Ijumaa, 14 Desemba 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tzChuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S.L.P. 10,
40479 DODOMA.

Tarehe: 10 Desemba, 2018.

WARAKA WA ELIMU NA. 2 WA MWAKA 2018
UTARATIBU WA KUKARIRI DARASA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI

Serikali imekuwa na utaratibu wa kupokea na kushughulikia maombi ya kukariri darasa kutoka kwa baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali. Aidha, Shule Zisizo za Serikali zimekuwa zikiwakaririsha darasa wanafunzi wanaoshindwa kufikia viwango vya ufaulu vinavyopangwa na shule husika.

Kufuatia hali hiyo kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wazazi na walezi kutokana na kutoshirikishwa ipasavyo katika kufanya uamuzi wa mwanafunzi kukariri darasa. Kutokana na changamoto zinazojitokeza kwenye suala hili wizara inapenda kutoa maelekezo kama ifuatavyo:

1.0 Kukariri Darasa
Maombi ya Kukariri darasa kwa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari yatashughulikiwa kama ifuatavyo:
(a)                  Maombi ya Kukariri darasa la I, II na III yatashughulikiwa na Halmashauri husika ambapo darasa la IV, V na VI kwa Shule za Msingi na kidato cha 1, 2, 3, na 5 kwa shule za Sekondari yatashughulikiwa na Mkoa;
(b)         Maombi ya kukariri darasa la VII kwa shule za Msingi na Kidato cha 4 na 6 ambayo ni madarasa ya mitihani ya mwisho ya Kitaifa yataendelea kutumwa kwa Kamishna wa Elimu ili kupata kibali cha kukariri; na
(c)                  Mwanafunzi atakayeomba na kukubaliwa kukariri katika ngazi ya Elimu ya Msingi na Sekondari atapewa fursa ya kukariri mara moja. Endapo mamlaka inayohusika itaona umuhimu wa Mwanafunzi kukariri darasa  mara ya pili, ataweza kupewa fursa hiyo.

(d)         Utaratibu wa Maombi ya Kukariri Darasa
                                 i.        Mzazi wa mwanafunzi wa darasa la I, II na III anatakiwa kuandika barua ya maombi ya kukariri darasa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri husika;
                               ii.       Mzazi wa mwanafunzi wa  darasa la IV, V na VI kwa shule za Msingi na Kidato cha 1, 2, 3, na 5 kwa shule za Sekondari anatakiwa kuandika barua kwa Katibu Tawala wa Mkoa;
                        iii.            Mzazi wa mwanafunzi wa darasa la VII kwa Shule za Msingi na Kidato cha 4 na 6 kwa shule za Sekondari anatakiwa kuandika barua kwa Kamishna wa Elimu kulingana na darasa husika;
                        iv.            Maombi yote yapitie kwa Mkuu wa Shule anayosoma mwanafunzi na Mkurugenzi wa Halmashauri husika, na
                           v.            Kila barua ya maombi ni lazima iwe na viambatisho vifuatavyo:
a.      Picha 2 za mwanafunzi aina ya pasipoti;
b.     Namba ya kuandikishwa shuleni; na
c.      Nyaraka zozote muhimu kulingana na sababu ya maombi                                        yanayowasilishwa.

2.0    Kukariri Darasa Wanafunzi Wanaoshindwa Kufikia Viwango vya Ufaulu Vilivyowekwa na Shule

Wizara inakumbusha kuwa wanafunzi waliofaulu mitihani ya upimaji inayofanywa kitaifa (Darasa la IV na Kidato cha 2) wanakuwa na sifa ya kumaliza ngazi ya elimu husika bila kukariri.

Hata hivyo, kwa makubaliano ya maandishi kati ya mzazi au mlezi na Mkuu wa shule ya Serikali au isiyo ya Serikali, mwanafunzi ataruhusiwa kukariri Darasa kwa kufuata utaratibu ulioainishwa hapo juu ambapo mzazi atakuwa ameridhia.

Waraka huu unafuta nyaraka zote zilizotangulia zilizokuwa zikitoa maelekezo kuhusu utaratibu wa kukariri darasa na utaanza kutumika Januari, 2019.Dkt. Edicome C. Shirima
KAIMU KAMISHNA WA ELIMU

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.