Waziri wa Elimu na Mafunzo
ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa mwishoni mwa wiki alitembelea Taasisi ya African Institute for
Mathematical Sciences - Next
Einstein Initiative (AIMS-NEI) kampasi ya Tanzania na kuzungumza na
viongozi na wanafunzi wa Shahada ya Uzamili katika masomo ya Hisabati na Sayansi kwa mwaka 2015/16.
Taasisi ya AIMS hapa nchini imeanzisha kampasi yake Bagamoyo, mkoani Pwani ambapo
hivi sasa inatumia kwa muda majengo ya Alpha Zulu Villa na baadaye itatumia
majengo ya Old Boma na Datoo yaliyoko Bagamoyo mjini baada ya
kufanyiwa ukarabati.
Wanafunzi 45 kutoka nchi
mbalimbali za Afrika wamedahiliwa kuanza masomo katika taasisi ya AIMS – Tanzania kwa mwaka 2015/16
wakiwemo Watanzania 17 na wengine wanatoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda,
Burundi, Cameroon, DRC, Msumbiji, Nigeria, Zimbabwe, Afrika Kusini, Sudani na
mmoja anatoka Uingereza.
Kuanza kwa mafunzo hayo ni
jitihada za Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na wataalam
wa kutosha katika Nyanja za Hisabati na Sayansi. Mheshimiwa Rais alikutana na
kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo alipokuwa ziarani nchini Canada
mwishoni mwa mwaka juzi.