JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
KATAZO LA KUONGEZA ADA KWA SHULE ZISIZO ZA SERIKALI KWA MWAKA WA MASOMO
2016
Waraka
wa Elimu Na. 4 wa Mwaka 2008 uliweka viwango vya ada vinavyotozwa katika shule
za Msingi na Sekondari za Serikali na zile zisizo za serikali. Ada iliyowekwa
kwa shule za kutwa zisizo za serikali ni Tsh. 150,000/= na shule za bweni Tsh. 380,000/=
kwa mwaka kwa kila mwanafunzi. Aidha waraka huo ulielekeza kwamba ongezeko
lolote la ada lazima lipate kibali cha Kamishna wa Elimu kabla ya kuanza
kutumika.
Hata
hivyo imegundulika kuna baadhi ya shule zisizo za serikali zimekuwa zikiongeza
ada kila mwaka pasipo kupata kibali cha Kamishna wa Elimu. Utamaduni huu wa
kuongeza ada kila ifikapo mwishoni mwa mwaka umekuwa ukisababisha usumbufu
mkubwa kwa wazazi/walezi na hata baadhi yao kushindwa kuendelea kusomesha
vijana wao katika baadhi ya shule.
Kwa
tangazo hili wamiliki wote wa shule zisizo za serikali wanaagizwa kufanya
yafuatayo:
1.
Kutokuongeza gharama za
uendeshaji wa shule zikiwemo ada kwa mwaka wa masomo unaoanzia mwezi Januari
mwaka 2016 mpaka watakapopata maelekezo kutoka kwa Kamishna wa Elimu; wale
ambao tayari wameongeza gharama na ada kwa mwaka wa masomo wa 2016 bila kibali
cha Kamishna wa Elimu, Wizara haitambui ongezeko hilo kwa kuwa ni batili na
hivyo zimefutwa.
2.
Ada zote kwa shule zisizo
za serikali zitabaki kama zilivyokuwa zimeidhinishwa na Kamishna wa Elimu.
3.
Kuwasilisha taarifa kwa
Msajili wa Shule aliyepo Idara ya Ithibati ya Shule inayoeleza kiasi cha ada na
gharama kinachotozwa kwa sasa (kabla ya
mwaka wa masomo 2016) na tarehe shule ilipopata kibali kutoka kwa Kamishna wa
Elimu kutoza kiwango hicho cha ada. Taarifa hiyo ifike ndani ya wiki mbili kuanzia
tarehe ya tangazo hili.
Wathibiti
ubora wa shule waliopo sehemu mbalimbali nchini wanaagizwa kulifuatilia suala
hili kwa karibu ili kila shule itekeleze agizo hili na kutoa taarifa
zilizoelekezwa katika tangazo hili. Hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wamiliki
ambao hawatatekeleza maagizo haya.
Aidha
Wizara iko katika hatua za mwisho za utafiti na kuandaa mfumo wa kielektroniki
wa kutambua gharama za kumsomesha mwanafunzi katika elimumsingi (elimu ya
awali, msingi na sekondari) na hivyo wadau mbalimbali watoe ushirikiano kwa
timu za wataalamu wanaofanya kazi hii ili kusaidia katika kuukamilisha mfumo na
hatimaye kuwa na ada elekezi katika maeneo mbalimbali.
IMETOLEWA
NA KATIBU MKUU