Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imetangaza sehemu ya pili ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na
mafunzo ya ualimu katika vyuo 35 vya serikali.
Akitoa taarifa hiyo
jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema jumla ya wanafunzi 2,834
wamechaguliwa kujiungana mafunzo ya ualimu ambapo kati yao 1,013 ni wa
Astashahada na 1,821 ni wa Stashahada.
Dkt. Akwilapo ameongeza
kuwa hadi sasa jumla ya wanafunzi 11,028 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya
ualimu vya serikali ambapo kati yao wanafunzi 8,194 walichaguliwa awali na
TAMISEMI na 2,834 wamechaguliwa na NACTE.
Aidha, Dkt. Akwilapo
amewataka wanafunzi hao waliochaguliwa kuripoti katika vyuo walivyopangiwa
kuanzia tarehe 20 Septemba mwaka huu na kwamba mwisho wa kuripoti ni tarehe 6
Oktoba mwaka huu. Amesisitiza
wahakikishe wanaripoti ndani ya muda huo kwani baada ya hapo hawatapokelewa na
nafasi zao zitajazwa na wengine wenye sifa ambao walikosa nafasi.
“Wanafunzi wote
waliochaguliwa wanatakiwa waripoti katika vyuo vyao kuanzia tarehe 20 mwezi huu
hadi 6 Oktoba mwaka huu. Watakaoripoti baada ya hapo hawatapokelewa na
nafasi zao zitajazwa na wanafunzi wengine walioomba ambao wana sifa ila
walikosa nafasi,” amesisitiza Dkt. Akwilapo.
Aidha, Dkt. Akwilapo
amesema serikali inatambua kuwepo kwa wanafunzi wengi waliokosa nafasi za
kujiunga na masomo katika kozi mbalimbali na hivyo ameliagiza Baraza la Taifa
la Elimu ya Ufundi (NACTE) kufungua dirisha dogo la udahili kwa siku 14 kuanzia
tarehe 7 Septemba ili wanafunzi waliokosa nafasi za masomo katika kada
mbalimbali waweze kutumia fursa hiyo.
“Wizara inatambua kuwepo
kwa idadi kubwa ya waombaji waliokosa nafasi katika awamu hii kutokana aidha na
ushindani au kutofanya uchaguzi sahihi wa kozi hivyo wizara inaiagiza NACTE
kufungua dirisha dogo la udahili kuanzia leo tarehe 7 hadi 21 Septemba ili
kuwapa nafasi waombaji waliokosa nafasi katika programu mbalimbali waweze
kufanya uchaguzi upya,” amesema Dkt. Akwilapo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Avemaria Semakafu akiongea katika
mkutano huo amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakichagua kozi ambazo hawana
sifa zinazohitajika. Amewaasa waombaju kuzingatia
sifa za kozi ili kuepuka kuenguliwa kwani masharti yanayowekwa kuhusu sifa
hayabadilishwi.
“Utakuta kwa mfano mtu
ana ufaulu mzuri wa alama A hadi C katika masomo ya lugha, badala ya kuchagua
kozi zinazotaka ufaulu wa lugha yeye atachagua kozi za masomo ya sayansi ambayo
kapata alama D, matokeo yake anajikuta hachaguliwi katika kozi alizoomba,”
amesema Dkt. Semakafu.
Naye Mkuu wa Kitengo cha
Udahili wa NACTE, Twaha Twaha amewatahadharisha waombaji hasa wa kozi za afya
kuhakikisha kuwa wamefaulu vizuri katika masomo ya sayansi kwani ndio sifa ya
msingi katika udahili wa kozi hizo.
“Katika kozi za afya
vigezo vinaangalia masomo, mfano mwanafunzi anayetaka kusoma clinical medicine
au nursing, anatakiwa awe na ufaulu wa alama D katika masomo ya Physics,
Chemistry na Biology. Sifa zote hizi
zipo katika kitabu cha Mwongozo wa Udahili ambacho kinapatikana kwenye tovuti
ya NACTE ambayo ni www.nacte.go.tz,” amesema Twaha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.