Jumamosi, 4 Mei 2019

RAIS DKT. MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI MAKTABA YA CHUO KIKUU CHA SAYANSI NA TEKNOLOJIA MBEYA NA KUZUNGUMZA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU VILIVYOKO MBEYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2500 kwa wakati mmoja na inayogharimu shilingi bilioni 5.5.

Akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa  Vyuo Vikuu vyote vilivyoko  jijini Mbeya baada ya kuweka jiwe la msingi Rais Dkt. Magufuli ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na uongozi wa MUST kwa kuenzi mawazo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kukiendeleza  Chuo hicho ambacho kilianza mwaka  1986 kama Chuo cha Ufundi na hatimaye mwaka 2012 kuwa Chuo Kikuu pekee cha Sayansi na Teknolojia nchini.

Mhe . Dkt. Joh Pombe Pombe Joseph Magufuli ,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiongozana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako kuelekea eneo la uwekaji jiwe la Msingi ujenzi wa Maktaba Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya  (MUST).

Rais Magufuli pia amekipongeza chuo kwa kutoa mchango mkubwa kwa jamii ikiwemo kushiriki katika kusimamia kama wataalamu elekezi katika mradi wa  ukarabati wa shule kongwe, Vyuo vya Ualimu na ujenzi wa Mji wa Serikali Dodoma.

Pamoja na pongezi Rais Magufuli ameutaka uongozi wa Chuo hicho na Wizara kuhahakikisha jengo la Maktaba linakamilika kwani limechelewa na amewahakikishia kutoa fedha zilizobaki kiasi cha shilingi bilioni 2.9 mwezi wa huu wa tano ili kukamilisha kazi hiyo kwa haraka. Katika hatua ingine ametoa shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni huku akiagiza chuo kutumia wataalamu wake wa ndani kufanya kazi hiyo.
Mhe . Dkt. Joh Pombe Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwasalimu wanafunzi na wananchi waliofika katika viwanja vya Chuo Kikuu cha  Sayansi na Teknolojia Mbeya  (MUST) kumsikiliza wakati akiingia uwanjani hapo kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako.

“Nawapongeza lakini jengo hili limechukua muda mrefu sana miaka saba, sasa hakikisheni linakamilika na Chuo Kikuu Mzumbe jengeni kwa spidi kubwa majengo yakamilike kwa uwakati na ubora.”  

Aidha, Dkt. Magufuli ametoa wito kwa Vyuo Vikuu nchini kuendelea kujiimarisha kutoa elimu bora hasa katika zama hizi ambapo nchi yetu inaeleka Uchumi wa kati kupitia viwanda ambapo sayansi na teknolojia ndio msingi wa maendeleo hayo na kuwataka  wanafunzi kusoma kwa bidii na kujiepusha masuala yasiyo na msingi ili kuepuka kufeli na kupata maradhi ikiwemo ugonjwa wa ukimwi.

Awali akizungumza Waziri wa Elimu Syansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amempongeza na kumshukuru Rais kwa kuipa Elimu kipaumbele na Kuwekeza kiasi kikubwa ikiwemo fedha za ujenzi wa Maktaba MUST, uwekezaji wa ,Shilingi Bilioni 3.8 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Utawala na Madarasa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Mbeya, Shilingi  Bilioni 6.3 ujenzi wa hosteli za wanafunzi 1,024 Mzumbe Kampasi kuu Morogoro na shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya ujenzi wa maabara mtambuka itokayochukua wanafunzi 1600 kwa wakati mmoja katika Chuo Kikuu Sokoine cha kilimo.

Ndalichako amesema fedha nyingine zilizotolewa lwa ajili ya sekta ya Elimu ni Shilingi bilioni 12 za ujenzi wa kituo cha umahiri cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kikubwa katika Afrika Mashariki kinachojengwa katika Chuo kikuu cha Afya na Sayansi  Shirikishi Muhimbili  Kampasi ya  Mlonganzila.   Waziri Ndalichako amemuhakikishia Mhe. Rais kuwa Wizara yake itasimamia kikamilifu miradi hiyo.

Wanafunzi wa Vyuo vikuu vilivyoko Mbeya wakifurahia hotuba ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza nao katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Wakitoa salamu, wakuu wa Vyuo Vikuu vya Mzumbe na MUST wameishukuru Serikali na kuahidi kuendelea kutoa mafunzo na kozi zinazoendana na wakati , huku changamoto kubwa ikiwa ni kuchelewa kupata idhibati ya kuendesha programu mbalimbali walizoomba kutoka Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU).

Kufuatia hali hiyo Rais Magufuli  amemuagiza Waziri kuhakikisha ndani ya siku 10 Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania na wataalamu wake kutembelea Chuo cha Sayansi na Teknojia Mbeya  ili kutoa majibu ya ithibati za kozi zilizoombwa.

Katika hatua ingine Rais Mhe. Dkt. Magufuli  amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kufuatilia ujenzi wa barabara kuelekea katika Chuo cha MUST ijengwe kwa haraka ili kulinda hadhi ya Chuo hicho.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako mara baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa Maktaba ya chuo hicho cha MUST.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni