Alhamisi, 6 Aprili 2017

DKT AKWILAPO KATIBU MKUU MPYA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli leo amemuapisha Dkt Leonard Akwilapo kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia baada ya aliyekuwepo Maimuna Tarishi kuhamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu. Kufuatia uteuzi huo nafasi yake aliyokuwa akiishika katika Wizara hiyo kama Naibu Katibu Mkuu  imechukuliwa na Dkt Ave Maria Semakafu ambaye alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya  na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)

Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara hiyo mara baada ya kuapishwa Dkt Akwilapo amewataka wafanyakazi  kufanya  kazi  kwa bidii na weledi mkubwa ili kufikisha malengo ambayo tumejiwekea ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto za watanzania walio  wengi. Alisema Wizara ya Elimu ni Kubwa, nzito na ina mambo mengi pamoja na changamoto zake tutumie mbinu  tulizo nazo kuhakikisha tunatatua changamoto hizo bila matatizo.

 “ katika kutatua changamoto mara nyingi hapakosi kuleta kusigana hivyo tuvumiliane tufanye kazi kwa pamoja ili tuweze kutimiza malengo makubwa ya Wizara” alisisitiza Dkt Akwilapo

Dkt Akwilapo amesema anaamini katika Wizara ya Elimu ana azina ya kutosha kwa kuwa amekulia katika Wizara hiyo hivyo anaifahamu vizuri na anaamini uzoefu alionao utasaidia kutatua changamoto zilizopo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Ave Maria Semakafua amesema wafanyakazi wote tuwe na lengo moja la kusonga mbele katika kufanya kazi  na kutatua changamoto kwa pamoja kwani wizara ya Elimu  ni kubwa na changamoto zake  ni kubwa pia.  Amesema changamoto hizo zinaanzia katika makuzi na malezi, ili kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa sisi kama walezi  tuhakikishe tunafuatilia kwa ukaribu. Amesema yeye ni mwanaharakati amekuwa akipigania haki za watoto wa kike kuhakiksha wanapata elimu lakini sasa suala la elimu kwa watoto wote linatakiwa  kupiganiwa kwani wapo watoto wa kiume wanaopata changamoto zinazo haribu maisha yao na kukatiza masomo yao.


Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi Bwana Nicholaus Moshi kiongozi wa Chama cha Walimu tawi la Wizara ya Elimu amesema tunawapongeza kwa nafasi walioshika kwani wameteuliwa kati ya watanzania wengi kuweza kuongoza Wizara hiyo na kwamba  tunaahidi kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kutimiza malengo ya watanzania walio wengi kwenye elimu ya watoto wao.

Maoni 1 :

  1. Je wizara imepanga kubadilisha mtaala? Kwa wadau wengi anaona mtaala uliopo hauendani na mabadiliko ya jamii. Je kama wizara inasema nini juu ya hilo?

    JibuFuta