Jumamosi, 29 Januari 2022

WAZIRI MKENDA AITAKA DIT KUANZA KUTENGENEZA VIPURI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Wizarani na Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo Januari 28, 2022.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameitaka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kujitanua zaidi kwa kutengeneza vipuri vya vyombo vya moto ikiwemo vya bajaji na pikipiki.

Ameyasema hayo leo Januari 28, 2022 Jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Taasisi hiyo ili kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa hapo ambapo amesema tunaweza kukua kiteknolojia kwa kuboresha vitu ambavyo tayari vimeshatengenezwa na nchi nyingine.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda akizungumza na Menejimenti ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wakati alipotembelea taasisi hiyo Januari 28, 2022.

"Nimefurahi sana kuona mna kampuni inayosaidia kubiasharisha bidhaa za ubunifu ila niwatake mboreshe kwa kutengeneza vipuri ambavyo vinahitajika sana kama vya bajaji na pikipiki," amesema Prof. Mkenda.

Aidha Waziri Mkenda ameipongeza taasisi hiyo kwa kuwa na kampuni inayosaidia kubiasharisha bunifu mbalimbali na kuwataka  DIT kuhamisha ujuzi wa kiteknolojia kutoka nchi nyingine na kuja kuutumia hapa nchini katika uzalishaji wa bidhaa zitakazokidhi mahitaji ya jamii.

"Tunaweza tukaleta nchini kitu ambacho kimezalishwa mfano nchi ya Uturuki kisha tukaangalia uwezekano wa kukitengeneza na kukiuza ndani na nje ya nchi ili kukuza uchumi wetu," amesema Prof. Mkenda.

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda ameusisitiza uongozi wa DIT kuendelea kujenga na kukuza ushirikiano na taasisi nyingine hasa za nje ya nchi ili kubadilishana wataalamu watakaosaidia kuendelea kukuza teknolojia nchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda (mwenye tai) akiwa ameongozana na Mkuu wa Taasisi ya DIT, Prof. Preksedis Ndomba (kushoto) na maafisa wengine kutoka Wizarani na DIT,  wakati Waziri huyo alipotembelea taasisi hiyo Januari 28, 2022.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Preksedis Ndomba amesema wamepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji wa taasisi hiyo.