• Ataka
VETA kutumia mafundi wao kujenga Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi
vya Wilaya
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya
Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha wanatumia mafundi wao kujenga Vyuo 25 vya
Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vya Wilaya nchi nzima.
Waziri Ndalichako ametoa agizo
hilo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kutengeneza samani cha
Ufundi Stadi na Huduma Dodoma ambapo amesema haiwezekani VETA wakawa
wanafundisha kujenga lakini wao wakiwa na kazi za ujenzi wanatafuta mafundi
kutoka nje.
“Kama VETA mnafundisha kujenga
lazima tuone mnafanya kazi kwa vitendo sio mnataka kupaka rangi mnatafuta
mafundi wa mtaani nimesema marufuku nataka kuona hizi VETA 25 zinajengwa na
ninyi kwa kutumia mafundi wenu vinginevyo nifute mafunzo ya ufundi, “alisema
Waziri Ndalichako.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt John pombe Magufuli imeendelea kuviimarisha vyuo
vya mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha
vinatoa mafunzo bora na mafunzo ya kisasa ambayo yanaendana na
teknolojia ya kisasa na ndio maana inatumia fedha nyingi tena za walipa kodi
kuhakikisha inajenga kiwanda cha samani na kutoa wito kwa vijana kujiunga na
mafunzo ya useremala katika chuo hicho.
“Nimeambiwa hapa na Mwenyekiti wa
Bodi kwamba takwimu za wanafunzi wanaosoma mafunzo ya ufundi seremala bado ziko
chini lakini nipende kuwaambia ufundi seremala ni mzuri, kila mtu anahitaji
vifaa vya ndani hivyo ni kozi ambayo inalipa natoa wito kwenu vijana
kujiunga na mafunzo haya na
niwakaribishe katika Chuo chetu cha VETA
Dodoma ambacho kitakuwa na mafunzo ya kisasa kabisa,”aliongeza Waziri
Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Kiwanda cha Samani VETA Dodoma. |
Waziri Ndalichako ameupongeza
uongozi wa VETA kwa kuweza kubuni na kutekeleza mradi wa kiwanda cha kisasa na
kuwataka pamoja na kutoa mafunzo kuhakikisha wanakuwa na mpango mzuri wa uzalishaji
mali utakaotumia mashine za kisasa zilizofungwa katika kiwanda hicho.
“Baada ya kuzindua kiwanda hiki
nimekitembelea na kujionea namna kinavyoweza kufanya kazi kwa ufanisi,
kutengeneza bidhaa kwa muda mfupi ni ukweli usiopingika kwamba kimejengwa vizuri, naamini kitazalisha samani
za hali ya juu na kwa bei nafuu na kuondoa dhana kuwa samani nzuri mpaka zitoke
nje ya nchi,’aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akijaribu moja ya mashine katika kiwanda kipya cha samani cha VETA Dodoma. |
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Juma Nkamia
amesema katika nchi nyingi duniani vyuo vingi vinavyozalisha nguvu kazi ni vyuo
vya VETA na kuwataka vijana wanaosoma katika chuo hicho na wale walio nje ya
chuo hicho kutoa hamasa kwa watanzania kusoma kwenye vyuo vya VETA ili kupata
ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Peter Maduki amesema kiwanda hicho
kitaendelea kuzalisha samani kwa ubora na kulingana na soko na kwamba uwepo wa
Kiwanda hicho utasaidia kuongeza mapato yatakayotokana na uzalishaji wa samani
zenye ubora na gharama nafuu.
Maduki alimweleza Waziri kuwa
katika kufanikisha hilo watahakikisha wanaweka Menejimenti itakayoweza
kuendesha kiwanda hicho na kuona malengo yaliyowekwa yanafikiwa huku akimweleza
Waziri kuwa changamoto kubwa wanayoipata katika vyuo vya Veta ni kushindwa
kupata na wanafunzi wa kutosha wa fani ya useremala.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akitoa maelekezo wakati alipotembelea kiwanda cha samani cha VETA mara baada ya kukizindua rasmi. |
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)..Pancras Bujulu alimweleza Waziri
Ndalichako kuwa ujenzi wa kiwanda cha utengenezaji samani Dodoma umetekelezwa
kwa awamu mbili moja ikiwa ya ujenzi wa jengo na miundombinu yake na awamu ya
pili ikiwa ununuzi na ufungaji wa mashine na mitambo kazi zote zikigharimu zaidi ya shilingi bilioni 3 ambazo ni fedha
za ndani.
Hafla ya ufunguzi wa Kiwanda cha
kutengeneza samani VETA Dodoma imekwenda sambamba na mahafali ya 36 ya Chuo cha
Ufundi Stadi na Huduma Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalicho akielekea kwenye tukio la uzinduzi wa kiwanda cha Samani VETA Dodoma. |