Mjumbe wa Baraza la
Ushauri wa Kisiasa la China (Chinese
Peoples Political Consultative Conference – CPPCC) Dkt.
Annie Wu amesema kuwa atatoa ufadhili wa nafasi za masomo kwa wanafunzi wa
Kitanzania kwenda kusoma elimu ya ufundi nchini China kwa lengo la kukuza na
kudumisha mahusiano mazuri yaliyopo kati
ya Tanzania na China.
Dkt. Wu amekuja nchini kwa
mwaliko rasmi wa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ambapo amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome ofisini kwake na kusema kuwa anatimiza
ahadi yake aliyotoa awali ya kusaidia kuinua Elimu ya Ufundi nchini.
Dkt. Wu alitoa ahadi ya ufadhili wa nafasi za
masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania kwenda kusoma elimu ya ufundi nchini China
wakati Profesa Mchome alipofanya ziara ya kikazi mwezi huu nchini China na
kukutana na kufanya mazungumzo na vingozi mbalimbali wa nchi hiyo wa namna ya kuimarisha uhusiano
uliopo kati ya Tanzania na China katika masuala ya elimu.
Kutokana na ufadhili huo uliotolewa na Dkt. Wu, Profesa
Mchome amesema ufadhili huo umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inaimarisha
elimu ya Ufundi ili kuwaandaa vijana katika kujiajiri wenyewe pindi
wanapomaliza masomo yao ya ufundi.
“Ni wakati sasa vijana wachangamkie fursa hii, wasome
masomo ya Ufundi ili wapate ufadhili na
hatimaye wanapomaliza masomo yao waweze kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa”
Alisema Profesa Mchome.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi
Dkt. Primus Nkwera amepokea ufadhili huo kwa
furaha na kuwataka wanafunzi kuchangamkia nafasi hizo zitakapotangazwa.
“Dkt. Wu ni mmoja kati ya marafiki wa Tanzania ambao
wanakuja mara kwa mara nchini na
kuhamasika na kujali Elimu ya Ufundi,
wengi wao hutoa vipaumbele katika elimu Msingi na Elimu ya Juu,” anasema Dkt.
Nkwera, anaendelea kusema pia ”Mahusiano ya Tanzania na China yametimiza miaka
50 hivyo kuja kwake kunaonyesha urafiki wa kweli tulio nao kati ya Tanzania na
China”.
Pamoja na kushika nafasi za juu katika Baraza la
Ushauri wa Kisiasa la China Dkt. Annie Wu ni mfanyabiashara ambaye amesaidia
kuanzishwa kwa Jumba la Sanaa (Culture House) lililoko Beijing ambalo pamoja na
mambo mengine jumba hilo linatumika kuuza vinyago kutoka kwa Wafanyabiashara wa
Tanzania.
Kuanzia
Jumatatu wiki Hii Tanzania itapokea ugeni kutoka nchini China utakaoongozwa
na Makamu wa Rais wa Nchi hiyo ambapo mambo mbalimbali yanayozihusu nchi hizi
mbili yatajadiliwa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.