Jumapili, 10 Novemba 2019

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA OFISI ZA UTHIBITI UBORA WA SULE WA WILAYA ZA MISUNGWI NA SHINYANGA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako leo Novemba 9, 2019 amefungua majengo ya ofisi mpya za Uthibiti Ubora wa Shule za Halmashauri ya  Wilaya ya Misungwi na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Akizungumza baada ya ufunguzi wa ofisi hizo Waziri Ndalichako amewataka wathibiti Ubora wa Wilaya kufanya kazi kwa bidii na weledi na waone kuwa uwepo wa ofisi hizo uwe chachu ya kuendelea kutoa taarifa za ukaguzi wa shule zenye ubora na kwa wakati. Ndalichako amewataka kuhakikisha kuwa changamoto zinazoainishwa katika kaguzi zao zinafanyiwa kazi ili kuinua ubora wa elimu hususan katika taaluma  na sekta ya elimu  kwa ujumla katika wilaya hizo.

"Tumieni ofisi hizi kuwa chachu ya kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa taarifa za changamoto zinazozikabili shule pamoja na sekta nzima ya elimu ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka," amesema Profesa Ndalichako.

Prof. Ndalichako amesema serikali itahakikisha changamoto zote zinazowakabili wathibiti ubora wa shule nchini zinafanyiwa kazi kwa dhati ili  kuzipunguza ama kuzimaliza kabisa  ikiwemo ukosefu wa ofisi na vitendea kazi.

Akizungumzia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya sekta ya elimu  unaoendelea nchini,  Profesa Ndalichako amesema suala hilo ni endelevu na litakuwa likifanyiwa kazi muda wote ili kuwezesha utoaji wa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka wathibiti ubora wa shule kwa kushirikiana na Maafisa Elimu kufanya tathimini za kina kila mara ili kubaini sababu halisi za mdondoko wa wanafunzi wote wa kike na kiume.

"Tumeona hapa Misungwi takwimu zinaonyesha mdondoko mkubwa zaidi upo kwa upande wa watoto, hivyo fanyeni tathimini ili tujue sababu na kuacha kuegemea upande mmoja wa mtoti wa kike na kwamba sababu ni mimba" amesema Profesa Ndalichako

Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ameishukuru serikali kwa kuhakikisha wathibiti ubora wa shule wanapata ofisi za kisasa na vitendea kazi na kuhaidi  kuwa wilaya ya Misungwi itaendelea kusimamia ubora wa elimu na kuongeza ufaulu katika ngazi zote.

"Sisi tutaendelea kusimamia utoaji wa elimu bora kwa watoto wote wa hapa Misungwi pamoja na kupunguza  mdondoko wa wanafunzi kwa kuanzisha mpango wa kutoa chakula shuleni" amesitiza Mkuu wa Wilaya.

Naye Mthibiti Mkuu wa Wilaya hiyo, Faustine Sahala ameishukuru serikali kwa kuona changamoto zilizokuwa zikiwakabili za ukosefu ofisi ambapo walipatiwa zaidi ya shilingi milioni 152 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo.
Sahala amesema ujenzi wa ofisi hiyo umekamilika kwa asilimia 100 pamoja na ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo mashine  ya kurudufu (photocopy), ufungaji  mtandao wa internet, uwekaji samani,  camera za ulinzi (CCTV) na ujenzi wa vyoo vya nje.

Katika Mpango huu Serikali inajenga ofisi 100 za Wadhibiti Ubora wa shule katika Halmashauri 100  kwa shilingi bilioni 15.2


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni