Ijumaa, 4 Desemba 2015



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
 
Coat of arms of Tanzania.png

KATAZO LA KUONGEZA ADA KWA SHULE ZISIZO ZA SERIKALI KWA MWAKA WA MASOMO 2016
 
Waraka wa Elimu Na. 4 wa Mwaka 2008 uliweka viwango vya ada vinavyotozwa katika shule za Msingi na Sekondari za Serikali na zile zisizo za serikali. Ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za serikali ni Tsh. 150,000/= na shule za bweni Tsh. 380,000/= kwa mwaka kwa kila mwanafunzi. Aidha waraka huo ulielekeza kwamba ongezeko lolote la ada lazima lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza kutumika.  
Hata hivyo imegundulika kuna baadhi ya shule zisizo za serikali zimekuwa zikiongeza ada kila mwaka pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu. Utamaduni huu wa kuongeza ada kila ifikapo mwishoni mwa mwaka umekuwa ukisababisha usumbufu mkubwa kwa wazazi/walezi na hata baadhi yao kushindwa kuendelea kusomesha vijana wao katika baadhi ya shule.
Kwa tangazo hili wamiliki wote wa shule zisizo za serikali wanaagizwa kufanya yafuatayo:
1.      Kutokuongeza gharama za uendeshaji wa shule zikiwemo ada kwa mwaka wa masomo unaoanzia mwezi Januari mwaka 2016 mpaka watakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu; wale ambao tayari wameongeza gharama na ada kwa mwaka wa masomo wa 2016 bila kibali cha Kamishna wa Elimu, Wizara haitambui ongezeko hilo kwa kuwa ni batili na hivyo zimefutwa.
2.      Ada zote kwa shule zisizo za serikali zitabaki kama zilivyokuwa zimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu.
3.      Kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Shule aliyepo Idara ya Ithibati ya Shule inayoeleza kiasi cha ada na gharama  kinachotozwa kwa sasa (kabla ya mwaka wa masomo 2016) na tarehe shule ilipopata kibali kutoka kwa Kamishna wa Elimu kutoza kiwango hicho cha ada.  Taarifa hiyo ifike ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe ya tangazo hili.
Wathibiti ubora wa shule waliopo sehemu mbalimbali nchini wanaagizwa kulifuatilia suala hili kwa karibu ili kila shule itekeleze agizo hili na kutoa taarifa zilizoelekezwa katika tangazo hili. Hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wamiliki ambao hawatatekeleza maagizo haya.  
Aidha Wizara iko katika hatua za mwisho za utafiti na kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimumsingi (elimu ya awali, msingi na sekondari) na hivyo wadau mbalimbali watoe ushirikiano kwa timu za wataalamu wanaofanya kazi hii ili kusaidia katika kuukamilisha mfumo na hatimaye kuwa na ada elekezi katika maeneo mbalimbali.
 
     
IMETOLEWA NA KATIBU MKUU