Jumapili, 31 Machi 2019

WIZARA YA ELIMU KUJENGA MAABARA YA FIZIKIA KATIKA SHULE MAALUM YA WASICHANA KISARAWE


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  kujenga maabara ya Fizikia  katika shule mpya maalum ya wasichana inayotarajiwa kujengwa katika wilaya ya Kisarawe.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uchangiaji fedha kwa ajili ya kujenga shule hiyo ambapo Waziri Ndalichako amesema pamoja na kujenga Maabara pia itatoa vifaa vyote vya maabara hiyo lengo likiwa kuhamasisha na kuongeza fursa za watoto wa kike kisarawe na kwingine nchini kusoma masomo ya sayansi.

Akizungumzia hafla ya kuchangia fedha kwa ajili ya kujenga shule hiyo maalum Waziri Ndalichako ameipongeza wilaya ya Kisarawe kwa kuja na kampeni ya Tokomeza Zero yenye lengo la kuboresha elimu katika wilaya hiyo huku mkazo ukiwekwa katika  kumuondolea mtoto wa kike changamoto anazokabiliana nazo wakati wa kujifunza kwa kuhakikisha anapata mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizungumza na wadau mbalimbali wa elimu (hawapo pichani) walioitikiwa wito wa kuchangia ujenzi wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe“Mtoto wa kike anapokuwa anatembea umbali mrefu kutoka shuleni kwenda nyumbani njiani anakutana na majaribu na vishawishi vingi vinavyokwamisha lengo lake la kupata elimu, kwa hiyo kuamua kujenga shule maalum kwa ajili ya mtoto wa kike ni uamuzi mzuri kwani  itawapa fursa kuweza kukaa na kusoma vizuri zaidi na hii ni hatua kubwa sana katika kuunga mkono Jitihada zinazofanywa na Rais wetu” Amesema Ndalichako.

Ndalichako amesemea  tathimini inaonyesha ufaulu kwa ujumla kwa mtoto wa kike uko chini ukilinganisha na watoto wa kiume kwa hiyo ujio wa shule hii maalum kwa ajili ya mtoto wa kike ni muhimu kutokana na mazingira wanayoishi ambapo wanaporudi kutoka shule wanakuwa na majukumu mengi ya nyumbani na kuwanyima muda wa kujisomea.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo amesema wilaya ya Kisarawe imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inapunguza ziro na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikikwamisha wanafunzi kujifunza hasa kwa mtoto wa kike.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Viti maalum wa Kisarawe Zainabu Vulu wakifatilia kwa makini zoezi la  wa kuchangia ujenzi wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe

“Wilaya ya Kisarawe imekuwa na utaratibu wa kufanya tathimini kila matokeo yanapotoka ili kuona nafasi ya wilaya katika ufaulu na kuziangalia changamoto ambazo zinakwamisha faulu na kuziwekea mikakati ili kuboresha mazingira ya kfundishia na kujifunza ” amesema Waziri Jafo.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo alimweleza Waziri wa Elimu kuwa lengo la kuanzishwa kwa Kampeni ya Tokomeza Zero ni kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule ili kuifanya kuwa rafiki na salama kwa utoaji wa elimu.

Mwegelo amesema ujenzi wa shule maalum katika wilaya ya kisarawe  ya uchangia ni moja ya mkakati mahsusi wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto wa kike ili kuwawezesha kupata muda wa ziada wa kujifunza zaidi.

Shule ya Sekondari maalum inayotarajiwa kujengwa katika wilaya Kisarawe itachukua wanafunzia wa kidato cha kwanza mpaka cha sita na inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu ambazo zinahusisha ujenzi wa miundombinu ya mabweni, madarasa, maabara, matundu ya vyoo pamoja na nyumba za walimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako na  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo kwa pamoja wakipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni kmi iliyolewa na kampuni ya star times kwa ajili ya ujenzi wa wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe

NDALICHAKO AZINDUA MAKTABA MTANDAO TAASISI YA ELIMU TANZANIA -TET


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amezindua Maktaba Mtandao ya Taasidi ya Elimu Tanzania (TET).

Akizindua Maktaba hiyo jijini Dar es salaam Waziri Ndalichako amesema itasaidia kupunguza changamoto iliyopo ya usambazaji wa vitabu kwani mara nyingi vimekuwa vikichelewa kufika katika shule kutokana na ugumu wa miundombinu ya usafirishaji na kuleta usumbufu katika mchakato wa ujifunzaji na ufundishaji.

Amesema Serikali imeiona changamoto hiyo na kuanzisha Maktaba Mtandao kama  moja ya njia ya kurahisisha upatikanaji wa machapisho ya Kiada, Ziada, Mitaala Mhtasari, Kiongozi cha Mwalimu, Miongozo mbalimbali na Moduli za Kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi walimu na watumiaji wengine.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizinduz Maktaba Mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania katika uzinduzi wa Maktaba hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam
“Kumekuwa na lawama katika suala la usambazaji wa vitabu kwani havifiki kwa wakati, kawaida mwanafunzi anapaswa kukuta vitabu shuleni lakini hali ilivyo sasa vitabu vinamkuta mwanafunzi shuleni hii si sawa, hivyo kuwepo kwa Maktaba Mtandao itasaidia katika kupatikana kwa vitabu mapema na kurahisisha mchakato wa kujifunza" amesisitiza Waziri Ndalichako.
Wakati huo huo Ndalichako ameiagiza Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) kuhakikisha inasimamia uandaaji wa machapisho ya mitaala, vitabu na machapisho mengine  ili yawe na ubora.
Ameeleza kuwa pamoja na Bodi hiyo kufanya kazi nzuri ya kusimamia na kuhakikisha vitabu vinavyochapishwa sasa vinakuwa na ubora lakini bado inapaswa kongeza umakini kwa sababu suala la uandaaji wa vitabu ni endelevu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia maonesho ya vitabu vinavyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania wakati wa uzinduzi wa  Maktaba Mtandao jijini Dar es Salaam

Ndalichako amesisitiza kuwa TET ni moyo wa Elimu nchini kwa kuwa ndio inaandaa mitaala, vitabu, miongozo ya shule za msingi na sekondari pamoja na machapisho mbalimbali ya Elimu, hivyo kukiwa na kasoro katika mchapisho hayo watoto wa Kitanzania watakuwa wamefundishwa vitu ambavyo si sahihi na serikali haitavumilia hilo.

Awali Mkurgenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt Aneth Komba alimweleza Waziri wa Elimu kuwa lengo la kuanzishwa maktaba mtandao hiyo kurahisisha usambazaji wa machapisho ya Taasisi hiyo katika shule za Serikali, Binafsi na kwa wadau wengine wa Elimu
Dkt Komba amesema  Maktaba Mtandao iliyozinduliwa inajumuisha vitabu mbalimbali vya kiada kuanzia ngazi ya Elimu ya awali, msingi na sekondari (kidato cha kwanza mpaka sita)  vinavyochapishwa na taasisi hiyo. Pia vitakuwepo vitabu vya  ziada kutoka Tanzania na Nchi nyingine.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akicheza na kufurahi na wanafunzi wa shule ya Fountain Gate wakati wa uzinduzi wa  Maktaba Mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania katika uzinduzi wa Maktaba hiy iliyofanyika jijini Dar es Salaam


Jumanne, 26 Machi 2019

HALMASHAURI ZATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUMOTISHA WALIMU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka mikakati ya kuwamotisha walimu wapya wanaoripoti kazini kwa kuwafikisha katika vituo vyao vya kazi ikiwa ni pamoja na kuwalipa maslahi yao yote.

Waziri Mkuu ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA) na kusisitiza kuwa hatua hiyo iende sambamba na kuendelea kuwatembelea walimu hao katika vituo vyao vya kazi kuwasikiliza, kushauriana na kupatia ufumbuzi changamoto walizo nazo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu wa  sita wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya (hawapo pichani) Jijini Dodoma.
Amesema walimu hao wanaporipoti wanakuwa ni wageni katika wilaya hizo hivyo kuwaelekeza tu kuripoti katika shule walizopangwa haitoshi ni vyema kuweka utaratibu wa kutumia magari ya Halmashauri kuwafikisha walimu hao katika vituo vyao vipya vya kazi.

“Ninyi Maafisa Elimu hakikisheni walimu hao wanaporipoti wanalipwa maslahi yao ya msingi, lakini pia hamasisheni Halmashauri zenu kuwamotisha walimu kwa kuwapa vianzilishi vya maisha kama ambavyo Wilaya nyingine zinafanya. Wilaya za Mkoa wa Njombe tangu mwaka 2013 zimekuwa zikitoa motisha kwa walimu wapya wanaoripoti kwa kuwapa kitanda, godoro, gunia la mahindi, viazi na maharage, hii inamfanya mwalimu kujisikia yuko nyumbani, muige mfano huu,” aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wakifuatilia Hotuba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita wa Umoja wa Maafisa Elimu hao uliofanyika jijini Dodoma.
Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa amewataka Maafisa Elimu hao kutumia mkutano huo kukumbushana wajibu wao katika kusimamia Elimu na kubadilishana uzoefu na mbinu mbalimbali za kusimamia elimu ili kuongeza ubora wa elimu hiyo.

“Mkutano huu umekuja kipindi muafaka kwa sababu matokeo ya upimaji wa Taifa wa ngazi mbalimbali yameshatoka, wote tunakumbuka upimaji umefanyika kwa mitihani ya darasa la nne, la saba, kidato cha nne na ile ya kidato cha sita, hii itoe fursa kwenu kujipima na kuona kama hatua mliyofikia ni nzuri na kama bado ni ya chini basi mbainishe changamoto zilizopelekea kuwa hivyo na kuweka mipango ya kuboresha,” alisema Mhe. Majaliwa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimkabidhi tuzo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kwa kusimamia vizuri Sekta ya Elimu. Tuzo hiyo imetolewa na Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA) kwa kutambua mchango wa Waziri huyo katika kusimamia ubora wa Elimu nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka Maafisa Elimu kusimamia Sera, Miongozo na Taratibu zinazosimamia utoaji wa elimu nchini huku akiwasihi maafisa hao kutoa taarifa zilizo sahihi kwani wakati mwingine taarifa zinazotolewa zinatofautiana na zile zinawasilishwa baada ya kufanyika kwa ukaguzi katika maeneo mnayoyasimamia.
   
“Wakati mwingine mnatoa taarifa zisizo sahihi, kwa sababu kaguzi ambazo  zimekuwa zikifanyika zinaonesha kuna baadhi ya maeneo ambayo bado kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kati ya 73 hadi 200 kwa upande wa sekondari na mazingira yanapokuwa katika hali hiyo si rahisi kutoa elimu bora, hivyo tutoe taarifa zilizo sahihi na taarifa hizi zikiwa sahihi itasaidia hata wakati wa uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza na kile cha tano,” aliongeza Waziri Ndalichako.

Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya Germana Mng’ao ameipongeza Serikali kwa kuboresha mazingira ya kufundishia  na kujifunzia na kuahidi kufanya kazi kwa bidii katika nafasi yao ya kusimamia Elimu Tanzania.


Kauli mbiu ya mkutano huo ni “ELIMU BORA ITATUFIKISHA KATIKA UCHUMI WA KATI IFIKAPO 2025.”
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akisalimiana na   Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita wa Umoja wa Maafisa Elimu hao uliofanyika jijini Dodoma.

Jumatatu, 25 Machi 2019

OLE NASHA: SERA YA KUWALINDA WABUNIFU YAJA


SERIKALI imesema iko katika hatua za mwisho kukamilisha Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambayo itatoa mwongozo wa namna ya utekelezaji wa masuala ya ubunifu na kuwatambua wabunifu kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mh. William Ole Nasha jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Ubunifu iliyoandaliwa na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Ole Nasha akizungumza na wabunifu (hawapo pichani) katika ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Ubunifu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Ole Nasha amesema, serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele katika teknolojia ili kuongeza chachu ya maendeleo na ipo tayari kufadhili bunifu mbalimbali zitakazochangia maendeleo ya uchumi wa Viwanda ifikapo 2025.

Naibu Waziri Ole Nasha amewataka waandaji wa maonesho hayo kuyapeleka katika maeneo ya wazi na rahisi kufikika ili wananchi wengi wapate fursa ya kujionea bunifu hizo.

"Wabunifu wengi ni wale wanaokumbana na changamoto za kila siku na kujaribu kuangalia namna ya kuzitatua hivyo wakati mwingine mtakapoandaa wiki ya ubunifu muhakikishe kwamba mnaweka katika maeneo ya wazi kwa ajili ya kuwakutanisha wabunifu wengi na wananchi ili waweze kujua kinachofanyika," ameeleza.

Baadhi ya wabunifu wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Ole Nasha (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Ubunifu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha Ole Nasha amewaasa wabunifu kufanya bunifu zitakazoendana na changamoto za maisha zilizopo nchini na siyo kufanya bunifu za kujifurahisha sababu wanaweza kukosa soko.

Naye, Kiongozi Mkuu wa Mfuko (HDIF), David McGinty amesema wadau wa maendeleo nchini, wamekuwa wakichangia Tanzania kupanda viwango vya kimataifa vya ubunifu kwani mpaka wanafunzi wa vyuo na sekondari wanahamasishwa kutumia teknolojia kwa ajili ya kujifunzia.

Wiki ya Ubunifu inatekelezwa na Mfuko wa Ubunifu kwa Maendeleo ya Watu (HDIF) kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na wadau wengine.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. William Ole Nasha na Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa ubunifu.