Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru
Kawambwa ameiasa jamii kuchangia kuboresha elimu nchini kwa kutoa misaada
mbalimbali itakayosaidia kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi
mbalimbali za elimu.
Waziri Kawambwa alikuwa akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Vitabu
Airtel Shule Yetu 2014 jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambapo wawakilishi
wa shule za Sekondari 30 walipatiwa msaada wa vitabu vya
Sayansi na Hisabati na Kampuni hiyo.
Waziri Kawambwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
uzinduzi huo alisema
Mradi huu wa Vitabu Airtel
Shule Yetu utakuwa wa manufaa makubwa sana si kwa wanafunzi shuleni tu bali kwa sekta nzima ya Elimu
hapa nchini na kwa Taifa kwa ujumla.
“Sote tunatambua kwamba kitu pekee
kinachotofautisha nchi zilizoendelea na zinazoendelea siyo utajiri na mali walizonazo
bali ni elimu na ujuzi. Hii ni kwa sababu
utajiri na mali havijileti vyenyewe isipokuwa huchochewa na maendeleo mazuri yaliyo
jengwa katika msingi mzuri wa ELIMU. Kwa kadri kiwango cha elimu na ujuzi au
maarifa kinapokuwa juu katika nchi, ndipo na kiwango cha maendeleo ya nchi yanapozidi
kukua katika nchi hiyo,”alisema Dkt. Kawambwa.
Dhamira ya
Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ni kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Lakini hilo litawezekana tu kwa kupitia elimu.
Yaani kuwa na Taifa lililoelimika; lenye
wasomi wanaoweza kubaini na kutatua matatizo ya maendeleo ya nchi yetu. Na katika wakati huu tulionao, Sayansi na Tekinolojia vina nafasi ya pekee
katika maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii.
“Tunaishukuru
sana Airtel Tanzania kwa kutuunga mkono katika dhamira ya Serikali yetu ya kuwekeza
katika sekta ya elimu nchini. Airtel imekuwa
mstari wa mbele katika kuchangia vitabu pamoja na misaada mbalimbali kwa shule zetu
hapa nchini. Vitabu hivi vilivyochangiwa
na Airtel vitasaidia sana katika juhudi za Serikali za kuimarisha ubora wa
elimu inayotolewa,” alisema Waziri Kawambwa.
Hivi
sasa kuna uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule zetu za
Sekondari hapa nchini. Takwimu zinaonesha
kwamba hadi mwaka 2013/14 tulikuwa na upungufu wa walimu wa Sayansi na Hisabati
26,998. Lakini hata kule kwenye walimu wa masomo haya bado
kuna tatizo la uhaba wa vitabu. Lakini
kule ambako kuna uhaba wa walimu uwepo wa vitabu hivi utakuwa ni wa msaada sana
kwa wanafunzi kuweza hata kujisomea wenyewe.
Tukio hilo la Kampuni ya Airtel kukabidhi vitabu ni mwendelezo wa mambo mengi
ambayo yamekwishafanya katika kuisadia Sekta ya elimu nchini. Mradi huu ulianza miaka takriban kumi
iliyopita na katika kipindi chote hiki mradi umeweza kupeleka vitabu na vifaa
vya maabara katika shule mbalimbali na pia kufanya ujenzi na matengenezo katika
shule kadhaa hapa nchini.
“Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza makampuni mengine na Taasisi mbalimbali nchini kuiga mfano huu
wa Airtel na kusaidia sekta ya elimu ili kujenga taifa lililo bora. Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi,
Makampuni na asasi mbalimbali katika kuendeleza Elimu ya watoto na vijana wetu,”
alisema Waziri Kawambwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Airtel
Tanzania Sunil Colaso alisema kampuni yake itaendelea kuisaidia sekta ya elimu
ili kuchangia katika juhudi za serikali za kuboresha elimu hapa nchini ambapo
hadi hivi sasa shule za sekondari 1,000 zimefaidika kwa kupewa vitabu na kampuni
hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.