Jumanne, 24 Mei 2016




JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


TAARIFA KWA UMMA
USAJILI WA SHULE ZA AWALI, MSINGI, SEKONDARI NA VITUO VINAVYOTOA ELIMU NJE YA MFUMO RASMI NA SEKONDARI HURIA  

Serikali kupitia Sheria ya Elimu Sura ya 353 inaelekeza  shule zote kusajiliwa kabla ya kusajili wanafunzi. Azma hii ya serikali ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na utaratibu madhubuti wa kusimamia Ubora wa Elimu.

Hata hivyo, kumekuwepo na baadhi ya wadau wanaanzisha na kuendesha shule au vituo vinavyotoa elimu nje ya mfumo rasmi  bila kupata Usajili.

Wanafunzi wanaotoka katika shule au vituo hivi hufanya mitihani ya taifa ikiwemo  mtihani wa maarifa (QT)  na mitihani mingine ya Taifa (Kidato cha Nne na Sita)  kama watahiniwa wa kujitegemea. Aidha, baadhi ya wanafunzi hawa huingizwa kwa utaratibu usio rasmi kufanya mitihani ya Darasa la Nne na Darasa la Saba katika shule zilizosajiliwa pasipo kuzingatia mazingira ya mahali waliposomea hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kushindwa katika mitihani hiyo.

Kwa tangazo hili serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inawataka wamiliki wote wa shule ambazo hazijasajiliwa kuwasilisha maombi yao katika Ofisi za Uthibiti Ubora wa shule Kanda, Wilaya au Idara ya Ithibati ya shule (Usajili) Makao Makuu ya wizara kabla au ifikapo tarehe 30/07/2016. Shule ambazo hazijafikia vigezo vya kusajiliwa, zitafungwa na hazitasajiliwa na Mwenye Shule husika atapaswa kuhamisha wanafunzi waliopo kwa gharama zake. 

Imetolewa na

Dkt. Leonard D. Akwilapo
KAIMU KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA