Jumatano, 12 Februari 2020

WIZARA YAKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA NA VITABU KWA VYUO VYA UALIMU VYA SERIKALI 35 KWA AJILI YA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekabidhi vifaa vya TEHAMA na vitabu  kwa vyuo vya ualimu vya serikali 35 kwa ajili ya  kufundishia na kujifunzia.




Akikabidhi vifaa hivyo kwa mkuu wa Chuo cha Ualimu Patandi  jijini Arusha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard  Akwilapo  amewataka wakuu wa vyuo hivyo kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

"Vifaa tunavyovikabidhi leo ni vya gharama kubwa sana wito wangu kwa wakuu wa vyuo wote kuhakikisha wanavitunza vifaa hivi ili viweze tumika kwa muda mrefu na kuwanufaisha hata wanachuo watakaojiunga kwa miaka mingine" amesisitiza Katibu Mkuu.

Amesema pamoja na  kukabidhi vifaa hivyo na kutoa mafunzo kwa wakufunzi wa vyuo vya ualimu lengo kubwa ni kuimarisha na kuboresha mafunzo yanayotolewa kwa walimu tarajali ili wanapomaliza mafunzo yao wawe na mbinu bora
 za ufundishaji ambazo zitasaidia kuinua ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ave Maria Semakafu amesema utoaji wa vifaa hivyo ni juhudi za  makusudi zinazofanywa na wizara katika kutekeleza azma ya  kuboresha elimu nchini.

Kansela Mkuu, Ushirikiano na Maendeleo kutoka Canada Gwen Waimsley amesema nchi yake itaendelea kusaidia katika kuhakikisha walimu tarajali wanapata mafunzo bora ambayo yataleta tija katika ufundishaji na ujifunzaji katika shule za msingi na sekondari.

Gwen amesema nchi ya Canada inaamini kuwa walimu wanapoandaliwa katika mazingira mazuri ya kupatiwa mafunzo zoezi zima la utoaji elimu katika hatua zote linakuwa limefanikiwa.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ualimu Patandi.....  ameishukuru serikali kwa  kufanya mabadiliko makubwa katika vyuo vya ualimu vya serikali ambavyo vimekuwa na mabadiliko ya miundombinu na kupatiwa vifaa vingi vya kufundishia na kujifunzia

Mkuu wa chuo huyo amesema kama watendaji walioaminiwa katika kusimamia vyuo hivyo wana wajibu wa kusimamia vyuo hivyo na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa kwani mazingira yamekuwa rafiki kwa utendaji na ufundishaji.

Vifaa vilivyokabidhiwa katika vyuo hivyo ni pamoja na kompyuta mpakato 43, kompyuta za mezani 780, mashine za kudurufu 74 vitabu vya masomo ya kufundishia na vitabu vya kitaaluma  26,470 , projectors na vifaa vya kufundishia elimu maalumu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.