikali na zisizo za Serikali mambo yafuatayo yatazingatiwa:

2.1   Wajumbe wa Kamati za Shule za Awali na Msingi za Serikali
                           i.            Mwalimu Mkuu ambaye pia atakuwa Katibu wa Kamati,
                        ii.            Mwalimu wa Taaluma katika shule,
                      iii.            Wawakilishi wawili (2) wa walimu shuleni,
                       iv.            Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo naye atakua Mjumbe,
                         v.            Wajumbe watatu (3) watakaochaguliwa na mkutano wa wazazi, na
                       vi.            Mkazi jirani atakayeteuliwa na Mkuu wa shule.

2.2     Kamati za Shule za Awali na Msingi Zisizo za Serikali
                             i.         Mkuu wa shule ambaye atakuwa Katibu wa Kamati ya shule,
                           ii.         Mmiliki wa shule,
                         iii.         Mwalimu wa Taaluma,
                         iv.         Wajumbe watatu (3) watakaoteuliwa na Mmiliki wa Shule,
                           v.         Mwakilishi mmoja (1) wa walimu shuleni.  
                         vi.         Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo naye atakua Mjumbe,
                    vii.            Mzazi mmoja (1) anayewakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi,
                  viii.            Mkazi mmoja jirani atakayeteuliwa na Mwenye shule.

2.3   Bodi za Shule za Sekondari za Serikali
                              i.         Mkuu wa Shule ambaye atakuwa Katibu wa Bodi,
                           ii.         Mwalimu wa Taaluma katika shule,
                         iii.         Wawakilishi wawili (2) wa walimu shuleni,
                          iv.         Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum; Mkuu wa Kitengo pia atakua mjumbe katika Bodi ya shule,
                            v.         Wajumbe watatu (3) wanaowakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo watakaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa wazazi, na
                          vi.         Mkazi jirani atakayeteuliwa na Mkuu wa shule.

2.4   Bodi za Shule za Sekondari Zisizo za Serikali
                    i.              Mkuu wa shule ambaye atakuwa Katibu wa Bodi ya shule,
                  ii.              Mmiliki wa shule,
                iii.              Mwalimu wa Taaluma,
                iv.              Wajumbe watatu (3) watakaoteuliwa na Mmiliki wa Shule,
                  v.              Mwakilishi mmoja (1) wa walimu shuleni.  
                vi.              Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo pia atakua Mjumbe,
              vii.              Mzazi mmoja (1) anayewakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi,
            viii.              Mkazi mmoja jirani atakayeteuliwa na Mwenye Shule.

Waraka huu unafuta Nyaraka zote za awali zilizokuwa zinatoa Mwongozo kuhusu Kamati za Shule za Awali na Msingi na Bodi za Shule za Sekondari na utaanza kutumika kuanzia Januari, 2019.




Dkt. Edicome C. Shirima

KAIMU KAMISHNA WA ELIMU



Nakala:      Makatibu Tawala wa Mikoa,
                    Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji,
                    Wathibiti Ubora wa Shule Wakuu Kanda na Wilaya.