Serikali ya Tanzania na Taasisi ya
African Institute for
Mathematical Sciences - Next
Einstein Initiative (AIMS-NEI) wamesaini Mkataba wa Makubaliano kuanzishwa
kwa kampasi ya taasisi hiyo nchini itakayofundisha na kuendeleza masomo ya Hisabati na Sayansi.
Mkataba huo umesainiwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome kwa upande
wa Serikali na Bwana Thierry Zomahoun,
Mkurugenzi Mtendaji wa AIMS-NEI
jijini Dar es Salaam.
Profesa Mchome amesema kusainiwa
kwa mkataba huo ni jitihada za Mheshimiwa
Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na wataalam wa kutosha
katika Nyanja za Hisabati na Sayansi. Mheshimiwa Rais alikutana na kufanya
mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo alipokuwa ziarani nchini Canada mwishoni
mwa mwaka jana.
Akizungumzia mkataba huo,
Profesa Mchome alisema “Hii ni nafasi ya pekee maana huwezi kupata Mainjinia
bila kujua hesabu, wala Madaktari na Wanasheria bila kuwa na ufahamu wa hesabu,
na hesabu ndiyo kila kitu,”.
Taasisi ya African Institute for Mathematical Science-Next
Einstein Initiative (AIMS-NEI), wameshafungua kampasi zake katika nchi za Afrika Kusini, Senegal, Ghana na
Cameroon, na kwa hapa Tanzania tayari wamepata eneo wilayani Bagamoyo katika
majengo ya Boma ambayo yatakarabatiwa. Kwa kuanzia masomo hayo yatatolewa
katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kilichopo Arusha ambapo wanafunzi 40 wa
awali wameshadahiliwa tayari kwa kuanza masomo hayo mwezi Septemba mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa African Institute for Mathematical Sciences-Next
Einstein Initiative (AIMS-NEI), Thierry Zomahoun, alisema Tanzania ni
miongoni mwa nchi bora kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ili ijijenge
katika misingi ya uchumi imara zaidi, haina budi kuwekeza katika masuala ya
hesabu na sayansi ili kupata watalaamu
watakaolisaidia taifa kusonga mbele kimaendeleo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.