Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameutaka Uongozi wa Benki ya
Biashara ya Mwalimu (MCB BANK) kuboresha huduma za kifedha ikiwemo kuweka vivutio
na masharti rafiki ambayo yatawawezesha walimu nchini kukopa fedha ili kukuza
vipato vyao.
Prof. Ndalichako
ametoa wito huo wakati akifunga Kongamano la Walimu wilayani Kasulu mkoani
Kigoma na kusisitiza kuwa matarajio ya serikali ni kuona benki hiyo inakuwa
rafiki kwa walimu nchini kwa kuondoa adha na vikwazo ambavyo kwa muda mrefu
walimu wamekuwa wakikabiliana navyo katika taasisi mbalimbali za kifedha.
"Benki ya
Biashara ya Mwalimu iwe na ahueni kwa mwalimu anapokuwa ni mteja katika kufanya
hivyo walimu wengi watahamasika kujiunga na benki hii, kupitishia mishahara
pamoja na hata kuchukua mikopo"
Aidha ameutaka Uongozi wa benki hiyo
kusimamia vizuri fedha iliyokwisha wekezwa na walimu ili kuwavutia
walimu wengine ambao bado hawajajiunga na kusisitiza kuwepo na kasi ya
uanzishwaji wa ofisi za benki hiyo katika mikoa yote nchini iongezeke ili
kuwavutia wateja.
"Nafahamu kwamba
tayari mnatoa huduma kidijitali na
mnashirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma katika maeneo ambayo hamna ofisi,
lakini ni muhimu mkaharakisha uanzishwaji wa ofisi zenu kila mkoa ili
kurahisisha upatikanaji wa huduma," amesema Ndalichako.
Waziri Ndalichako pia
amewaasa walimu nchini kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba pindi wanapopata
mishahara yao ili iwasaidie kuanzisha miradi mingine ya kiuchumi ambayo itakuwa
mkombozi wa maisha yao pindi wanapostaafu.
"Walimu tambueni
akiba ni kile kitu unachokiweka kwanza kabla ya kuanza matumizi, lakini watu
wengi wanadhani akiba ni bakaa baada ya matumizi kwa utaratibu huo kamwe
hakutakuwa na kitu kinachobaki," amesema Ndalichako.
Baadhi ya Walimu wa mkoa wa
Kigoma walioshiriki Kongamano wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako. Kongamano limeandaliwa na Benki ya
Biashara ya walimu ili kutoa elimu ya kifedha kwao.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara ya Mwalimu, Richard Makungwa amesema benki
hiyo imeendelea kujiimarisha katika kusogeza
huduma kwa wateja wake na kwamba
tayari imeanzisha ofisi zake katika baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Mbeya, Morogoro na Mwanza huku
ikishirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma kwa wateja ambao bado mikoa yao
haijafikiwa.
Amesema katika benki
hiyo mwalimu mmoja anamiliki hisa takribani asilimia 35.28 huku chama cha
walimu na kampuni yao wakimiliki takribani asilimia 16.17.
"Ukiangalia
utakubaliana nami kuwa chombo hiki ni cha walimu na madhumuni yake ni kuwaletea
maendeleo wao wenyewe ndiyo maana tukasema lazima tuwafikie walimu popote
walipo," amesema Mkurugenzi huyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya
Biashara ya Mwalimu Richard Makungwa wakati wa hafla ya kufunga Kongamano la
Walimu lililoandaliwa na Benki hiyo Kasulu Mkoani Kigoma.
Naye Mkuu wa wilaya
ya Kasulu, Kanali Simon Anange amesema mara nyingi watumishi wanakosa nidhamu
ya fedha na kutumia zaidi ya kile anachopata na kusisitiza kuwa ni vizuri
walimu wakawa na utaratibu wa kujiwekea akiba ili pindi wanapostaafu waweze
kuishi maisha ambayo wameishi wakiwa kazini.
Mwalimu mstaafu
aliyeshiriki kongamano hilo, Kalist Tarimo ameishukuru Benki ya Biashara ya
Mwalimu kwa kufanya Kongamano hilo ili kutoa elimu kwao lakini pia ameishauri
benki hiyo kuwa na ofisi katika kila Wilaya ili walimu waweze kutumia huduma za
benki hiyo.
Kongamano hilo
limeandaliwa na Benki ya Biashara ya Mwalimu na limeshirikisha walimu kutoka
mkoa wa Kigoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa
Benki ya Biashara ya Mwalimu pamoja na baadhi ya walimu wa mkoa wa Kigoma
walioshiriki Kongamano hilo lililofanyika Kasulu Mkoani Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.