Ijumaa, 29 Novemba 2019

NDALICHAKO AZINDUA CHUO CHA VETA NDOLAGE WILAYANI MULEBA - 380 KUDAHILIWA JANUARI 2020

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezindua chuo kipya cha VETA Ndolage kilichopo Kamachumu Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kilichojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 281.

Ujenzi wa Chuo hicho ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya kushirikiana na jamii kufikisha Elimu ya Ufundi karibu na Wananchi pamoja na kujenga Vyuo vya VETA katika kila Wilaya nchini ifikapo mwaka 2020, ambapo Wizara imetenga zaidi ya Sh. bilioni 40 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo vya VETA katika Wilaya 25 nchini.

Ujenzi wa Chuo cha Ndolage ulianzishwa na Wananchi kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Muleba  Kaskazini, Charles Mwijage ambapo wananchi walitoa kiwanja na kuanza ujenzi wa madarasa kwa kutumia michango yao.

Akizungumza katika hafla hiyo Profesa Ndalichako amewataka VETA  kuhakikisha wanajenga majengo yote yanayohitajika  katika Chuo hicho kwa kutumia mapato ya ndani ya VETA.

"Nimezindua Chuo hiki lakini sijaridhishwa na majengo, ni machache na hayana hadhi kwani Wizara imetoa hela kulingana na mahitaji  yenu, inakuwaje bado kuna changamoto za majengo? Natoa miezi sita mkamilishe kwa fedha zenu," alisisitiza Ndalichako.

Wakati huo huo Ndalichako amewashukuru Wananchi wa Ndolage na Mbunge wa Jimbo hilo  kwa  hatua ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto na Vijana katika eneo hilo wanapata Elimu kwa kujitolea ardhi bure kwa ajili ya ujenzi huo na kuchangia fedha za vifaa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ameishukuru Wizara ya Elimu kwa ujenzi wa Chuo hicho na ameahidi kuhamasisha Wananchi kuandikisha Vijana wao kujiunga na Chuo hicho.

Akitoa salamu za VETA, Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Peter Maduki amesema Chuo hicho kitadahili wanafunzi 80 wa kozi za muda mrefu na wanafunzi 300 wa kozi fupifupi ambao wanatarajiwa kuanza mafunzo Januari mwaka 2020.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo hilo la Muleba kaskazini, Charles Mwijage ameishukuru Serikali kwa kujenga Chuo  hicho huku akiushauri uongozi wa VETA kuongeza mafunzo ya fani ya usindikaji mazao  kwani wananchi wa eneo hilo wamejikita katika kilimo.

Mafunzo mengine yatakayotolewa katika Chuo hicho ni ya fani za  Uashi, Ushonaji, Uhazili, Urembo na Uungaji wa Vyuma.

TANZANIA CHINA KUJENGA CHUO KIKUBWA CHA VETA MKOANI KAGERA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amezindua ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Kagera na kusema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni muendelezo wa jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kunakuwa na Vyuo vya ufundi stadi vya Mikoa na Wilaya.

Akizindua ujenzi wa chuo hicho mkoani Kagera Waziri Ndalichako amesema  chuo hicho  kinajengwa  na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu tulio nao  na kwamba pindi ujenzi  utakapokamilika vijana wengi wa kitanzania watapata fursa ya kusoma katika chuo hicho na kupata ujuzi katika fani mbalimbali zitakazo fundishwa.

"Kama nilivyosema Tanzania na China ni marafiki na rafiki yako anaangalia mahitaji yako, waswahili husema akufaaye kwa dhiki ndio rafiki wa kweli. China imeona Tanzania inajenga uchumi wa Viwanda ikiwa ni azma ya serikali ya awamu ya Tano  nao wakaamua watuunge mkono katika ujenzi wa Chuo cha Ufundi stadi ili kuandaa vijana wenye ujuzi watakaofanya kazi katika viwanda.

"Nikuombe Balozi  tufikishie shukrani zetu za dhati kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa msaada huu mkubwa na wa kihistoria ,"aliongeza Waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako amesema ujio wa mradi huo utaongeza ajira kwa vijana wa kitanzania kwa kuwa wazawa 400 wataajiriwa katika mradi huo ikiwa ni pamoja na kupata  ujuzi  kulingana na kazi watakazokuwa wakizitekeleza.

"Vijana watakaofanya kazi eneo la mradi pamoja na kufanya kazi  watapata na mafunzo, kwa hiyo ujuzi wao wa kiufundi utaimarishwa kupitia kazi ambazo watakuwa wakifanya katika mradi,"alisema waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA kupitia upya fani zilizopangwa kutolewa katika chuo hicho ili ziendane na Mazingira halisi ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.

"Nimepitia fani ambazo zimeanishwa kutolewa katika chuo hiki pindi kitakapokamilika, nikiangalia eneo ambalo chuo kinajengwa ni eneo la ziwa na watu wa Kagera au wazazi wa hapa ni wavuvi lakini sijaona kozi ya uvuvi sasa tunawaletea mambo ya uchomeleaji, ufundi bomba, useremala, upakaji rangi kwenye bahari, nilitegemea kuwe na fani ya uvuvi pia
 tuweke fani zinazoendana na mazingira," alisema Waziri Ndalichako

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania Balozi WANG Ke amesema Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania amezingatia maboresho ya sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwaongoza watanzania kuelekea dira ya  maendeleo 2025 hivyo China iko tayari kuchangia maendeleo katika sekta ya elimu ili kufikia malengo ya elimu ambayo serikali ya tanzania imejiwekea.

Nae Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Generali Marco Gaguti  amewataka wanakagera hasa vijana kushiriki vizuri katika kazi za ujenzi zitakazofanyika katika mradi huo  ili kupata ujuzi wa ufundi ambao utawasaidia kushirikia katika kazi za ujenzi zitakazojitokeza katika Mkoa wa Kagera mara baada ya mradi kukamilika.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi   VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema Chuo hicho kinajengwa katika eneo lililotolewa na wananchi wa kijiji cha Burugo wilayani Bukoba na lina ukubwa wa hekta 40. 5 sawa na hekari 100.

Dkt. Bujulu amesema Chuo hicho pindi kitakapokamilika kitatoa fani za useremala, uchomeleaji, upakaji rangi, ufundi bomba na kitachukua wanafunzi 800 wa kozi ndefu na 2000 wa kozi fupi

Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Mkoa wa Kagera kinajengwa kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  kwa gharama za fedha za kitanzania sh bilioni 19.4  ambapo ujenzi wake utachukua miezi 18

Gharama hizo zinajumuisha usanifu, upembuzi yakinifu na ujenzi mpaka ukamilike.

Jumapili, 24 Novemba 2019

VYUO BINAFSI VINA MCHANGO MKUBWA KWENYE UTOAJI WA ELIMU YA JUU: PROF. NDALICHAKO

Serikali imesema inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na vyuo binafsi katika kuleta maendeleo ya elimu ya juu kikiwemo Chuo Kikuu cha St. John’s cha hapa nchini.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s ambapo amesema kuwepo kwa vyuo binafsi hapa nchini kunasaidia na kuwezesha nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya elimu ya juu.

Waziri Ndalichako amesema Chuo hicho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika utayarishaji wa wataalamu katika fani mbalimbali ikiwemo fani ya ufamasia, uuguzi, ualimu wa Sayansi na Sanaa, kilimo, usimamizi wa fedha, uendeshaji katika utawala, masoko, uhasibu na wataalamu wa maabara.

“Nimeelezwa kuwa tangu chuo hichi kuanza mwaka 2007 hadi hivi sasa kimeweza kutoa wahitimu wasiopuungua elfu kumi na mbili, huu ni mchango mkubwa kwa Taifa letu, hongereni sana,” alisema Prof Ndalichako.


Amewapongeza wahadhiri wa Chuo hicho kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuwafundisha vijana ambapo amewataka kuendelea kuwaandaa vema wahitimu ili wakawe chachu na mfano wa kuigwa katika jamii wanazokwenda kuishi baada ya kuhitimu masomo yao.

“Nimefurahi kusikia kuwa Chuo hiki pamoja na masuala ya kitaaluma kinatilia mkazo suala la maadili, kinasisitiza umuhimu wa wanachuo kumuheshimu Mungu, kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa bidii na kuwa tayari kuhudumia wengine,” aliongeza Prof. Ndalichako.


Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amesema suala la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo wanapata na kuwawezesha kusoma bila changamoto yoyote.

“Nimefarijika kusikia kwamba idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo katika chuo cha St. John’s imeongezeka na kwamba mikopo hiyo inatoka kwa wakati, na hii niwaambie ukweli ni mpango wa Mhe. Rais. Mtakumbuka wakati akifanya kampeni aliahidi na kueleza namna alivyokuwa akisononeka kuona watoto wa kitanzania, wanafunzi wa elimu ya Juu walivyokuwa wakihangaika kupata fedha za mikopo, hivyo jambo la kwanza aliliolifanya alipoingia madarakani ni kuongeza kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya mikopo kutoka bilioni 341 mwaka 2014/15 na sasa fedha zilizotengwa  kwa mwaka 2019/20 ni sh bilioni 450,” alisema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa wakati akitolea mfano wanafunzi  ambao wameanza masomo mwanzoni mwa mwezi Novemba 2019 Serikali imetoa fedha zao tangu mwezi Septemba.

“Hadi kufikia Oktoba 15, 2019 Serikali ilikuwa imekwishatoa jumla ya sh bilioni 185 sawa na asilimia 41 ya fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2019/20,” alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuviagiza vyuo vyote nchini ambavyo kwa namna moja au nyingine bado havijatoa fedha kwa wanafunzi kutoa fedha hizo kwani Serikali inatoa fedha kwa ajili ya wanafunzi na sio kwa ajili ya vyuo.

Aidha Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wanaohitimu masomo ya elimu ya juu kuwa mabalozi wazuri wa vyuo walivyosoma na Taifa kwa ujumla huku akiwataka kuwa wazalendo na watu ambao wanaweka maslahi ya taifa mbele na kupinga vitendo vya aina yoyote vyenye lengo la kuvuruga amani na mshikamano wa Taifa letu.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St.John’s, Prof. Yohana Msanjila amesema wanafunzi wanaohitimu katika Chuo hicho kwa mwaka 2019 wako 1,730 huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaopata mikopo ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi mzuri wa utoaji mikopo ya elimu ya juu.

“Fedha za wanafunzi na ada zao zinatolewa mapema tofauti na miaka ya nyuma. Nakuomba mgeni rasmi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako utufikishie pongezi zetu kwa Mhe. Rais kwamba siku hizi fedha za mikopo na ada za wanafunzi zinafika kwa wakati na hii imesaidia kudumisha utulivu chuoni. Hongera kwa Serikali yetu, hongera Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu,” alisema Prof Msanjila.

Mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s kwa mwaka 2019 yalikuwa na Kauli mbiu isemayo “Udijitalishaji wa Elimu ya Juu kwa Vyuo binafsi: Kiungo Bora kwa Uchumi wa Viwanda.”

Ijumaa, 15 Novemba 2019

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA KIMATAIFA WA *GIRL*GUIDES*


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imejizatiti  na ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba  inaondoa fikra potofu kuhusiana na masuala ya kijinsia.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo jijni Dar e Salaam alipomuwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike (Girl Guides) katika masuala ya Uongozi ijulikanayo kama Julitte Low Seminar.

Amesema lengo la semina ni kupanua na kuimarisha ushiriki wa wasichana katika masuala ya girl guides lakini pia kuwawezesha kushirikiana katika masula ya kiutamaduni na uongozi ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo wasichana hao ili wazidi kufanya vizuri zaidi katika Jamii wanazotoka.

“Naamini baada ya semina hii ya siku saba wasichana watakuwa na uwezo kushiriki katika masuala ya uongozi na kukemea imani potofu ambazo zinakuwa zikionesha kuwa mwanamke ni kiumbe dhaifu na kutengeneza mtazamo chanya kuwa wanawake ni viumbe kama wanaume na wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu,”Alisema Prof Ndalichako.

Prof Ndalichako amesema Nchi ya Tanzania inatekeleza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia na kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanawake na wanaume wana fursa sawa katika maendeleo.

“Mhe Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu asingeweza kupata nafasi aliyo nayo kama nchi ingekuwa bado ina dhana potofu , uwepo wake ktk nafasi ya Makamu wa Rais, viongozi na wataamu  wengine katika nyanja mbalimbali  inaonesha kuwa nchi yetu imepiga hatua katika kuweka usawa wa kijinsia ”aliongeza Prof ndalichako

Amewapongeza Waandaaji wa Semina hiyo kwa kuchagua Tanzania kuwa nchi mwenyeji na kwamba Tanzania ina historia ya kutoa wanawake ambao ni wa nguvu akiwataja viongozi hao kwa uchache  kuwa ni marehemu bibi Titi Mohamed ambaye amekuwa kiongozi wa nchi yetu wakati wa uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Getrude Mongela ambaye alishiriki kwenye mkutano wa Beijing, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anna makinda na  sasa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Girl Guides Taifa Prof Martha Qorro amesema semina  ya mafunzo ya uongozi kwa vijana wa kike (Girl Guides) inafanyika ulimwengu mzima na itasaidia wasichana hao  kujitegemea, kujitambua, kujithamini, kupenda taifa lao kumpenda Mungu kuhesimu wengine na kusaidia mahali popote panapohitaji msaada.

Kwa upande wake mwakilishi wa Bodi ya Dunia katika "World Association of Girl Guide and Girl Scout" kwa kanda ya Afrika  Florentina Mganga amesema semina hii inaendelea ulimwenguni kote na vijana wa kike 700 watapata mafunzo juu wa uongozi  na itawawezesha kujua kuwa mtoto wa kike anaweza kuwa kiongozi wanachotakiwa ni kujiamini.

Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya masula ya uongozi inashirikisha nchi 17 ambazo ni Marekani, Uingereza, Ujerumani  Swizaland, Ghana, Zimbawe, Malawi, Rwanda, Burundi, Kenya, Madagascar, Egypt, Germany,Uganda,  Sierra Leone, Poland, Hong Kong, Philippines na Tanzania ikiwa kama Mwenyeji wao.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako na Prof Martha Qorro ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Girl Guides Taifa wakifurahia ngoma kutoka kwa wanafunzi wa shule ya msingi Diomond (hawapo pichani)wakati wa ufunguzi wa semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya masuala ya uongozi inayofanyika jijini Dar es Salaam
Girl Guides kutoka shule ya Msingi Oasis ya jijini Dar es Salaam wakiimba ngonjera mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana hao  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiwa kwenye picha ya pamoja na Girl Guides   wa shule ya msingi Oasisi ya jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo vijana wa kike kwenye masuala ya uongozi inayofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Makamishna na Volunteers wa Girl Guides Tanzania wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani)wakiwa wameshika bendera za nchi mbalimbali wakati wa ufunguzi wa semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya uongozi iitwayo Juliette Low Seminar Jijini Dar es Salaam
Baadhi  ya Girl Guides kutoka nchi mbalimbali wanaoshiriki semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo watoto wa kike juu ya masuala ya uongozi ijulikanayo kama Juliette Low  inayofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa seminia hiyo


Alhamisi, 14 Novemba 2019

ZAIDI YA MILIONI 280 ZATUMIKA KUJENGA NA KUKARABATI MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI BUHANGIJA

Serikali kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imetumia kiasi cha shilingi milioni 286.6 kwa ajili ya kukarabati na kujenga miundombinu katika shule ya msingi Buhangija ya Mkoani Shinyanga.

Akizungumza shuleni hapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Selemani Kipanya amesema mwaka 2018 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliipatia shule hiyo fedha hizo kwa ajili ya kujenga vyumba vinne vya madarasa, mabweni mawili na matundu 18  ya vyoo.

"Majengo haya yamesaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vyooni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia," amesema Mwalimu Kipanya.

Mwalimu Kipanya amesema shule hiyo ambayo ni jumuishi ina jumla ya wanafunzi 1,052 ambapo kati yao 230 ni wenye mahitaji maalum na kwamba wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wanaishi bweni wakati wengine wanasoma kutwa.

Naye Mwalimu Mohamed Makana ameishukuru serikali kwa kuikumbuka shule hiyo ambayo ilikuwa na changamoto nyingi za miundombinu pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia hasa kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mwalimu Makana amesema shule hiyo imepatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kutosha kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo kofia pamoja na miwani kwa ajili ya watoto wenye ualbino.

Mwanafunzi Jesca Michael mwenye ualbino ameishukuru Serikali kwa kuwalinda pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia huku akiiomba serikali kuendelea kuwaangalia kwa ukaribu wanafunzi wenye mahitaji maalum ili nao waendelee kupata elimu bora.


Darasa lililojumuisha watoto wenye mahitaji maalum na wale wa kawaida katika shule ya msingi BuhangijaBaadhi ya miundombinu iliyojengwa na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika shule ya msingi Buhangija iyopo mkoani Shinyanga 
Mtoto mwenye ulemavu wa kutokuona akitumia kifaa maalum kwa ajili ya kuandikia katika shule ya msingi Buhingili. Kifaa hicho ni moja ya vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum .


ZAIDI YA MILIONI 280 ZATUMIKA KUJENGA NA KUKARABATI MIUNDOMBINU YA SHULE...

Jumapili, 10 Novemba 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATEMBELEA SHULE YA WASICHANA MISUNGWI

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SULE WA WILAYA ZA MISUNGWI NA SHINYANGA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako leo Novemba 9, 2019 amefungua majengo ya ofisi mpya za Uthibiti Ubora wa Shule za Halmashauri ya  Wilaya ya Misungwi na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa ofisi hizo Waziri Ndalichako amewataka wathibiti Ubora wa Wilaya kufanya kazi kwa bidii na weledi na waone kuwa uwepo wa ofisi hizo uwe chachu ya kuendelea kutoa taarifa za ukaguzi wa shule zenye ubora na kwa wakati. Ndalichako amewataka kuhakikisha kuwa changamoto zinazoainishwa katika kaguzi zao zinafanyiwa kazi ili kuinua ubora wa elimu hususan katika taaluma  na sekta ya elimu  kwa ujumla katika wilaya hizo.

"Tumieni ofisi hizi kuwa chachu ya kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa za changamoto zinazozikabili shule pamoja na sekta nzima ya elimu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka," amesema Profesa Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema serikali itahakikisha changamoto zote zinazowakabili wathibiti ubora wa shule nchini zinafanyiwa kazi kwa dhati ili  kuzipunguza ama kuzimaliza kabisa  ikiwemo ukosefu wa ofisi na vitendea kazi.

Akizungumzia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya sekta ya elimu  unaoendelea nchini,  Profesa Ndalichako amesema suala hilo ni endelevu na litakuwa likifanyiwa kazi muda wote ili kuwezesha utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka wathibiti ubora wa shule kwa kushirikiana na Maafisa Elimu kufanya tathimini za kina kila mara ili kubaini sababu halisi za mdondoko wa wanafunzi wote wa kike na kiume.

"Tumeona hapa Misungwi takwimu zinaonyesha mdondoko mkubwa zaidi upo kwa upande wa watoto, hivyo fanyeni tathimini ili tujue sababu na kuacha kuegemea upande mmoja wa mtoti wa kike na kwamba sababu ni mimba" amesema Profesa Ndalichako

Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameishukuru serikali kwa kuhakikisha wathibiti ubora wa shule wanapata ofisi za kisasa na vitendea kazi na kuhaidi  kuwa wilaya ya Misungwi itaendelea kusimamia ubora wa elimu na kuongeza ufaulu katika ngazi zote.

"Sisi tutaendelea kusimamia utoaji wa elimu bora kwa watoto wote wa hapa Misungwi pamoja na kupunguza  mdondoko wa wanafunzi kwa kuanzisha mpango wa kutoa chakula shuleni" amesitiza Mkuu wa Wilaya.

Naye Mthibiti Mkuu wa Wilaya hiyo, Faustine Sahala ameishukuru serikali kwa kuona changamoto zilizokuwa zikiwakabili za ukosefu ofisi ambapo walipatiwa zaidi ya shilingi milioni 152 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo.
Sahala amesema ujenzi wa ofisi hiyo umekamilika kwa asilimia 100 pamoja na ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo mashine  ya kurudufu (photocopy), ufungaji  mtandao wa internet, uwekaji samani,  camera za ulinzi (CCTV) na ujenzi wa vyoo vya nje.

Katika Mpango huu Serikali inajenga ofisi 100 za Wadhibiti Ubora wa shule katika Halmashauri 100  kwa shilingi bilioni 15.2


Jumatano, 6 Novemba 2019

WAZIRI NDALICHAKO AKUTANA NA MKUU MPYA WA ELIMU KUTOKA UNICEFWaziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako leo Novemba 6, 2019 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Elimu Tanzania kutoka Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) Tanzania, Dkt. Daniel Baheta.

Dkt. Baheta amefika katika ofisi za Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizopo Jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha  baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo ambapo amemweleza waziri kuwa UNICEF inatekeleza vipaumbele vitatu katika sekta ya elimu.

Mkuu huyo amevitaja vipambele vya Kimataifa vya UNICEF kuwa ni kuwa ni ubora katika utoaji elimu na ujifunzaji, elimu kwa  vijana, ajira  na kutatua changamoto ya mdondoko wa wanafunzi katika shule.

Waziri Nadlichako amesema angependa kuona UNICEF ikishirikiana zaidi na Serikali  katika kuimarisha mafunzo ya stadi za maisha ambazo zitawawezesha wanafunzi wa kike kukwepa vishawishi vinavyosababisha mdondoko shuleni na ukuzaji wa ushirikishwaji jamii katika kusimamia ubora wa elimu na wanafunzi.

Katika mazungumzo yao wamekubaliana kutekeleza programu   ambazo ni pamoja na kuanzisha mfumo wa kidigitali wa kusimamia mahudhurio ya wanafunzi na kuwezesha mawasiliano kati ya Taasisi za elimu  na wazazi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako awakiangalia kishikwambi pamoja na wageni kutoka UNICEF

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na Mkuu wa Elimu kutoka UNICEF Tanzania Dkt. Daniel Bahate (Mwenye suti ya bluu) aliyefika ofisi kwake leo jijini Dodoma kwa lengo la kujitambulisha. 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Dkt Daniel Bahate (kushoto) Mkuu wa Elimu kutoka UNICEF Tanzania.

MIAKA 4 YA SERIKALI YA AWAMU YA TANO. MWANAFUNZI AELEZA ALIVYOFAIDIKA NA...

Jumatatu, 4 Novemba 2019

WANAFUNZI MWAKA WA KWANZA WALIOPATA MIKOPO WAFIKIA 46,838

Jumapili, Novemba 3, 2019

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya tatu yenye jumla ya wanafunzi wa mwaka kwanza 4,785 waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 14.3 bilioni na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 162.86 bilioni hadi sasa kufikia 46,838.

Orodha ya kwanza ilitolewa Oktoba 17 mwaka huu na ilikuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 30,675 waliopata mikopo yennye thamani ya TZS 113.5 bilioni. Orodha ya pili ilitolewa Oktoba 26 mwaka huu ikiwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 11,378 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 35.06 bilioni.

Taarifa iliyotolewa leo (Jumapili, Novemba 3, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru imeeleza kuwa wanafunzi waliopata mikopo katika awamu ya tatu wanaweza kupata taarifa zao kupitia akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account.

Pamoja na SIPA, Badru amesema majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya pili yanapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo (https://olas.heslb.go.tz) na tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).

“Awamu hii ya tatu inajumuisha wanafunzi wahitaji ambao wamekamilisha taratibu za udahili pamoja na kukamilisha marekebisho ya maombi yao yaliyokuwa na dosari … tutaendelea kufanyia kazi maombi yanayorekebishwa na wale wenye sifa watapangiwa,” amesema Badru. 

Kuhusu taratibu za malipo kwa wanafunzi, Badru amesema fedha za wanafunzi waliopata mikopo zimeshapelekwa vyuoni na vyuo vimeleekezwa kuhakikisha fedha zinawafikia wanafunzi walengwa mara wanapofika na kukamilisha taratibu za usajili.

“Serikali imeshatupatia TZS 125 bilioni ambazo tulikuwa tunazihitaji kwa ajili ya malipo ya robo ya kwanza ya Oktoba hadi Disemba mwaka huu na sisi tumeshatuma vyuoni na maafisa wetu wameanza kwenda vyuoni ili kukutana na wanafunzi na kutatua changamoto iwapo zitajitokeza,” amesema Badru.

Badru amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga TZS 450 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 128,285. Kati yao, wanafunzi 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, tatu na kuendelea.

Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Mwisho.

Ijumaa, 1 Novemba 2019

WIZARA YA ELIMU YAPONGEZWA KWA KUREJESHA MASHINDANO YA UMISAVUTA

SERIKALI YATENGA BILION 201 KWA AJILI YA UBORESHAJI NA UJENZI WA MIUNDOM...

SERIKALI KUIMARISHA MICHEZO KATIKA VYUO VYA UALIMU


Serikali ya Awamu ya Tano imeweka kipaumbele katika kuimarisha michezo kama eneo muhimu la mtaala wa mafunzo ya ualimu kutokana na ukweli kwamba michezo inaimarisha stadi za kujifunza, nidhamu na ni ajira pia.

Hayo yamesemwa Mkoani Mtwara na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa kufunga Mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara (UMISAVUTA).
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa kombe la ushindi wa mpira wa miguu kwa wachezaji wa Kanda ya Ziwa wakati wa ufungaji wa mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa ya Vyuo vya Ualimu UMISAVUTA yaliyomalizika mkoani Mtwara.

Amesema pamoja na kuwepo kwa mchepuo wa michezo katika baadhi ya vyuo vya Ualimu ni vizuri vyuo hivyo kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu wakaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ufundishaji na ujifunzaji wa michezo na Sanaa unalenga kuwawezesha vijana kufanya vizuri katika eneo hilo kwa maendeleo yao na Taifa.

Ametaja vyuo ambavyo kwa sasa vinatoa mchepuo wa michezo kuwa ni Chuo cha Ualimu Tarime, Butiama, Butiama Mtwara Kawaida na Ilonga na kwamba Wizara itahakikisha kuwa michezo inaimarishwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini.

Naibu Waziri Ole Nasha amevitaka vyuo vya ualimu kuhakikisha vinaendeleza michezo chuoni kutoka na faida zitokanazo na michezo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  wahitimu wa mafunzo ya ualimu wanapata mafunzo ambayo wakihitimu wanakwenda kuwa walimu mahiri wa michezo katika shule za msingi na sekondari ambapo ndipo wanamichezo na wasanii wanaandaliwa.

“Nimefarijika kuona mashindano ya michezo na Sanaa kwa vyuo vya ualimu imerudi tena baada ya kutokuwepo kwa miaka 20 iliyopita hatuna budi kuwekeza katika michezo kwa sababu ni fursa za kuweza kusaidia kukua kiuchumi. Nchi nyingi duniani michezo imekuwa sehemu kubwa ya kusaidia kukua kiuchumi,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akisalimiana na wachezaji kabla ya kuanza mechi ya fainali wakati wa ufungaji wa Mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara yaliyofanyika Mkoani Mtwara.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambae pia ni Afisa Elimu Mkoa Germina Mng’aho amesema kufanyika kwa michezo hiyo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inataka kuwepo kwa mashindano ya michezo kwa shule na vyuo ili kuwezesha kuinua vipaji ambavyo vitaleta mafanikio katika michezo ya kitaifa na kimataifa.

Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agusta Lupokela amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua faida zinazopatikana katika michezo ikiwemo stadi za kujifunza na kuamua kurejesha mashindano ya michezo kwenye Vyuo vya Ualimu.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na TeknolojiaAgusta Lupokela akikabidhi kikombe kwa mwakilishi wa Kanda ya Kaskazini ambao ni washindi wa mbio wakati wa kufunga mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu, UMISAVUTA mkoani Mtwara

Akitoa taarifa ya mashindano hayo kwa  Naibu Waziri Mwenyekiti wa UMISAVUTA Taifa Agustine Sahili amesema kuwa michezo hiyo imeendeshwa kulingna na taratibu za michezo na matokeo yameamuliwa kwa weledi na haki katika kupata washindi.

Sahili ameiomba  Wizara  kuimarisha kozi ya michezo na fani mbalimbali za ndani katika vyuo vya ualimu ili wataalamu waweze kupatikana shuleni ambako ndiko chimbuko halisi la vipaji linapatikana lakini pia kuwajengea uwezo wasimamizi na waamuzi wa michezo kwa kuendesha kozi fupi na ndefu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Pia ameiomba Wizara kuongeza wakufunzi wa michezo na Sanaa vyuoni kwani kwa sasa vyuo vingi havina wakufunzi wa aina hiyo hali inayodunisha uendeshaji wa michezo na ukuzaji wa vipaji kwa vijana chuoni ambapo pia inasababisha shule za msingi na sekondari kukosa walimu mahiri katika michezo na Sanaa.
Wanamichezo wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa kufunga mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ulimu yaliyofanyika Mkoani Mtwara.

Nae Mshiriki wa Mashindano ya Michezo na Sanaa Albert Thomas kutoka Kanda ya Ziwa ameishukuru Serikali kwa kurejesha mashindano ya UMISAVUTA kwani inasaidia kujenga afya na  akili lakini pia inasaidia kuwa na uelewa wa masula ya michezo na kutoa elimu ya michezo kwa wanafunzi ambao watakwenda kuwafundisha  baada ya kumaliza masomo. Ameiomba Serikali kuendeleza vipaji vya wanamichezo wanaoshindana katika mashindano ya ngazi ya shule na vyuo na kuonekana washindi ili vipaji hivyo visiishie kwenye ngazi ya kitaifa bali katika ngazi ya kimataifa.

Ufungaji wa mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa vyuo vya ualimu yaliyoanza Oktoba 25, 2019 na kuhitimishwa Oktoba 31, 2019 yamepambwa na mechi kati ya Kanda ya ziwa na kanda ya kusini ambapo kanda ya ziwa wameibuka kidedea baada ya kuwafunga kanda ya kusini goli moja kwa sifuri.
Kanda ya Ziwa wakifurahia kupata vikombe vya ushindi katika michezo mbalimbali ambayo wameshindania katika mashindano ya kitaifa ya michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara yaliyofanyika Mkoani Mtwara.