Benki ya Dunia imepongeza
Serikali ya Tanzania kwa kutoa kipaumbele
kwa sekta ya Elimu na kwamba ni moja kati ya nchi zilizofanikiwa sana
katika kuhakikisha watoto wenye umri wa kwenda shule wanapata nafasi hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa
jijni dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia ukanda wa nchi za
Africa Anne Kabagambe alipofanya ziara katika shule ya Sekondari Kibasila akiwa
na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na walimu wa Shule ya Sekondari
Kibasila ya Jijini Dar es Salaam (hawapo pichani) wakati alipofanya ziara
katika shule hiyo akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia kanda ya
Afrika Anne Kabagambe.
Mkurugenzi huyo ametembelea
shule ya Kibasila kwa sababu Benki ya Dunia inaendelea kushirikiana na Serikali
ya Tanzania katika juhudi zinazofanywa katika sekta ya elimu ikitambua kuwa
elimu ni ndio chimbuko la maendeleo katika katika nchi yoyote.
Nae Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amesema Benki ya Dunia imekuwa
ikishirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa Elimu unaojulika kama Lipa
Kulingana na Matokeo (EP4R) ambapo Benki ya Dunia imetoa dola za kimarekani
milioni 202 katika mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2014 na unategemewa
kumalizika mwaka 2021.
Walimu wa shule ya Sekondari
Kibasila iliyopo Jijini Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati alipotembelea shule hiyo
akiwa na ugeni kutoka Benki ya Dunia.
Waziri Ndalichako amesema
kupitia mradi huo takribani Sh bilioni 141 zimeshatumika kwa ajili ya kukarabati
shule kongwe 62, kujenga vyumba vya madarasa 2,876, matundu ya vyoo 6,558,
nyumba za walimu 59, mabwalo 76, majengo ya utawala 16, Mabweni 533 kwa ajili
ya kuwaepusha watoto wa kike na changamoto za mbalimbali, pamoja na kujenga
mifumo ya maji safi kwenye baadhi ya shule ambazo hazikuwa na vyanzo vya maji.
Aidha Waziri Ndalichako
alisema kwa upande wa Shule ya Sekondari Kibasila shilingi milioni 900 zimetengwa kwenye bajeti
ya mwaka wa fedha 2019/2020 kwa ajili ya
ukarabati na tayari wataalamu wameanza
kufanya tathmini ya majengo ya shule hiyo ambayo ukarabati wake utaanza wakati
wowote kuanzia sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki
ya Dunia kanda ya Afrika Anne Kabagambe akizungumza na walimu wa shule ya
sekondari Kibasila wakati alipotembelea shule hiyo. Ameipongeza serikali kwa
kutoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu.
Awali akitoa taarifa ya
shule Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibasila Yasinta Matilya amesema moja ya
changamoto inayokabili shule hiyo ni utoro wa wanafunzi unaotokana na
changamoto za kifamilia ikiwemo watoto kulelewa na mzazi mmoja, kipato duni,
umbali wa makazi ya wanafunzi.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wanafunzi wa shule hiyo wameiomba Serikali kuwapatia walimu wa
saikolojia watakaowasaidia kujitambua ikiwa ni pamoja na kuwajengea mabweni ili
kuepukana na vishawishi vya barabarani pamoja na usumbufu wa usafiri wa
unaopelekea wanafunzi kuacha shule.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji
wa Benki ya Dunia kanda ya Afrika Anne Kabagambe mara baada ya kuhitimisha
ziara katika shule ya sekondari kibasila iliyoko jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.