Jumatano, 23 Septemba 2015

Waziri Kawambwa afanya ziara AIMS – Tanzania


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa mwishoni mwa wiki alitembelea Taasisi ya  African  Institute for  Mathematical  Sciences - Next Einstein Initiative (AIMS-NEI) kampasi ya Tanzania na kuzungumza na viongozi na wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika masomo ya  Hisabati na Sayansi kwa mwaka 2015/16. Taasisi ya AIMS hapa nchini imeanzisha kampasi yake Bagamoyo, mkoani Pwani ambapo hivi sasa inatumia kwa muda majengo ya Alpha Zulu Villa na baadaye itatumia majengo ya Old Boma na Datoo yaliyoko Bagamoyo mjini baada ya kufanyiwa ukarabati.
Wanafunzi 45 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wamedahiliwa kuanza masomo katika taasisi ya AIMS – Tanzania kwa mwaka 2015/16 wakiwemo Watanzania 17 na wengine wanatoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Cameroon, DRC, Msumbiji, Nigeria, Zimbabwe, Afrika Kusini, Sudani na mmoja anatoka Uingereza.
Kuanza kwa mafunzo hayo ni jitihada za Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na wataalam wa kutosha katika Nyanja za Hisabati na Sayansi. Mheshimiwa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo alipokuwa ziarani nchini Canada mwishoni mwa mwaka juzi.
 
 






 

 

 

Jumatano, 16 Septemba 2015


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAONESHO YA MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA ELIMU YA MSINGI
Wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi inaandaa maonesho ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ajili ya kuongeza Ufanisi katika Ujifunzaji na Ufundishaji katika Elimu ya Msingi nchini.
Maonesho haya yanalenga kutoa fursa kwa wabunifu, wauzaji na wadau wa elimu kuonesha bunifu mbalimbali za teknolojia ya habari na mawasiliano zitakazoweza kutumiwa katika Elimu ya Msingi ili kuongeza ufanisi katika Ujifunzaji na Ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) na katika masomo mengine.
Maenesho haya yatafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere mkoani Dar es Salaam, kuanzia tarehe 28/9/2015 hadi tarehe 02/10/2015
Washiriki wa maonesho haya wanatakiwa kujiandikisha kupitia wavuti: www.lanes-moe.go.tz, kabla ya tarehe 24/9/2015. Aidha, washiriki watakaokidhi vigezo vinavyotakiwa, kazi zao zitatumika katika Ujifunzaji na Ufundishaji katika Elimu ya Msingi Nchini.
Wizara inawahimiza wabunifu wote  wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maonesho haya.
Imetolewa na
Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
13/09/2015