Jumamosi, 14 Machi 2020

ZIARA YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII

ZIARA YA KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMIIEO


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Peter Serukamba ametoa rai kwa Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kutangaza programu na huduma ziazotolewa Chuoni hapo ili wananchi wanufaike na huduma hizo.

 Serukamba ametoa rai hiyo Jijini Arusha wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea chuo cha Ufundi Arusha  kukagua miradi ya elimu inayotekelezwa chuoni hapo.

 "Nimefurahishwa na ubora wa huduma na wanafunzi wa chuo hiki sasa wakati umefika kwa chuo kujitangaza ili kupata masoko ya bidhaa zinazozalishwa lakini pia kuongeza wanafunzi wengi zaidi kujiunga na kozi zinazofundishwa hapa" amesema Serukamba.

Pia amekitaka Chuo hicho kuanzisha Kampuni itakayosimamia na kufanya kazi mbalimbali kibiashara katika maeneo waliyobobea ikiwemo uhandisi ujenzi, ufundi wa magari, umeme na maeneo mengine, hatua ambayo itasaidia kukuza mapato ya ndani ya Chuo ambayo yatakiwezesha kutekeleza miradi mingine ya kimkakati.

 Mheshimiwa Serukamba amesema Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa Miradi ya Serikali ambayo Chuo cha ATC kinasimamia na kukitaka chuo hicho  kupanua wigo wa wateja kwa kutafuta miradi toka sekta Binafsi ili kuondoa utegemezi wa Miradi ya Serikali pekee.

Aidha, Mheshimiwa Serukamba ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa uwekezaji mkubwa  uliofanyika wa miundo mbinu ya kufundishia katika chuo hicho ikiwa ni pamoja na kukipatia kazi za usimamizi  wa Miradi ya Ujenzi katika Vyuo  vya Ufundi na Ualimu.

Pia amekipongeza Chuo cha Ufundi Arusha kwa kuendesha programmu ya Mafunzo ya muda mfupi ya ufundi ujenzi ambayo mpaka sasa  takriban wanafunzi 305 wamehitimu mafunzo hayo, huku  akiishauri Wizara ya Elimu, kushirikiniana na Chuo hicho kuhakikisha wahitimu hao wanapata nafasi ya kufanya kazi katika miradi ya ujenzi inayoendelea.
 

Nae Mbunge wa Biharamulo Magharibi na Mjumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma  na Maendeleo ya Jamii Oscar Mukasa amesema kwa mara ya kwanza ameona chuo kimesimama  katika dhamira yake, na hivyo kupongeza hatua ya Chuo cha ATC  kujikita katika kutoa mafunzo kwa ubora ambayo ndio msingi wa kuanzishwa  kwake, akiongeza kuwa  vipo  vyuo ambavyo vilianzishwa kwa malengo fulani lakini kwa sasa  vinatekeleza malengo mengine.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye elimu ya Ufundi  kwa kuimarisha vyuo vya ufundi wa kati na ufundi stadi kwani ndiko wataalamu wanapopatikana wa kufanya kazi kwenye viwanda na ndio maana serikali imewekeza takriban  sh bilioni 16 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na mitambo ya  karakana zote za chuo hicho. 

“Tangu serikali ya Awamu ya Tano imeingia  madarakani viwanda 800 vimeanziswa, hii maana yake ni kwamba tunahitaji kuzalisha vijana wengi wenye ujuzi wa kufanya kazi katika viwanda hivyo," amesema Profesa Ndalichako

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Ufundi Arusha Prof. Siza Tumbo amesema katika uongozi wake atahakikisha chuo hicho kinajitangaza kwa kupitia njia anuahi za mawasiliano  ili huduma zinazotolewa chuoni hapo  ziwafikie watanzania wengi zaidi, ikiwa ni pamoja na kuwa na mkakati wa kuongeza idadi ya wasichana kujiunga na chuo hicho.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha Dkt Musa Chacha amesema kwa sasa Chuo kina mipango mingi ikiwa ni pamoja na kujenga bweni la wasichana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 500, kuongeza mapato ya ndani kutumia kazi zinazofanyika, kuendeleza kituo cha mafunzo ya nishati jadidifu cha Kikuletwa na kituo cha mafunzo ya kilimo na umwagiliaji cha Oljoro pamoja na ukarabati wa miundombinu ya Chuo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya  Jamii iko Mkoani Arusha katika ziara ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.


Ijumaa, 6 Machi 2020

MAKTABA MPYA YAZINDULIWA CHUO CHA UALIMU KOROGWE

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa  Machi 5, 2020 amezindua maktaba mpya ya  Chuo cha Ualimu Korogwe kilichopo Mkoani Tanga.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akikata Utepe kuashiria uzinduzi wa Maktaba mpya ya Chuo cha Ualimu Korogwe, Tanga kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mh Martin Shigela, Mbunge wa Korogwe Mjini Mhe. Mary Chatanda na Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo
 Akizungumza na baadhi ya walimu tarajali na wanafunzi aliowakuta katika maktaba hiyo mara baada ya kuizindua Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao kuitumia vyema maktaba hiyo kwa lengo la kujipatia maarifa na kuongeza uwezo katika taaluma.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa akipata maelezo toka kwa mtaalamu wa Tehama wa Chuo cha Ualimu Korogwe baada ya kuzindua Makataba ya Chuo hicho
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi  na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akimkaribisha Waziri Mkuu amesema
Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 338 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maktaba hiyo ambayo ujenzi wake ukianza kwa Micjango ya Wananchi wa Korogwe.

Katibu Mkuu huyo amesema Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kutoa kiasi hicho cha fedha ili kuunga mkono juhudi za wananchi ambao walichanga shilingi milioni 1.9 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.
Chumba cha kompyuta katika Maktaba mpya ya Chuo cha Ualimu Korogwe
"Wananchi wa Korogwe waliona umuhimu wa chuo hiki kuwa na maktaba na wakaanza kuchanga fedha na kuanza ujenzi" amesema  Dkt. Akwilapo.

Mmoja wa walimu tarajali  katika Chuo cha Ualimu Korogwe Emanuela Bombo ameishukuru Serikali kwa kuwekeza kwenye ujenzi wa maktaba hiyo kwani itasaidia katika ujifunzaji.
Muonekano wa moja ya  Eneo la kujisomea katika Maktaba mpya ya Chuo cha Ualimu Korogwe
Maktaba hiyo ina vifaa vya kisasa pamoja zikiwemo kompyuta ambazo zinawezesha matumizi  maktaba mtandao na kwamba Maktana itatumiwa na walimu tarajali zaidi ya 1000 ambao wanasoma masomo ya Sayansi, Hisabati na TEHAMA na pia wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari wa wilaya ya Korogwe.


PUBLIC NOTES