Jumanne, 2 Septemba 2014

NAIBU WAZIRI AWAAGIZA MAAFISA ELIMU KUWARUDISHA WANAFUNZI WATORO SHULENI


Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe.Jenista Mhagama amewaagiza Maafisa Elimu wote nchini kuhakikisha wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali wanarudi shuleni ili kuendelea na masomo.

Naibu Waziri alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki  wakati wa ziara yake mkoani Pwani kukagua miradi inayojengwa na Mpango wa Maendeleo  ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Elimu ya Sekondari (MMES). Shule zilizotembelewa ni Nyamisati, Mkamba na WAMA Nakayama zote zikiwa za sekondari na shule ya Msingi ya Mazoezi Vikindu, .

Aliwataka Maafisa Elimu  kufuatilia  sababu za utoro unaojitokeza shuleni na kuandika taarifa juu ya utoro huo na kutafuta njia za kupunguza utoro shuleni. Pia aliwataka Wakaguzi wa Shule wa Kanda pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kukagua ufundishaji na vigezo, ukaguzi unaofanyika sasa ujikite  katika kujibu hoja ya utoro wa wanafunzi katika shule. Alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shule kutoka Wizarani Bibi Hidaya Mohamed kutopokea ripoti zisizotoa uelekeo wa namna ya kuwarudisha watoto shuleni.
“Katika kila shule ambapo kutakuwa na utoro mkubwa wa wanafunzi Wakaguzi msipokee ripoti ya ukaguzi isiyotoa majibu kwanini wanafunzi katika shule zetu za msingi na sekondari wanaendelea kutoroka na ripoti ionyeshe hatua zilizochukuliwa kuwarudisha shuleni, mipango na mikakati ya kuhakikisha suala hili halijirudii ili kuwa na ubora wa elimu.” Alisema Mhe. Mhagama   

 Kuhusiana na maslahi ya Walimu Mhe. Mhagama alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga kuanzisha dawati la malalamiko litakalowawezesha walimu  kupeleka malalamiko yao  na kuwataka yafanyiwe kazi haraka iwezekanavyo. Alisema kuanzishwa kwa dawati hilo kutawapunguzia adha walimu ya kupoteza muda kufuatilia madai yao na badala yake watatumia muda huo kuwafundisha wanafunzi.
                                      
“Sitaki walimu hawa tunaowaleta huku wapoteze muda mwingi katika majengo ya Halmashauri kufuatilia madai yao kwani hawa ndio watumishi wengi kwenye Halmashauri hakikisheni mnawatengea dawati maalumu la kushughulikia kero zao.”Alisema Mhe.  Mhagama.






Maoni 1 :

  1. safi sana , kila mtu anahitaji elimu. by AMIDU EDSON mwandishi wa blog ya geographymaterials.blogspot.com

    JibuFuta