Jumanne, 6 Oktoba 2015

WATAALAM WA ELIMU KUTOKA SWEDEN WAFANYA ZIARA YA KIKAZI NCHINI

 
Wataalam wa Elimu kutoka Sweden ambao ni Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Juu nchini humo wameanza ziara ya kikazi nchini  kwa lengo la kujifunza mfumo wa elimu katika ngazi zote, mipango ya maendeleo pamoja na mageuzi mbalimbali ya Elimu.
 
Wataalam hao ni Wakaguzi wawili toka Kitengo cha Elimu ya Juu (Cecilia George na Petra Nord); Wakaguzi wawili kutoka Kitengo cha Elimu ya Sekondari (Eva Neihoff na Isabelle Nilsson); na Mkaguzi mmoja toka katika Kitengo cha Elimu ya Ufundi (Stefan Lofkvist).
 
Ujumbe huo umekutana na kufanya mazungumzo na watumishi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakiongozwa na Kamishna wa  Elimu nchini Prof. Eustella Bhalalusesa aliyemwakilisha Katibu Mkuu. Mazungumzo yao yalijikita zaidi katika kubadilishana uzoefu kuhusu mifumo ya elimu inayotumika katika nchi hizo mbili.
 
Aidha, wataalam hao katika ziara yao iliyoanza tarehe 5 hadi 7 Oktoba, 2015  wanatembelea taasisi zilizo chini ya Wizara zikiwemo; Taasisi ya Elimu Tanzania, Baraza la Mitihani, Tume ya Vyuo Vikuu, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi.  Pia watatembelea shule mbili za sekondari zenye kidato cha tano na cha sita kwa lengo la kuanzisha uhusiano wa kirafiki na shule kama hizo nchini Sweden.

Alhamisi, 1 Oktoba 2015

MAMLAKA YA ELIMU TANZANIA YATOA MKOPO WA SHILINGI BILIONI 3 KWA TAASISI YA ELIMU TANZANIA


 Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imeingia makubaliano na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ya Mkopo wa Shilingi Bilioni tatu. Mkopo huu umetolewa na TEA ili kuiwezesha Taasisi ya Elimu Tanzania Kufanya utafiti wa kubaini mahitaji ya maboresho kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu, Kuandaa mitaala na  mihtasari ya masomo ya Elimu ya Msingi na Kuandika vitabu vya kiada kwa Darasa la III hadi la VI ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014.

Mkataba huo umetiwa saini tarehe 30 Septemba, 2015 na Joel Laurent Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TEA na Dkt. Leonard Akwilapo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TET na kushuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Prof. Sifuni Mchome ambapo Mkopo  huo ni nafuu unatarajiwa kulipwa katika kipindi cha  miaka 6.
Matokeo tarajiwa kutokana na Mkopo huo ni Pamoja na uwepo wa Mitaala inayoendana na wakati na inayokidhi mahitaji ya sekta na shirikishi, uwepo wa mihutasari ya masomo itakayosambazwa katika kila shule kama ilivyoainishwa katika mitaala na uwepo wa vitabu vya kiada kulingana na mtaala ili kuepusha kuwa na vitabu vinavyotofautiana.


Aidha, ufadhili huu unalenga kuiongezea Taasisi ya Elimu Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa njia yenye tija na kuongeza mapato ya Taasisi na utakuwa ni chachu ya kuboresha mfumo wa upatikanji wa vitabu sahihi kulingana na mitaala nchi nzima kupitia TIE.

MKUTANO WA KUTATHMINI SEKTA YA ELIMU NCHINI WAFANYIKA


Mkutano wa kutathmini Sekta ya Elimu nchini kwa mwaka 2015 umefanyika jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuanzia tarehe 28 hadi 30 Septemba, 2015 ambapo Wadau mbalimbali wa Elimu ikiwa ni pamoja na Serikali, Washirika wa Maendeleo na Taasisi Zisizokuwa za Serikali zinazojihusisha na Elimu walikutana na kujadiliana kuhusu mafanikio, changamoto na mikakati ya kuboresha elimu nchini.

 Mkutano huo ambao ulifanyika sambamba na Maonesho ya Matumizi ya TEHAMA katika Elimu ya Msingi ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome ambae aliwataka washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Elimu nchini.

Mkutano huo umefungwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anaeshughulikia Elimu Mhe. Kassimu Majaliwa ambae alisema ushirikiano ulioko kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo unasaidia kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika kuimarisha mahudhurio ya shule, kugharamia Elimu  Msingi  kwa wanafunzi wote, kupatikana kwa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika Elimu Msingi.