Ijumaa, 25 Julai 2014

AWAMU YA PILI KUCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO

Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili kwa wanafunzi waliobaki kutokana na ufinyu wa nafasi za shule za kidato cha tano, baada ya kubaini uwepo wa nafasi hizo; na baadhi ya wanafunzi wenye sifa watachaguliwa kwenda kusomea ualimu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa  Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  Bwana Jumanne Sagini alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari tarehe 22/07/2014  jijini Dar es salaam juu ya wanafunzi waliofaulu masomo ya sayansi.

Serikali kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi kusoma masomo hayo, imeendelea kuimarisha miundombinu ya shule kwa kutoa fedha za ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa majengo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kusoma masomo ya sayansi.

Bwana Sagini alisema wanafunzi ambao wamefaulu vizuri masomo ya sayansi na wanapenda kusoma masomo hayo wanayo fursa ya kubadilisha tahasusi (Combination) endapo zinapatikana kwenye shule walizopangwa kupitia kwa wakuu wao wa shule.  Iwapo tahasusi wanazozitaka hazifundishwi kwenye shule hizo wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa Maafisa Elimu Mikoa ambayo shule hizo zipo kupitia kwa wakuu wa shule walizopangiwa ili waweze kubadilishiwa tahasusi za sayansi kwenye shule zilizopo kwenye Mikoa husika.

“Jamii inaweza kuwasiliana na watendaji wa wizara na Mikoa kwa simu ambazo zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya waziri Mkuu- TAMISEMI. Hivyo, naendelea kuwasisitiza watendaji wote wa Elimu hususani Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu Mikoa kusimamia utekelezaji wa suala hili. Lengo la Serikali ni kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ili kuendana na Malengo ya Milenia na kutekeleza Mpango wa BRN.”alisema Katibu Mkuu.

Serikali inaendelea kusisitiza kila mwanafunzi kwenda kuripoti shule aliyopangiwa kuanzia tarehe 10-30 Julai, 2014, orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano mwaka 2014 inapatikana katika tovuti za www.pmoralg.go.tz na www.moe.go.tz

Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalamu katika fani za sayansi kwa kujiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa kila Mwanafunzi aliyefaulu masomo ya sayansi anapangiwa tahasusi ya masomo ya sayansi.

Katika matokeo ya mtihani kwa mwaka 2014, inaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 22,685 kati yao wasichana 7,859 na wavulana 14,826, wamechaguliwa kusoma tahasusi za sayansi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 18,746 kati yao wasichana 5,038 na wavulana 13,708 kwa mwaka 2013.

Uchaguzi wa wanafunzi kidato cha tano kwa mwaka 2014, ulifanyika mwezi mei, 2014 na matokeo yake kutangazwa kupitia tovuti ya OWM-TAMISEMI mwezi Juni 2014.Tofauti na miaka mingine iliyopita, Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I-III umeongezeka kutoka watahiniwa 35,357 mwaka 2012 hadi 71,527 mwaka huu. Ufaulu huu ni zaidi ya asilimia mia moja ya watahiniwa waliokuwa na sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka 2013.


Matokeo haya  yanakaribia sana malengo ambayo Serikali imejiwekea kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (yaani Big Results Now-BRN) ambapo serikali ilijiwekea lengo la kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa asilimia 60 mwaka 2013. Matokeo halisi yanaonyesha kuwa ufaulu umepanda kutoka asilimia 43 mwaka 2012 hadi asilimia 58.25 mwaka 2013.

Yapo manufaa mbalimbali ambayo yatapatikana kutokana na ufaulu huu wa wanafunzi kwa taifa na kwa wanafunzi husika. Kwa taifa ufaulu katika masomo ya sayansi utasaidia kupunguza uhaba wa wataalamu katika fani mbalimbali  za sayansi na pia unarahisisha kazi ya kuwapatia wanafunzi nafasi mbalimbali za kujiendeleza katika masomo ya ngazi ya juu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.