Ijumaa, 28 Aprili 2017

Mwongozo wa Kitaifa wa huduma ya maji, Afya na usafi wa mazingira shuleni wazinduliwa.


Kaimu Kamishna  wa Elimu Nicholas Bureta amewataka wadau wa Program ya Maji, Afya na usafi wa Mazingira shuleni kurejea mipango yao ili kuona jinsi na mbinu ngani itumike katika kukabiliana na changamoto za miundombinu ya  Vyoo, Afya na usafi wa Mazingira zinazozikabili shule mbalimbali nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa huduma ya maji, Afya na usafi wa mazingira shuleni uliofanyika jijini Dar es Salaam amesema kuwa serikali imeboresha na kujenga miundombinu ya vyoo kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  ingawa bado kuna upungufu wa matundu ya vyoo bora, uwepo wa baadhi ya miundombinu isiyo rafiki na kukosekana kwa maji safi na salama shuleni kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Bureta alielezea changamoto nyingine ambazo zimekuwa kikwazo katika kuboresha miundombinu na mazingira ya shule kuwa ni pamoja na jamii kutoshiriki kikamilifu katika kuchangia ujenzi wa miundombinu ya vyoo na maji. Aidha, aliendelea kusisitiza kuwa changomoto hizi zimeleta athari kwa wanafunzi ikiwemo watoto wa kike kushindwa kuhudhuria darasani ipasavyo na kusababisha kushindwa kumudu na kutimiza malengo yao ya kielimu na wanafunzi kupoteza hadhi ya utu kutokana na ukosefu wa vyoo.

“Ili kuharakisha utatuzi wa changamoto  hizi, ni lazima kila mdau kujitoa kikamilifu ili kusaidia kuboresha shule zetu ziweze kufika katika viwango vinavyostahili kwani naamini uboreshaji wa mazingira ya shule utaleta hamasa kubwa kwa wanafunzi, walimu na jumuiya yote ya shule na hatimaye kuinua kiwango cha elimu nchini” alisisitiza Kaimu Kamishna wa Elimu.

Aidha, amewashukuru wadau wote wa program ya Maji, Afya na usafi wa Mazingira shuleni kwa ufadhili wao mkubwa katika kuboresha miundombinu ya vyoo shuleni ambapo jumla ya shule 2490 ziliweza kujengewa vyoo bora pamoja na kuwapatia maji safi na salama. Aliwataja wadau hao kuwa ni pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uingereza (DFID), Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) na Water Aid ambao wamewezesha kujengwa kwa miundombinu hiyo katika baadhi ya shule nchini.

Naye Mratibu wa Program ya Maji, Afya na usafi wa Mazingira shuleni kutoka Wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia Theresia Kuiwite amesema Program hiyo ilianzishwa baada ya utafiti uliofanyika mwaka 2009 katika mikoa kumi na mbili ambapo matokeo yalionyesha kati ya shule 2997 ni asilimia kumi na moja tu ya shule zilikuwa na vyoo vilivyofikia viwango vinavyohitajika na asilimia sitini na tisa za shule hazikuwa na huduma ya maji. Aidha, shule zote hazikuwa na miundombinu vya vyoo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum.

Kuiwite anasema program hii imewezesha kuwekwa kwa mikakati ya kuboresha miundombinu hiyo. Mikakati hiyo ndo ilipelekea kuwepo kwa umuhimu wa kuwa na Mwongozo wa Kitaifa wa namna gani miundombinu ya vyoo inapaswa kuwa.

“Leo hii tunazindua Mwongozo wa Kitaifa wa huduma ya maji, Afya na usafi wa mazingira shuleni ili kuwezesha shule zote nchini kuwa na miundombinu iliyo bora na salama kwa ajili ya watoto wetu na kuwawezesha kuwa na mazingira bora kwa ajili ya kufundishia na kujifunza”  alisema mratibu huyo.

Kuiwite anasema toka kuanza rasmi kwa program mwaka 2011 mpaka sasa shule 2500 zimeweze kujengewa na kuboreshewa miundombinu bora ya vyoo, yenye vyumba vya watoto wenye mahitaji maalum, na vyumba vya kujihifadhi vya watoto wa Kike wanapokuwa katika siku za hedhi. 

Program hii unaendeshwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Wizara ya Maji na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee ambao ni watekelezaji wakuu wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira.












Alhamisi, 6 Aprili 2017

DKT AKWILAPO KATIBU MKUU MPYA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli leo amemuapisha Dkt Leonard Akwilapo kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia baada ya aliyekuwepo Maimuna Tarishi kuhamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu. Kufuatia uteuzi huo nafasi yake aliyokuwa akiishika katika Wizara hiyo kama Naibu Katibu Mkuu  imechukuliwa na Dkt Ave Maria Semakafu ambaye alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya  na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)

Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara hiyo mara baada ya kuapishwa Dkt Akwilapo amewataka wafanyakazi  kufanya  kazi  kwa bidii na weledi mkubwa ili kufikisha malengo ambayo tumejiwekea ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto za watanzania walio  wengi. Alisema Wizara ya Elimu ni Kubwa, nzito na ina mambo mengi pamoja na changamoto zake tutumie mbinu  tulizo nazo kuhakikisha tunatatua changamoto hizo bila matatizo.

 “ katika kutatua changamoto mara nyingi hapakosi kuleta kusigana hivyo tuvumiliane tufanye kazi kwa pamoja ili tuweze kutimiza malengo makubwa ya Wizara” alisisitiza Dkt Akwilapo

Dkt Akwilapo amesema anaamini katika Wizara ya Elimu ana azina ya kutosha kwa kuwa amekulia katika Wizara hiyo hivyo anaifahamu vizuri na anaamini uzoefu alionao utasaidia kutatua changamoto zilizopo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Ave Maria Semakafua amesema wafanyakazi wote tuwe na lengo moja la kusonga mbele katika kufanya kazi  na kutatua changamoto kwa pamoja kwani wizara ya Elimu  ni kubwa na changamoto zake  ni kubwa pia.  Amesema changamoto hizo zinaanzia katika makuzi na malezi, ili kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa sisi kama walezi  tuhakikishe tunafuatilia kwa ukaribu. Amesema yeye ni mwanaharakati amekuwa akipigania haki za watoto wa kike kuhakiksha wanapata elimu lakini sasa suala la elimu kwa watoto wote linatakiwa  kupiganiwa kwani wapo watoto wa kiume wanaopata changamoto zinazo haribu maisha yao na kukatiza masomo yao.


Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi Bwana Nicholaus Moshi kiongozi wa Chama cha Walimu tawi la Wizara ya Elimu amesema tunawapongeza kwa nafasi walioshika kwani wameteuliwa kati ya watanzania wengi kuweza kuongoza Wizara hiyo na kwamba  tunaahidi kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kutimiza malengo ya watanzania walio wengi kwenye elimu ya watoto wao.