Jumatatu, 6 Mei 2019

WATANZANIA WATAKIWA KUTHAMINI ELIMU INAYOTOLEWA NCHINI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Semakafu amesema Elimu inayotolewa nchini ina ubora unaokubalika ambapo amewataka wale wanaoibeza na kuidhalilisha kuacha kufanya hivyo.

Dkt. Semakafu ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kutunuku vyeti kwa wanafunzi washindi wa kitaifa ambao wameshiriki uandishi wa shindano la Insha za Jumuiya ya Maendeleo nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Yapo mengi yanasemwa kuhusu Elimu yetu, tuache kujidhalilisha maana wanafunzi wetu ambao wanawakilisha nchi nje ya Tanzania katika masuala ya kielimu wamekuwa wakifanya vizuri,” alisema Dkt. Semakafu.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. AveMari Sekafu akizungumza wakati wa hafla ya kutunuku vyeti kwa washindi wa Kitaifa wa shindano la uandishi wa Insha za Jumuiya ya Maendeleo nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Amewataka walimu kuwasaidia wanafunzi  kufuata taratibu wakati wa uandishi wa insha.

Kiongozi huyo amesema mashindano hayo ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika katika kujenga uelewa kwa wanafunzi juu ya kazi na mipango ya Jumuiya hizo.

Aliongeza kuwa uandishi wa insha unawapa wanafunzi hamasa ya kutafiti na kupata taarifa zaidi, kuelewa na kuwawezesha kujadili masuala mbalimbali kwa kina.

Kwa upande wake Mratibu wa mashindano hayo ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Ithibati ya shule Sylivia Chingwile ametoa wito kwa walimu na wazazi kuwahimiza wanafunzi kushiriki mashindano hayo ya insha na mengine yanayojitokeza, kwani uzoefu unaonesha wanafunzi wanaoshiriki katika mashindano hayo wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho.

Mshindi wa kwanza kikanda wa shindano la uandishi wa  Insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki Innocent Shirima ambae ni mlemavu wa macho kutoka shule ya Sekondari  Moshi iliyoko Mkoa wa Kilimanjaro akipokea zawadi  na cheti wakati wa hafla ya kutunuku washindi  wa shindano la insha, hafla hiyo hao imefanyika jijini Dodoma.

Naye Mwanafunzi mshindi wa insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kikanda kwa mwaka 2018 Innocent Shirima kutoka shule ya Sekondari ya Moshi, iliyopo mkoani Kilimanjaro ameshauri mashindano ya insha ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ziwe zinatoa fursa kwa wanafunzi kuchagua aina ya lugha wanayoweza kuitumia wakati wa kuandika insha hizo.

“Ili tuendelee kufanya vizuri katika masuala mbalimbali ya kijamii, nashauri kama ilivyo kwenye mashindano ya Insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatoa machaguzi ya lugha kama vile Kifaransa, Kiingereza au Kiswahili, hivyo hivyo ningeomba ifanyike kwa mashindano mengine kwa lengo la kutangaza lugha zetu hususan Kiswahili, ili siku moja tuje kuona Sudan Kusini wanaandika insha kwa lugha ya Kiswahili,” alisisitiza mwanafunzi Innocent Shirima.

Kwa maelezo zaidi kuhusu  taarifa za  mashindano hayo ya uandishi wa insha na namna ya kushiriki tembelea tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (www.moe.go.tz).

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Ave Maria Sekafu akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Kitaifa wa shindano la uandishi wa Insha za Jumuiya ya Maendeleo nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na zile za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni