Serikali
ya Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imefanikiwa kuimarisha
usimamizi na udhibiti wa matumizi ya Teknolojia ya Nyuklia nchini.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekenolojia Mheshimiwa William
Ole Nasha wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa kimataifa wa waratibu wa miradi ya Sayansi
na Teknolojia ya Nyuklia kutoka nchi 46 wanachama wa Shirika la Kimataifa la Nguvu
za Atomiki (IAEA) unaofanyika jijini Arusha.
Naibu
Waziri Ole Nasha amesema Shirika hilo linafadhili miradi mingi katika sekta mbalimbali
hapa nchini ikiwemo sekta ya afya ambapo imewezesha kupatikana kwa vifaa mbalimbali
vya uchunguzi wa tiba na maradhi ya saratani ambavyo vimefungwa katika hospitali
ya Rufaa ya kanda ya ziwa, Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Ocean Road jijini
Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe William Ole Nasha (Kushoto)
akifurahia jambo na Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki,
Profesa Shaukat Abdulrazak katika Mkutano huo.
|
Pamoja
na vifaa vya uchunguzi katika hospitali hizo mbili, pia taasisi nyingine mbalimbali
zimepata vifaa vya maabara ambapo kwa ujumla wake vifaa vyote vina thamani ya kiasi
cha Shilingi za Tanzania Bilioni 6.2 na pia kutoa mafunzo kwa wataalamu katika eneo
la matumizi ya mionzi na teknolojia ya Nyuklia, mpango ambao uligharimu Shilingi
za Tanzania Bilioni 3.3.
Mhe
Ole Nasha amelishukuru na kulipongeza shirika hilo kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano
baina ya mataifa wanachama hususan kwa utaratibu wake wa kuwa na mikutano inayowezesha
kubadilishana uzoefu baina ya wanachama. Amewataka washiriki wa mkutano huo kuhakikisha
wanafanya majadiliano yenye tija kwa lengo la kusaidia nchi zao kwenye udhibiti
na matumizi salama ya teknolojia ya Nyuklia.
“Majadiliano
yenu yalenge katika kuhakikisha mionzi na teknolojia ya Nyuklia katika Afrika inatumika
vizuri kwa maendeleo,” alisema Ole Nasha.
Mheshimiwa
Naibu Waziri ametumia nafasi hiyo pia kuwakaribisha sana washiki nchini
Tanzania na kuwashauri kutembelea vivutio vya kitalii zikiwemo Mbuga za wanyama.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA), Profesa Shaukat
Abdulrazak amesema wataendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha
kunakuwa na matumizi salama ya teknolojia ya Nyuklia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo
sekta ya Afya, Kilimo, Mifugo, Maji, Viwanda na Ujenzi.
Nae
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Profesa Lazaro Busagala amesema taasisi yake imeendelea kudhibiti na kuwachukulia hatua
za kuwafungia taasisi zinazokiuka taratibu za matumizi salama ya mionzi na teknolojia
ya Nyuklia hapa nchini ikiwemo kutokuwa na leseni, kutokuwa na wafanyakazi wenye
utaalamu wa matumizi ya mionzi na teknolojia ya Nyuklia na Mionzi.
Akitoa
mfano wa Hospitali amesema mwaka 2018 walifungia hospitali 112 zilizoshindwa kufuata
masharti hayo, katika hizi tayari hospitali 40 zimekidhi na kufunguliwa huku hospitali
72 zikiwa bado zimefungiwa kutumia vifaa vinavyotumia mionzi.
Mkutano
huo wa siku tano utamalizika tarehe15 Machi, 2019.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.