Alhamisi, 2 Julai 2020

NDALICHAKO ATIMIZA AHADI ATOA VYEREHANI 10 VETA MPANDA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja  na wanafunzi wa VETA Mpanda wanaotoka katika mazingira magumu mara baada ya kuwakabidhi cherehani alizoahidi kuwapatia

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ametimiza ahadi ya kutoa vyerehani 10 kwa wanafunzi waliohitimu​ mafunzo ya ushonaji kutoka Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi​ Mpanda​ wanaotoka katika mazingira magumu.
Akizungumza katika halfa hiyo Mkoani Katavi, Profesa Ndalichako amesema ahadi hiyo aliitoa​ mwaka 2018 baada ya kuwakuta vijana wadogo wamemaliza masomo ya darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari​ na kujiunga na mafunzo ya ushonaji katika chuo hicho kupitia msaada wa kanisa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja  na wanafunzi wadogo wa VETA Mpanda wanaotoka katika mazingira magumu mara baada ya kuwakabidhi cherehani alizoahidi kuwapatia

“Mwaka juzi nilifika katika chuo hiki na kuwakuta hawa vijana wawili wadogo wakiwa katika mafunzo ya ushonaji na nilipozungumza nao niligundua kuwa wametoka katika mazingira magumu, hivyo kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari, ndipo nilipowaahidi kuwapatia vyerehani watakapomaliza ili viwawezeshe kujiajiri.​ Hata hivyo, nimetoa vyerehani 10 ili na wengine wenye mazingira ya namna hiyo waweze kupata,” amesema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikabidhi fedha taslimu kiasi cha Sh. 500,000 kwa mmoja wa wanafunzi wa VETA Mpanda aliowapati cherehani  kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuwawezesha kuanza kushona ili waweze kujiingizia kipato.
Aidha, Waziri huyo amemuagiza Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Mpanda kuona namna ya kuwapatia nafasi ya kuendelea na ngazi nyingine ya mafunzo watoto hao​ ili kuwawezesha kuwa mahiri katika ushonaji na kuhakikisha anawasimamia na kuwashauri popote watakapokuwa wanafanya shughuli zao.
Mkuu wa Chuo cha Ufundi Mpanda Elisha amemshukuru waziri kwa kutimiza ahadi aliyoitoa mwaka 2018 kwani inakwenda kuinua watoto wanaotoka katika familia masikini, na kuahidi kuendelea kuwasimamia ili cherehani hizo ziwe na manufaa kwa watoto wenyewe na familia zao.
Mhitimu wa mafunzo ya Ushonaji kutoka VETA Mpanda Gift Giles (miaka 16) kutoka katika mazingira magumu akionesha chereheni aliyokabidhiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
Mmoja wa wanafunzi waliopatiwa cherehani Gift Giles amemshukuru Waziri kwa kuwapatia cherehani hizo ambazo zinakwenda kubadili maisha yao kwani zitawawezesha kupata fedha ambazo zitawasaidia kujiendeleza katika masomo
Naye mmoja wa walezi wa wanafunzi hao Bibi Flora Cosmas amemshukuru Mhe. Ndalichako na kuahidi kuwasimamia ili waweze kutumia machine hizo vizuri ikiwa ni pamoja na kuwaendeleza zaidi kiujuzi.
Thabitha Venance mwenye umri wa miaka 14 aliyemaliza mafunzo ya ushonaji katika chuo cha ugundi VETA Mpanda na  anayetoka katika mazingirs magumu akiwa na cherehani aliyojabidhiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
"Sisi walezi wa vijana hawa tunamahukuru sana Mhe. Waziri​ kwa kuguswa kwake kuamua kwa moyo wake kufanya jambo hili kubwa maana anakwenda badili naisha ya vijana hawa ambao hawakuwa na uwezo wa kununua hizi cherehani" amesema bi Cosmas.

Jumatano, 1 Julai 2020

WAZIRI NDALICHAKO AKAGUA MIRADI YA ELIMU HALMASHAURI YA KASULU MKOANI KIGOMA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amekagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri ya Kasulu mkoani Kigoma yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 12.

Miradi hiyo ni pamoja na  ujenzi wa Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kasulu, Chuo cha Ualimu Kabanga na jengo la Utawala la shule ya Sekondari Grand.

Akizungumzia maendeleo​ ya ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga mara baada ya kukagua, Waziri Ndalichako amesema chuo hicho kinajengewa upya miundombinu yote​ baada ya ile ya awali kuchakaa sana na kushindwa kukarabatiwa.
Msimamizi wa Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga, Luteni Kanali Onesmo Njau akimweleza jambo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipofanya ziara ya kukagua mradi huo mkoani Kigoma
Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu ya​ chuo  hicho unagharimu zaidi ya bilioni 10, na kuwa utakapokamilika utabadili taswira ya mji huo kwa kuwa majengo yanayojengwa ni ya kisasa na imara ambayo yatadumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa jengo jipya la utawala na utengenezaji wa mfumo wa maji katika shule ya sekondari ya Grand, Profesa Ndalichako amesema umegharimu zaidi ya Shilingi milioni 534 na kwamba utakapokamilika utaongeza morali ya walimu​ kufundisha na kusaidia wanafunzi waliopo katika shule hiyo.
Mradi mwingine uliotembelewa na Waziri wa Elimu ni ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha wilaya ya Kasulu ambao upo katika hatua za mwisho ambao umegharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.97. Jumla ya majengo 15 yatajengwa​ na kitachukua wanafunzi 320 watakaokuwa wakilala chuoni hapo.
Mhandisi Faraja Magania kutoka Chuo cha Ufundi Arusha akifafanua jambo wakati Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alipofanya ziara ya kukagua Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Kasulu.
Waziri Ndalicahko amewataka wananchi wa wilaya ya Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kutumia fursa ya kuwepo kwa vyuo mbalimbali katika Halmashauri hiyo kujipatia maarifa na ujuzi utakaowawezesha kuajiriwa ama kujiajiri ili kujiletea maendeleo binafsi na ya mkoa wa Kigoma.


Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia​ kwa namna ilivyojikita katika kupanua wigo wa elimu. Amesema kuwa katika wilaya yake kuna maeneo ambayo ni ya wafugaji na watoto hawakuwa wakienda shule lakini kwa sasa zimejengwa shule shikizi katika maeneo hayo ya mbali hivyo kuwezesha watoto kusoma na kuleta matokeo chanya.
Kanali Anange amesema baada ya Serikali kutekeleza Sera ya Elimu bila ada kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi, hivyo kupelekea Serikali kupanua​ miundombinu katika ngazi zote za elimu ili kuwezesha fursa za masomo kwa wanafunzi ikiwemo na kuongeza walimu.​
Muonekano wa hatua ya ujenzi wa moja ya jengo la Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Kasulu kilichopo Halmashauri ya Kasulu, Kigoma

Aliongeza kuwa  ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu itawezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu katika mazingira bora.
Naye Mratibu wa Mradi wa Uendelezaji wa Elimu ya Ualimu (TESP), Ignas Chonya amesema ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Kabanga awamu ya kwanza unatarajiwa kukamilika Oktoba 2020 na chuo kitakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 400 kwa wakati mmoja na kwamba chuo kinatarajiwa kuanza mafunzo mwaka huu.

Alhamisi, 18 Juni 2020

SERIKALI KUTUMIA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 700 KUWAENDELEZA WABUNIFU

Serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni 750 kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kuwaendeleza wabunifu 70 walioshiriki katika fainali za Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU) 2020.


Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akitangaza Washindi wa MAKISATU 2020 ambapo amesema Serikali imepanga kuendeleza ubunifu unaozalishwa ili kuwa bidhaa na kuchangia katika harakati za kukuza uchumi.


Waziri Ndalichako amefafanua kuwa MAKISATU ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuibua, kutambua na kuendeleza ubunifu na ugunduzi unaofanywa na watanzania hususani wa ngazi za chini.


Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwashukuru wadhamini wa MAKISATU 2020 ambao wamekuwa sehemu ya kuendeleza Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambao ni benki ya CRDB, VODACOM Foundation, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Binadamu (HDIF)Jumatano, 17 Juni 2020

NDALICHAKO ATANGAZA MIHULA NA TAREHE ZA KUANZA MITIHANI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Juni 17, 2020 ametangaza tarehe za kuanza kwa mitihani ya Taifa ya Darasa la Saba, Kidato cha Nne na Upimaji wa kitaifa wa Darasa la Nne na Kidato cha Pili.

Akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dodoma, Prof. Ndalichako amesema Darasa la Saba watafanya Mtihani kuanzia tarehe 7 - 8 Oktoba, 2020 wakati Kidato cha Pili wataanza mitihani Novemba 9 - 20, 2020. Darasa la Nne watafanya Novemba 25 - 26, 2020 wakati Kidato cha Nne watafanya kuanzia Novemba  23 hadi Disemba 11, 2020.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani) Jijini Dodoma wakati akitangaza mihula na tarehe za kuanza mitihani ya Taifa kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Profesa Ndalichako amezungumzia mihula mipya ya shule ambapo amesema shule za msingi na sekondari watamaliza muhula wa kwanza wa masomo Agosti 28, 2020 na kuanza muhula wa pili utakaoishia Disemba 18, 2020. Amesema kuwa ili kukamilisha muhtasari wa masomo, shule zitalazimika kuongeza saa 2 za masomo kwa kila siku ili kufidia muda uliopotea huku akisisitiza kuwa maelekezo ya kuongeza muda hayatahusu madarasa ya awali.

Aidha, Profesa Ndalichako ametoa ufafanuzi kuhusu mihula kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano ambapo amesema wanafunzi hao wataanza masomo Juni 29, 2020 kama ilivyoagizwa na kukamilisha muhtasari wa masomo yao na kufanya mitihani yao ya kumaliza Kidato cha Tano ifikapo Julai 24, 2020. Wanafunzi hawa wataanza rasmi masomo ya Kidato cha Sita Julai 27, 2020.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (katikati) akiongea na Waandishi wa habari (hawapo pichani) Jijini Dodoma wakati akitangaza mihula na tarehe za kuanza mitihani ya Taifa kwa shule za msingi na sekondari nchini. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu, Profesa James Mdoe na kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ave Maria Semakafu.

Waziri Ndalichako ameagiza Uongozi wa shule zote kuhakikisha wanafunzi, walimu na wafanyakazi wengine wote wanazingatia maelekezo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kama yalivyotolewa katika Mwongozo wa Wizara ya Afya ikiwemo kuhakikisha kuwa shule zote zinanunua vifaa vya kutosha kwa ajili ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.