Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa, Mwishoni mwa Wiki
amefunga Mafunzo ya Kuwajengea Uwezo Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu (SLOs)
na Maafisa Elimu Taaluma (DAOs) (Msingi Na Sekondari) Tanzania Bara Kuhusu
Kukabiliana na Majanga Katika Taasisi za Elimu, Yaliyofanyika ADEM - Bagamoyo
Kuanzia tarehe 19/05/2014 hadi 06/06/2014.
Mafunzo haya yalishirikisha jumla ya Maafisa Elimu
Vifaa na Takwimu na Maafisa Elimu Taaluma (Msingi na Sekondari) wapatao 636
kutoka Tanzania Bara. Maafisa hawa wanahusika moja kwa moja katika kusimamia
utekelezaji wa utoaji Elimu bora nchini katika ngazi ya halmashauri chini ya mkakati
mpya wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika sekta ya elimu.
Mafunzo haya yatawawezesha kusimamia utoaji wa elimu
bora shuleni na pia kutumia mbinu mbalimbali walizojifunza katika kuzuia na
kukabiliana na majanga yanapotokea katika maeneo yao. Maafisa hao wataweza
kutoa elimu kuhusu majanga kwa walimu, wanafunzi, viongozi na wadau wote wa
elimu katika halmashauri zenu. Aidha, Elimu waliyoipata itawawezesha pia kuwa
na uwezo wa kusimamia, kufuatilia na kuimarisha miundombinu shuleni na kuchukua
hatua za tahadhari zitakayowezesha kukabiliana na majanga, mbalimbali kama vile
umuhimu wa milango ya majengo ya shule kufungukia nje, kuwa na vifaa vya kuzima
moto na kuwa na visanduku vya huduma ya kwanza.
Shule zetu zimekuwa zikikumbwa na
majanga mbalimbali kwa mfano moto, mafuriko na vimbunga. Majanga haya yameleta
athari kubwa kwa maisha ya walimu na wanafunzi, katika majengo yakiwemo
madarasa, nyumba za walimu, maabara na vyoo. Samani za shule, vifaa vya
kufundishia na kujifunzia, barabara, huduma za maji na umeme, viwanja vya
michezo na mazingira yote ya shule yamekuwa yakiharibiwa na majanga.
Imeshuhudiwa moto ukiteketeza shule za Sekondari za Shauritanga, Idodi,
Morogoro n.k na kusababisha vifo kwa wanafunzi na kuharibika kwa miundo mbinu
ya shule. Pia tumeshuhudia mafuriko yakisababisha kutoendelea kwa masomo katika
Wilaya za Kilosa, Kyela, Ilala, Mvomero n.k mafuriko haya yalisababisha
shughuli za shule kukwama.
Serikali inaamini kuwa baada ya
mafunzo haya, washiriki wataweza kutimiza majukumu haya mapya kama ifuatavyo:
- kuunda Kamati za kukabiliana na Majanga Shuleni;
- kuandaa mipango kazi ya kukabiliana na majanga katika ngazi ya halmashauri na shule;
- kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo milango kufungikia nje, kuweka vizima moto (fire extinguishers), ndoo za michanga na kuboresha mazingira ya shule;
- kujenga uelewa wa pamoja wa namna ya kukabiliana na majanga miongoni mwa walimu, wanafunzi na jumuiya inayozunguka shule
- kujenga mtandao (network) wa kukabiliana na majanga kati ya shule na jumuiya inayozunguka shule;
- kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusu majanga shuleni; nakuandika taarifa sahihi kuhusu uwezekano wa kutokea majanga na madhara ya majanga shuleni mara yanapotokea.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.