Jumatano, 29 Aprili 2015JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
MAADHIMISHO YA WIKI YA ELIMU MWAKA 2015

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inawatangazia wabunifu wote wa namna ya kutoa elimu kwa njia mbalimbali kuwasilisha andiko la ubunifu wao, ili waweze kushiriki katika maonesho yatakayokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Elimu itakayoanza tarehe 11- 15 Mei 2015 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Andiko la ubunifu liwe limewasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo, 7 Mtaa wa Magogoni, 11479 DAR ES SALAAM siku ya Jumamosi tarehe 02/05/2015.Elimu Msingi ni Haki ya Kila Mtoto kwa Maendeleo ya Taifa


IMETOLEWA NA:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
MAADHIMISHO YA WIKI YA ELIMU MWAKA 2015

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inawatangazia wadau wa Elimu na wananchi wote kwa ujumla kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Elimu kwa mwaka 2015 yatafanyika kuanzia mwezi April 2015 hadi Mei 2015.
Maadhimisho haya yatafanyika kwa mara ya Pili kitaifa mwaka huu 2015.

Maadhimisho ya Wiki ya Elimu yataanzia katika  ngazi za Halmashauri, Mikoa na baadaye kuhitimishwa kitaifa. Uzinduzi wa maadhimisho hayo kitaifa utafanyika tarehe 11/05/2015 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ambapo mgeni Rasmi atakuwa ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda. Kilele cha Maadhimisho kitafanyika tarehe 15/05/2015 katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma ambapo mgeni Rasmi atakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye pamoja na kuongea na wananchi atatoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi, shule, mikoa na Halmashauri zilizofanya vizuri na zilizoongeza ufaulu kwa kiasi cha Juu katika Mitihani   ya Taifa Darasa la Saba na Kidato cha Nne mwaka 2014.

Maadhimisho ya kitaifa yataenda sambamba na maonesho ya wadau mbalimbali wa elimu yatakayofanyika katika uwanja wa Jamhuri Mkoani Dodoma kuanzia tarehe 11-15/05/2015.
Ili kufanikisha maonesho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inakaribisha wadau wote wa Elimu na Mafunzo kushiriki katika Maadhimisho hayo katika ngazi za Halmashauri, Mikoa na Taifa.

.
Elimu Msingi ni Haki ya Kila Mtoto kwa Maendeleo ya Taifa


IMETOLEWA NA:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
7 Mtaa wa Magogoni,
11479  DAR ES SALAAM.
Tovuti: www.moe.go.tz
19/04/2015

Jumatatu, 20 Aprili 2015

WALIMU ZAIDI YA 4000 WAPATIWA MAFUNZO YA KUKUZA STADI ZA KKKWalimu zaidi ya 4000 wa shule za msingi nchini wamepatiwa mafunzo ya kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) unaolenga kuhakikisha walimu wote wanaofundisha darasa la I na II wanakuwa mahiri katika ufundishaji wa Stadi za KKK

Akizungumzia mafunzo hayo wakati wa ufunguzi Mhe. Kassim Majaliwa Kassim (MB) Naibu Waziri (Elimu), Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI alisema Serikali imefanya juhudi za makusudi kuendesha mafunzo haya ili kuhakikisha inawajengea uwezo walimu ili waweze kuwasaidia wanafunzi kumudu kikamilifu stadi za KKK.

Alisema ni vema wale wanaosimamia kuratibu walimu kuja kwenye mafunzo kuhakikisha wanaokuja ni wale ambao kweli wanahusika na kufundisha darasa la I na II, na kwamba ufuatiliaji ufanyike kuona kuwa walimu wa madarasa yaliyolengwa ndio wanakuja kwenye mafunzo hayo.

Mhe. Majaliwa amewataka walimu waliochaguliwa kushiriki mafunzo haya kutumia fursa hii vizuri na kuwa chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika ufundishaji wa Stadi za KKK. ‘’Napenda kuwakumbusha kuwa mmechaguliwa miongoni mwa walimu walio wengi kushiriki mafunzo haya hivyo, itumieni fursa mliyoipata vizuri na hata mkirejea katika vituo vyenu vya kazi mkaache mtindo wa kufanya kazi kwa mazoea bali kujituma na kutanguliza uzalendo” Alisema Naibu Waziri Majaliwa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Kituo cha Mafunzo ya Mtaala Bibi Fika Mwakabungu alisema Mafunzo ya Kukuza Stadi za Kusoma Kuandika na Kuhesabu ni endelevu na yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na yanalenga kuwafikia walimu 18,000 kutoka mikoa 14 ya Tanzania Bara.

Akiitaja Mikoa itakayohusika ni pamoja na Arusha, Dar Es Salaam, Morogoro, Pwani, Rukwa, Ruvuma,Tanga,Singida, Kilimanjaro, Manyara, Kagera, Katavi, Geita na Mwanza.

Kwa upande mwingine Mhe. Majaliwa alisema Serikali imeanzisha chombo kimoja maalumu kitakachosimamia stahili za Walimu na kurahisisha usimamizi wa upandishaji wa madaraja sambamba na kurekebisha mishahara ikiwa ni hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili walimu.

Pia alisema Serikali imeridhia na kutoa muundo mpya wa kada za walimu ambao utawawezesha walimu waliokuwa wamefikia ukomo katika muundo wa zamani kunufaika na muundo mpya katika bajeti ya Mwaka 2015/16.