Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imeanza kutoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule kote nchini ya
namna ya kutekeleza mfumo mpya wa Uthibiti Ubora wa Elimu.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mafunzo hayo Jijini Dodoma Mthibiti Mkuu wa Shule kutoka Wizara
hiyo Euphrasia Buchuma amesema mfumo huo unaondoa mfumo ambao wathibiti ubora
wamekuwa wakitazamwa kama polisi pindi wanapofika shuleni na kuwa watu ambao
wanatakiwa kutoa msaada katika shule.
Buchuma amesema mfumo huo
mpya unashirikisha jamii nzima ya shule Viongozi wote, Wazazi, Kamati za Shule,
Bodi ya shule na walimu ambao wanapaswa kufahamu Mthibiti Ubora wa Shule
anapoingia katika Shule anafanya nini katika shule hiyo na taarifa za ukaguzi
ni lazima ziwafikie viongozi wote wenye mamlaka na kutoa maamuzi.
Amesema kwa kuwa mfumo huu ni
shirikishi unaleta uwazi zaidi na kuondoa usiri ambao ulikuwapo katika mfumo
uliokuwa ukitumika zamani katika kukagua shule ambao uliitaji usiri kuanzia
unapokagua shule uandikaji wa ripoti na hata uwasilishaji wa taarifa ya
ukaguzi.
Mthibiti
Mkuu wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchuma
akiongea na Wathibiti Ubora wa Shule wakati wa ufunguzi wa mafunzo eelekezi ya
namna ya kutumia mfumo mpya wa ukaguzi wa Shule Jijini Dodoma.
Amewataka wathibiti ubora wa
shule kushiriki mafunzo hayo kikamilifu kwa kuwa wana dhamana kubwa ya Elimu na
kwamba kila mmoja kwa nafasi yake atambue wajibu wake, abadili mtizamo, afanye
kazi kwani kunahitajika mabadiliko makubwa katika kuhakikisha Elimu ya nchi hii
inatolewa kama inavyopaswa kutolewa.
“Tumekuwa tukinyooshewa
vidole sana kwamba hatufanyi kazi na ni kwa sababu matokeo yanaonekana kama
hatupo kumbe tupo, hatuonekani katika utendaji kazi na ndio maana kila
panapotokea tatizo tunaonekana hatupo na hatufanyi kazi tubadilike tufanye kazi
kwa moyo, bidii na weledi,” alisisitiza Buchuma
Baadhi
ya Wathibiti Ubora wa Shule wakifuatilia hotuba ya Mthibiti Mkuu wa Shule
kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchuma wakati wa
ufunguzi wa mafunzo elekeze kwa Wathibiti Ubora wa Shule ya nama ya kutumia
mfumo mpya wa ukaguzi wa Shule.
Katika hatua nyngine Buchuma
amewataka wathibiti ubora wa shule mara baada ya mafunzo hayo kukamilika, wahakikishe
wanakagua Shule zote za Sekondari ambazo ni Kongwe kwani zinaonesha kutofanya
vizuri katika miaka ya hivi karibuni.
“leo ukienda katika shule nyingi ukiukwaji wa sheria za
Shule ni mkubwa lakini na sisi tupo na hatusemi tunasema hatuhusiki, kimsingi
sisi ndio wasimamia Sera, Miongozo, taratibu na kanuni zote za uendeshaji wa shule
kuanzia ngazi ya Shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimuhivyo
tukafanye kazi,” aliongeza Buchuma
Mafunzo elekezi ya namna ya kufanya ukaguzi kwa mfumo
mpya wa uthibiti ubora wa Shule yanafanyika kwa siku nne kuanzia Julai 30,
mwaka huu nchi nzima.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.