Ijumaa, 4 Desemba 2015



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
 
Coat of arms of Tanzania.png

KATAZO LA KUONGEZA ADA KWA SHULE ZISIZO ZA SERIKALI KWA MWAKA WA MASOMO 2016
 
Waraka wa Elimu Na. 4 wa Mwaka 2008 uliweka viwango vya ada vinavyotozwa katika shule za Msingi na Sekondari za Serikali na zile zisizo za serikali. Ada iliyowekwa kwa shule za kutwa zisizo za serikali ni Tsh. 150,000/= na shule za bweni Tsh. 380,000/= kwa mwaka kwa kila mwanafunzi. Aidha waraka huo ulielekeza kwamba ongezeko lolote la ada lazima lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza kutumika.  
Hata hivyo imegundulika kuna baadhi ya shule zisizo za serikali zimekuwa zikiongeza ada kila mwaka pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu. Utamaduni huu wa kuongeza ada kila ifikapo mwishoni mwa mwaka umekuwa ukisababisha usumbufu mkubwa kwa wazazi/walezi na hata baadhi yao kushindwa kuendelea kusomesha vijana wao katika baadhi ya shule.
Kwa tangazo hili wamiliki wote wa shule zisizo za serikali wanaagizwa kufanya yafuatayo:
1.      Kutokuongeza gharama za uendeshaji wa shule zikiwemo ada kwa mwaka wa masomo unaoanzia mwezi Januari mwaka 2016 mpaka watakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu; wale ambao tayari wameongeza gharama na ada kwa mwaka wa masomo wa 2016 bila kibali cha Kamishna wa Elimu, Wizara haitambui ongezeko hilo kwa kuwa ni batili na hivyo zimefutwa.
2.      Ada zote kwa shule zisizo za serikali zitabaki kama zilivyokuwa zimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu.
3.      Kuwasilisha taarifa kwa Msajili wa Shule aliyepo Idara ya Ithibati ya Shule inayoeleza kiasi cha ada na gharama  kinachotozwa kwa sasa (kabla ya mwaka wa masomo 2016) na tarehe shule ilipopata kibali kutoka kwa Kamishna wa Elimu kutoza kiwango hicho cha ada.  Taarifa hiyo ifike ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe ya tangazo hili.
Wathibiti ubora wa shule waliopo sehemu mbalimbali nchini wanaagizwa kulifuatilia suala hili kwa karibu ili kila shule itekeleze agizo hili na kutoa taarifa zilizoelekezwa katika tangazo hili. Hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wamiliki ambao hawatatekeleza maagizo haya.  
Aidha Wizara iko katika hatua za mwisho za utafiti na kuandaa mfumo wa kielektroniki wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimumsingi (elimu ya awali, msingi na sekondari) na hivyo wadau mbalimbali watoe ushirikiano kwa timu za wataalamu wanaofanya kazi hii ili kusaidia katika kuukamilisha mfumo na hatimaye kuwa na ada elekezi katika maeneo mbalimbali.
 
     
IMETOLEWA NA KATIBU MKUU
 
 
 




 
 

Maoni 7 :

  1. kwanza napenda kuuliza kwa wizara ya elimu kwamba mwanafunzi ngazi ya shule ya msingi serikali/binafsi anatakiwa kuwa darasani kwa siku ngapi kwa mwaka mzima wa masomo?kwa nini shule za binafsi wanakuwa na mihula mitatu(sio zote)hivyo kuwa na likizo tatu kubwa na ndogo tatu na jumla kuwa na miezi mitatu na wiki tatu za likizo mwaka mzima wakati shule za serikali zina mihula miwili na kuwa na likizo mbili kubwa na ndogo mbili na kuwa na jumla ya miezi miwili na wiki mbili za likizo kwa mwaka mzima je serikali haiona hili kuwa ni unyonyaji unaofanywa dhahiri na shule hizi kwa wazazi wanaolipa mamilioni ya pesa kuwapatia watoto wao elimu/kuwakosesha wanafunzi muda wao muhimu wa mwezi mmoja na wiki moja wa kuwa darasanikama wenzao wa shule zingine hususan za serikali?.Kama haitoshi shule hizi nyingine ufungwa hata kabla ya wakati na kutulazimisha wazazi kupeleka watoto tuisheni wasikae muda mrefu nyumbani na kuwafanya wayasahau waliyofundishwa nyuma.Nakuomba mheshimiwa mwenye mamlaka ulione hili chini ya Mh Rais wetu Dr Magufuli.Hakuna sababu shule zingine ziige mfano wa nchi jirani yenye mihula mitatu wakati sisi tuna utaratibu wetu wa mihula miwili.Asante MH DR J P MAGUFULI.'HAPA KAZI TU'.

    JibuFuta
  2. Maoni yang mm serikal inatakiwa kufuatilia saana hili jambo

    JibuFuta
  3. Mimi maoni ni kwamba serikali iwe karibu na shule hizi za binafsi ama iteulowe kamati maalumu toka mamlaka husika,ili kuepupukana na mfumuko wa kupanda kwa ada kila wakati maana kweli baadhi ya wamiliki wa shule za binafsi, wamekua wakiwabebesha wazazi mzigo mkubwa mpaka kupelekea wengine kuuza mpaka nyumba zao na viwanja walivyowekeza kwaajili ya Maisha ya baadae.pia kwa swala la likizo ni kwamba wapewa amri wa kufunga shule pamoja na za serikali,ili kuepuka wazazi kupekeka watoto tuishen na kuepuka garama zisizo za lazima.

    JibuFuta
  4. Wizara imetuacha kwenye mataa, kwani kama wazazi hatujui gharama halisi amnazo tunatakiwa kulipia. Mfano shule wanayosoma watoto wangu tulitangaziwa kuwa ada ni laki 3 kwa muhula, sasa kwa tangazo hili la wizara ilitakiwa itoe mwongozo unaoelekeza namna ya kilipa.

    Inilikane kuwa kuna baadhi ya shule zilikiwa zinatoza ada kubwa na sasa wameongeza tena juu yake. Sasa kwa wizara kusema tu ada elekezi bila kuwa na utaratibu wa kuhakikisha kwamba hiyo ndo ada inayolipwa haitasaidia.

    wazazi wataendelea kulipa ada kubwa pasipo msaada. Na vipi wamiliki pia kuwalazimisha wazazi kulipia gharama za jengo?

    Ili zoezi ili lifanikiwe wizara itoe mwongozo kama ambavyo sumatra walivyoweka mwongozo kwenye mabasi, kwa kufanya hivyo mzazi anaenda dhule akijua gharama halisi.

    JibuFuta
  5. umbwe boyz huku kilimanjaro tuna tatizo la walimu wa accountancy msaaada tafadhari

    JibuFuta
  6. Maoni haya yameondolewa na mwandishi.

    JibuFuta
  7. ushauri wangu kuhusu kuboresha elimu yetu ni kwamba,serikali iangalie namna ya kumaliza matatizo ambayo yanasababishwa na watendaji waelimu pamoja na wakurugenzi. bahati nzuri mie ni mwalimu kwa kiasi kikubwa matatizo mengi ya walimu yapo kwa maafisa elimu na wakurugenzi. mfano upendeleo wa kupandishwa madaraja, likizo kutolipwa, matusi kwa walimu kutokuwathamini walimu kama watumishi, kutojibiwa haraka barua zao zinapopelekwa ofisini ni tatizo. naomba watanzania tuunge mkono jitahada za viongozi wetu wakubwa.

    JibuFuta