Ijumaa, 14 Desemba 2018


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Anuani ya simu “ELIMU”
Simu: 026  296 35 33
Baruapepe:info@moe.go.tz
Tovuti: www.moe.go.tz
Chuo cha Masomo ya Biashara
na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jengo Na. 10,
S.L.P. 10,
40479 DODOMA.

Tarehe: 14 Desemba, 2018.


WARAKA NA. 1 WA MWAKA 2018
MWONGOZO WA UUNDAJI NA UENDESHAJI WA KAMATI NA BODI ZA SHULE
Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Na. 25 ya mwaka 1978 na Rekebisho lake Sura 353 ya mwaka 2002 kila Shule ya Msingi na Sekondari sharti iwe na Kamati ya Shule (kwa shule za Awali na Msingi) au Bodi ya Shule (kwa shule za Sekondari) iliyo hai. Aidha, Serikali imekuwa ikitoa miongozo juu ya utaratibu wa kuunda na kuendesha Kamati na Bodi hizo.
Waraka huu unalenga kutoa mwongozo mahsusi kuhusu muundo, wajibu na uendeshaji wa Kamati na Bodi za shule.

1.0        KAMATI ZA SHULE ZA AWALI NA MSINGI/BODI ZA SHULE ZA SEKONDARI
1.1     Kamati za Shule za Awali na Msingi za Serikali na Zisizo za Serikali
Shule zote zitakuwa na Kamati (Kwa Shule za Awali na Msingi) na Bodi kwa Shule za Sekondari).

1.2   Sifa za Wajumbe na Utaratibu wa Uundaji wa Kamati na Bodi za Shule
a)            Itaundwa na wajumbe wasiopungua tisa (9),
b)            Diwani, Mwenyekiti na Katibu wa Serikali ya Kijiji/Mtaa (wa eneo shule ilipo) hawatakuwa na sifa ya kuwa wajumbe wa Kamati/Bodi ya shule. Hii ni kuepusha mgongano wa kiutendaji kutokana na jukumu lao la kuiwakilisha Serikali katika ngazi zao za utawala,
c)            Kamati itakuwa na vikao visivyopungua viwili (2) kwa mwaka. Mwenyekiti anaweza kuitisha kikao cha dharura kama kuna suala linalohitaji kujadiliwa,
d)            Wajumbe wa Kamati/ Bodi wanatakiwa wawe na sifa zifuatazo:
                                                  i.Wawe na elimu ya Kidato cha Nne au zaidi,
                                                ii.Wawe na shughuli halali za kujipatia kipato,
                                              iii.Uwiano wa wajumbe uzingatie jinsi zote mbili,
                                              iv.Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti achaguliwe na Wajumbe wa Kamati kutoka miongoni mwao.
e)            Kamati ya Shule itakuwa na kamati ndogondogo tatu (3) zifuatazo:
                                                i.     Kamati ya Taaluma, Malezi na Unasihi,
                                                ii.Kamati ya Fedha, Mipango na Miundombinu, na
                                              iii.Kamati ya Mazingira, Afya na Chakula.
f)              Wajumbe wa Kamati/Bodi za Shule watathibitishwa na Afisa Elimu wa Wilaya.


1.3 Wajibu na Majukumu ya Kamati ya Shule
a)            Kuandaa/kuidhinisha Mpango wa Maendeleo ya shule na mikakati ya utekelezaji wake,
b)            Kuitisha na kuendesha vikao vya wazazi na kutoa taarifa ya maendeleo ya shule,
c)            Kwa shule za serikali kuidhinisha matumizi ya fedha za shule na kusimamia matumizi bora ya fedha za uendeshaji na maendeleo ya shule,
d)            Kwa shule zisizo za serikali, kushauri namna bora ya matumizi ya fedha  kwa miradi ya maendeleo ya shule ikiwemo ukarabati wa miundombinu,
e)            Kuhimiza ujenzi wa shule na usafi wa mazingira ya shule na wanafunzi,
f)             Kwa shule za serikali, kusimamia ujenzi na ukarabati wa madarasa na miundombinu mingine na utunzaji wa mazingira ya shule,
g)            Kusimamia ufundishaji na ujifunzaji shuleni kwa kuhakikisha kuwa walimu wanafanya kazi zao kwa ufanisi,
h)            Kuhakikisha wanafunzi wote wanahudhuria masomo kwa mujibu wa sheria,
i)             Kuhakikisha shule inakuwa na Sanduku la Huduma ya Kwanza na pia shule inadumisha elimu ya afya shuleni kwa njia mbalimbali,
j)             Kuhakikisha huduma za Malezi na Unasihi kwa wanafunzi zinaendeshwa kwa ufanisi shuleni,
k)            Kutathmini uhalali wa kumsimamisha/kumfukuza shule mwanafunzi bila upendeleo wala kushawishiwa na mtu au kikundi chochote kabla ya kuhalalisha uamuzi huo,
l)             Kuhakikisha Kamati inakutana ndani ya wiki mbili inapotokea shule imependekeza kumsimamisha/kumfukuza mwanafunzi ili uamuzi sahihi utolewe kwa wakati kuepusha ucheleweshaji unaoweza kuathiri haki za kielimu za mwanafunzi husika pasipo sababu za msingi, na
m)         Kamati itafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu (3).


2.0 MUUNDO WA KAMATI/BODI ZA SHULE
Katika kuunda Kamati na Bodi za Shule za Serikali na zisizo za Serikali mambo yafuatayo yatazingatiwa:

2.1   Wajumbe wa Kamati za Shule za Awali na Msingi za Serikali
                           i.            Mwalimu Mkuu ambaye pia atakuwa Katibu wa Kamati,
                        ii.            Mwalimu wa Taaluma katika shule,
                      iii.            Wawakilishi wawili (2) wa walimu shuleni,
                       iv.            Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo naye atakua Mjumbe,
                         v.            Wajumbe watatu (3) watakaochaguliwa na mkutano wa wazazi, na
                       vi.            Mkazi jirani atakayeteuliwa na Mkuu wa shule.

2.2     Kamati za Shule za Awali na Msingi Zisizo za Serikali
                             i.         Mkuu wa shule ambaye atakuwa Katibu wa Kamati ya shule,
                           ii.         Mmiliki wa shule,
                         iii.         Mwalimu wa Taaluma,
                         iv.         Wajumbe watatu (3) watakaoteuliwa na Mmiliki wa Shule,
                           v.         Mwakilishi mmoja (1) wa walimu shuleni.  
                         vi.         Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo naye atakua Mjumbe,
                    vii.            Mzazi mmoja (1) anayewakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi,
                  viii.            Mkazi mmoja jirani atakayeteuliwa na Mwenye shule.

2.3   Bodi za Shule za Sekondari za Serikali
                              i.         Mkuu wa Shule ambaye atakuwa Katibu wa Bodi,
                           ii.         Mwalimu wa Taaluma katika shule,
                         iii.         Wawakilishi wawili (2) wa walimu shuleni,
                          iv.         Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum; Mkuu wa Kitengo pia atakua mjumbe katika Bodi ya shule,
                            v.         Wajumbe watatu (3) wanaowakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo watakaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa wazazi, na
                          vi.         Mkazi jirani atakayeteuliwa na Mkuu wa shule.

2.4   Bodi za Shule za Sekondari Zisizo za Serikali
                    i.              Mkuu wa shule ambaye atakuwa Katibu wa Bodi ya shule,
                  ii.              Mmiliki wa shule,
                iii.              Mwalimu wa Taaluma,
                iv.              Wajumbe watatu (3) watakaoteuliwa na Mmiliki wa Shule,
                  v.              Mwakilishi mmoja (1) wa walimu shuleni.  
                vi.              Iwapo shule ina kitengo kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, Mkuu wa Kitengo pia atakua Mjumbe,
              vii.              Mzazi mmoja (1) anayewakilisha wazazi wenye watoto katika shule hiyo atakayechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wazazi,
            viii.              Mkazi mmoja jirani atakayeteuliwa na Mwenye Shule.

Waraka huu unafuta Nyaraka zote za awali zilizokuwa zinatoa Mwongozo kuhusu Kamati za Shule za Awali na Msingi na Bodi za Shule za Sekondari na utaanza kutumika kuanzia Januari, 2019.
Dkt. Edicome C. Shirima

KAIMU KAMISHNA WA ELIMUNakala:      Makatibu Tawala wa Mikoa,
                    Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya/Mji/Manispaa/Jiji,
                    Wathibiti Ubora wa Shule Wakuu Kanda na Wilaya.

Maoni 8 :

 1. JE,KAMA MWENYEKITI WA KIJIJI HAWEZI KUWA MJUMBE WA BODI?

  JibuFuta
 2. Kwenye kamati waalimu ni wengi, huoni katka upigaji kura kumchagua m/kiti na makamu wanaoamua apite nani ni wajumbe upande wa waalimu, kwa kuwa wao ni wengi na hawagombei nafasi hizo.Ni nini muongozokuhusu hilo?

  JibuFuta
 3. Hawezi kuwa mjumbe kwa sababu ya kuepuka msuguano wa masilahi

  JibuFuta
 4. Utaratibu wa kujiondoa katika bodi ya shule Ni upi?

  JibuFuta
 5. Sidhani Kama ipo sawa huwezi kuwaweka walimu wengi hivo halafu useme kamati no uwakilishi was wazazi huu muundo hauwezi kudhibiti fedha za shule

  JibuFuta
 6. Je kamati ya nidhamu ya walimu ngazi ya shule inaundwa na akina nani? Yaani muundo wa kamati ya nidhamu ni upi?

  JibuFuta

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.