Serikali imesema
haitavumilia vitendo vya udhalilishaji ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika
baadhi ya shule hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukukuliwa
kwa wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa leo na
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako mkoani Dodoma
wakati akikabidhi tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika masomo yao
ya kuhitimu darasa la saba, Kidato Cha Nne na kidato Cha Sita kwa shule za
serikali na zisizokuwa za serikali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akitoa cheti na fedha kwa mwanafunzi bora
kitaifa katika masomo ya sayansi Sophia Juma aliyefanya vizuri katika matokeo ya kumaliza
kidato cha sita mwaka 2017. Utoaji wa tuzo hizo umefanyika mkoani Dodoma katika
kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu
Waziri Ndalichako amewataka
wanafunzi nchini kote kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu pamoja na kuishi kwa
kufuata maadili ya kitanzania na siyo kuiga maadili ya watu wa nje.
“Wakuu wa shule nchini kote
nawaagiza kuhakikisha mnasimamia kwa weledi malezi ya wanafunzi, ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha walimu mnakemea vitendo vya udhalilishaji ambavyo
vimekuwa vikijitokeza katika shule hapa nchini. Suala hili nasema si la
kufumbia macho na wale wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo hatua
kali za kisheria zitachukuliwa,” amesema Waziri Ndalichako.
Waziri Ndalichako amewaeleza
wanafunzi hao kuwa suala la kupata ushindi ni rahisi lakini kudumu katika
ushindi si kazi nyepesi.
Katibu
Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na
wajumbe walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Elimu (hawapo pichani) amesisitiza
kuwa lengo la utoaji wa tuzo katika Wiki ya Elimu ni kutoa motisha na kuongeza
ari kwa wanafunzi ili wafanye bidii katika masomo yao. Hafla ya utoaji wa tuzo
hizo umefanyika leo Mkoani Dodoma katika Shule ya Sekondari Dodoma.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge amewapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika
masomo yao kitaifa ambapo amesema Silaha pekee ya ujenzi wa Taifa na rasilimali
za Taifa ni Elimu, ambapo pia amewataka wanafunzi kudumisha nidhamu na maadili.
Akizungumza kwa niaba ya
Serikali ya Uingereza katika maadhimisho hayo ya wiki ya Elimu Gertrude
Mapunda amesema serikali ya Uingereza
itaendelea kuisaidia Serikali ya
Tanzania katika kuboresha sekta ya Elimu.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea maelezo ya
awali kutoka kwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango Gerald Mweli kuhusu vigezo
vilivyozingatiwa katika kupata wanafunzi bora waliofanya vizuri kitaifa katika
masomo yao ya kuhitimu darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita kwa
Shule za serikali na zisizokuwa za Serikali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.