Alhamisi, 21 Juni 2018

PROFESA MDOE APONGEZA UBUNIFU NA KUWATAKA WANAFUNZI WABUNIFU KUJITOKEZA KWA WINGI


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wanafunzi ambao wanakipaji cha ubunifu kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili waweze kuonyesha vipaji vyao, kwa kuwa bunifu zao zinatakiwa zitatue changamoto mbalimbali hapa nchini.

Profesa Mdoe ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifunga jukwaa la Maonesho ya ubunifu kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 13 hadi 21 yanayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mradi wa kukuza Ujuzi, na stadi za kazi, ESPJ.
Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema vijana wabunifu wakiendelezwa vyema watapata fursa ya kuchangia uchumi wa Taifa kupitia bunifu zao mbalimbali.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza na wadau mbalimbali wa masuala ya ubunifu wakati akifunga maonesho ya ubunifu yaliyohusisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kutoka Tanzania bara na Visiwani, yaliyofanyika mkoani Dodoma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza katika maonesho hayo ametambua mchango wa kijana Keton Mbwiro ambaye amehitimu Elimu yake ya Msingi na ameweza kubuni kijiko maalumu cha gari ambacho hutumika kuchimba na kuchota mchanga. Pia amebuni gari la kubeba vifaa vya ujenzi hivyo ameahidi kuwa kijana huyo atapelekwa shule ya ufundi ili aweze kujiendeleza.

“Keton Mbwiro ni kijana mdogo lakini ameweza kubuni kitu ambacho miaka ya nyuma tulizoea kuona vitu vya namna hii vinafanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu, hivyo uwezo wake lazima tuuendeleze kwa kuhakikisha anakwenda shule ya Ufundi, pia ni vyema watanzania tukaachana na dhana ya kuwa vyuo vya ufundi ni vya useremala pekee bali ni zaidi ya hapo.” anasema Dk. Semakafu.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiwa na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wakiangalia moja ya ubunifu uliohusisha mashine ya kusafishia/kuondoa uchafu kwenye mazulia. Maonesho hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Mjini Dodoma. 

Mradi wa kukuza Ujuzi na Stadi za kazi, ESPJ ni mradi wa miaka miatano ambao unatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia, lengo likiwa ni kuhakikisha mkakati wa Serikali wa Tanzania kuwa
nchi ya Uchumi wa viwanda mpaka 2025 inatimia.
Prof. James Mdoe ambae ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa ameshika chupa yenye dizeli iliyotokana na kuyeyushwa kwa chupa za plastiki ambazo zimekwisha matumizi yake.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni