Jumatano, 12 Septemba 2018

WIZARA YA ELIMU YAWAJENGEA UWEZO WABUNGE WA KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII KUHUSU MAJUKUMU YANAYOTEKELEZWA NA WIZARA HIYO


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia leo imewajengea uwezo Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kuwasilisha majukumu 14 yanayotekelezwa na Wizara hiyo kwa mujibu wa hati idhini iliyotolewa April 22, 2016.

Akiwasilisha majukumu hayo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Makuru Petro ametaja majukumu hayo kuwa ni pamoja na kutunga na kutekeleza Sera za Elimu, utafiti, Huduma za Maktaba, Sayansi na Teknolojia na uendelezaji wa mafunzo ya Ufundi, kuendeleza Elimu kwa kutoa ithibati ya mafunzo ya Ualimu na Maendeleo ya kitaalamu ya Walimu, Kusimamia uendelezaji wa mafunzo katika vyuo vya Maendeleo ya wananchi, na kusimamia mfumo wa tuzo wa Taifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akifafanua jambo kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Wizara hiyo wakati wa kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii mkoani Dodoma.

Majukumu mengine ni kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi, kuweka viwango vya Taaluma ya Ualimu ikiwemo kuanzisha bodi ya kitaalamu ya walimu, kusimami ithibati na uthibiti ubora wa shule kwa kuweka viwango, kusimamia Huduma za machapisho ya kielimu ikiwemo mitaala na vitabu, kuimarisha utumiaji wa Sayansi, Teknolojia na hisabati, kuendeleza wataalamu wa ndani katika Sayansi na Teknolojia, kuratibu na kusimamia utafiti, ubunifu katika fani za Sayansi na Teknolojia, kusimamia Tume ya Taifa ya UNESCO, uendelezaji wa Rasilimali watu na kuratibu shughuli za Idara, mashirika, wakala, programu na miradi iliyo chini ya Wizara.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo wakati wa kikao na  Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika mkoani Dodoma.

Kupitia uwasilishaji wa majukumu hayo ya Wizara wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo walipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na Wabunge kwa lengo la kupata uelewa.

Baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakishiriki kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika mkoani Dodoma
Taasisi zilizoshiriki katika kujibu maswali mbalimbali ya Wabunge ni pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, (NACTE), Tume ya vyuo Vikuu Tanzania, (TCU), Taaaisi ya Elimu Tanzania (TET).
1.      Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakishiriki kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika mkoani Dodoma

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni