Jumatano, 13 Februari 2019

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA KUSIMAMISHWA KAZI ALIYEKUWA MKUU WA CHUO CHA UALIMU ILONGO NA WATUMISHI WENGINE WAWILI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kumvua madaraka na kumsimamisha kazi Benjamini Mwilapwa aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Ualimu Ilonga kabla ya kuhamishiwa Chuo cha Ualimu Mpwapwa  kwa kushindwa kusimamia ukarabati  Chuoni hapo.

Waziri Ndalichako pia amemuagiza Dkt. Akwilapo kuwasimamisha kazi watumishi wengine akiwemo afisa manunuzi na ugavi Ally Masanja na Muhasibu Godlove Yona ambao ni watumishi wa chuo hicho ili kupisha uchunguzi kwa kile kinachodaiwa kufanya manunuzi yasiyofuata taratibu na kulipa fedha kwa kazi ambazo hazijakamilika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya ujenzi wa mabweni katika Chuo cha Ualimu Ilonga kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.

Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo  mkoani Morogoro  alipofanya ziara chuoni hapo ya kukagua maendeleo ya ujenzi, na uboreshaji wa miundombinu inayofanywa na Wizara hiyo.

Amesema ukarabati uliofanyika hauridhishi huku aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho ambae ndie  alikuwa mwenyekiti wa kamati za ujenzi na manunuzi  chuoni hapo kuwa  mtoa maamuzi ya mwisho bila kujali kufuata  sheria ya manunuzi inayoelekeza unapotumia Force Akaunti unatakiwa kuwa na kamati aina gani na majukumu yake ni yapi. 

“Inaonekana Mkuu wa Chuo alipora madaraka, ninafahamu kuwa amehamishiwa Chuo cha Ualimu Mpwampwa  sasa namuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amrudishe na avuliwe madaraka mara moja, haiwezekani mtu akapandishwa cheo wakati Chuo hiki ambacho ni kidogo kilimshinda kusimamia ukarabati”, alisisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiangalia sakafu ya moja ya bweni lililokarabatiwa lakini bado imeonesha kuchakaa kwa muda mfupi.

Aliongeza kuwa kazi zilizofanyika za ukarabati chuoni hapo niza ubabaishaji na kwamba zimefanyika chini ya kiwango, akitolea mfano sakafu kwenye majengo yote kuonesha nyufa, huku nyongeza ya gharama za ukarabati zikiwa kubwa.

Pia Waziri Ndalichako amemtaka Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Profesa Joseph Msambichaka kufika katika Chuo Cha Ualimu Ilonga  siku ya  kesho , February 13, 2019 kuona namna wataalamu wa taasisi hiyo  walivyoshindwa kusimamia kazi waliyokabidhiwa kwao ambao ni  washauri elekezi.

Pia amemtaka Katibu Mkuu kuvisimamia kwa karibu vyuo vya ualimu kwa  kuwa sasa vimeanza kuwa kama vichaka ambapo michango haifuati utaratibu ikiwa  ni pamoja na kuitaka timu  ya wakaguzi wa wizara  waliofika chuoni hapo kufanya uchunguzi wa kina   kwa sababu inaelekea kuna mahali pengine nyaraka zilikuwa zinaghushiwa.
Muonekano wa Jengo la Utawala lililokarabatiwa katika Chuo cha Ualimu Ilonga kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi ameiomba wizara kama iliyo katika miradi  mingine inayotekelezwa na Serikali katika Wilaya hiyo kuhakikisha wanawahirikishwa kwa karibu ili waweze kusimamia kile kinachotekelezwa katika eneo husika.
Zaidi ya Shilingi bilioni moja zimetolewa na Serikali kukarabati Chuo cha Ualimu Ilonga kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.