Serikali inatambua na
kuthamini mchango wa Asasi za Kijamii, ikiwemo HakiElimu, katika kuweka mkazo
kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa
jumla.
Kauli hiyo ya
Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti ya
HakiElimu kuhusu changamoto za Elimu ya mtoto wa Kike.
Dkt. Akwilapo amesema
nia ya Serikali ni kushirikiana na wadau wa elimu ili
kuona kuwa vikwazo vyote dhidi ya elimu kwa mtoto wa kike vinapatiwa suluhisho
sahihi.
“Ili kufanya maamuzi
sahihi, Wizara ninayoiongoza hutumia uthibitisho unaotokana na tafiti mbalimbali
zinazofanywa na Wizara yenyewe na wadau wengine wa elimu. Sisi kama watunga
sera hatuwezi kufanya kazi kwa ufanisi bila ya kutumia matokeo ya utafiti,” Alisema
Dkt. Akwilapo.
Dkt Akwilapo
ameipongeza Taasisi ya HakiElimu kwa kuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti
mbalimbali ambazo zinatoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu.
“Ripoti ya utafiti ninayoizindua leo ni mfano hai wa
kile ninachokisema kuhusu mchango wa Sekta binafsi kwani inahusu changamoto
zinazosababisha wasichana kushindwa kuendelea na masomo na kuvuka katika hatua
nyingine. Utafiti huu unaendana na lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa
wasichana wanaoandikishwa katika Elimumsingi wanamaliza safari yao ya elimu kwa
mafanikio makubwa,” aliongeza Dkt. Akwilapo.
Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika
kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu Dkt. Akwilapo amesema Serikali imekuja
na Sera
ya Elimu bila malipo katika ngazi ya Elimumsingi ambayo imewezesha wasichana
wengi kuandikishwa katika shule ikiwa ni pamoja na Ujenzi wa mabweni ambayo
yamesaidia kuwaweka wasichana karibu na shule na kuepuka vishawishi vya
barabarani wakati wa kwenda na kurudi shule.
Jitihada nyingine ni kutunga
sheria ambayo inawabana watu wanaotaka kuoa watoto wa shule au kushirikiana nao
kimapenzi, na hivyo kuwaharibia masomo kwa kuwapa ujauzito pamoja na kutoa
elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, Dkt. John Kalaghe akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa ripoti ya Utafiti kuhusu wasichana kushindwa kuendelea na masomo iliyofanyika Jijini Dodoma. |
Naye Mkurugenzi
Mtendaji HakiElimu, Dkt. John Kalaghe amesema azma ya kufanya utafiti huu imechagizwa
na kampeni ya Elimu ya mtoto wa kike ambayo HakiElimu inaifanya. Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji
wa mpango mkakati wa mwaka 2017 hadi 2021 ambao wamejiwekea na umejikita katika
kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha kwamba watoto
wa kitanzania wakiwemo watoto wa kike wanapata elimu bora itakayowawezesha
kukabili changamoto katika maisha yao na kusaidia ujenzi wa Taifa letu.
“HakiElimu tunatilia
mkazo katika kuhamasisha utolewaji wa elimu jumuishi yenye ubora na usawa pamoja
na elimu kwa watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kupunguza au kuondoa kabisa
unyanyasaji wa watoto shuleni na nje ya mipaka ya shule,” Alisema Dkt. Kalaghe.